Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewapongeza Waislamu wote kwa kuhitimisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na kuwasihi mafunzo yote waliyoyapata wakati wa mfungo kuyaendeleza kwa manufaa yao na Taifa zima kwa ujumla.
Mhe. Rais Samia amesema hayo leo tarehe 14 Mei, 2021 wakati akihutubia katika Baraza la Idi lililofanyika Kitaifa katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Amefafanua kuwa pamoja na kumcha Mwenyezi Mungu, Waislamu na Waumini na Madhehebu mengine ya Dini wanapaswa kuendelea kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa, na kwa wafanyabiashara kulipa kodi kama inavyostahili ili kuiwezesha Serikali kutoa huduma mbalimbali za kijamii ambazo ni pamoja na afya, maji na elimu.
Mhe. Rais Samia amemshukuru Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Aboubakar bin Zubeir bin Ally Mbwana kwa kuunga mkono juhudi za kukuza uchumi na ametoa wito kwa Madhehebu mengine ya Dini kuunga mkono juhudi hizo kwa kuanzisha shughuli za uzalishaji mali.
Kuhusu salamu za Baraza Kuu la Wasilamu Tanzania (BAKWATA) zilizosomwa na Katibu Mkuu wa BAKWATA Ustaadhi Nuhu Jabir Mruma, Mhe. Rais Samia amesema Serikali ina dhamira ya dhati ya kuendeleza na kukuza uhuru, haki, demokrasia na utawala bora na ametoa wito kwa viongozi wa Dini kutoa ushirikiano.
Ametoa wito kwa viongozi hao kuendelea kusimamia malezi na maadili bora ya vijana na pia ametoa wito kwa Waumini wa Madhehebu yote ya Dini nchini kuendelea kuheshimana na kuvumiliana ambayo ni moja sifa kubwa za Tanzania.
Kuhusu janga la ugonjwa wa Korona, Mhe. Rais Samia ameungana na viongozi hao kutaka Watanzania waendelee kuchukua tahadhari kama zinavyoelezwa na wataaluma na amewatoa hofu kuwa Serikali itaendelea kuchukua tahadhari zote zinazotakikana ikiwemo vifaa vinavyoletwa nchini kwa ajili ya kukabiliana na janga hilo na kama itaamua kuruhusu ama kutoruhusu chanjo.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa BAKWATA Bi. Shamim Khan na viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Mhe.Rais Samia ameondoka Jijini Dar es Salaam na kwenda Zanzibar kwa mapumziko ya sikukuu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇