LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 15, 2021

RAIS SAMIA AFANYA UTEUZI WA MA-RC, YUMO KAFULILA, MAKALLA ATUA DAR, IBUGE APEWA MIKOBA YA MNDEME RUVUMA

Rais Samia Suluhu Hassan


Ikulu, Zanzibar
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan  amefanya uteuzi wa Wakuu wa Mikoa na Watendaji Wakuu wa Taasisi.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu leo Jumamosi, Mei 15, 2021, kutokea Zanzibar, imesema:-

Aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Simiyu Anthony John Mtaka ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Sinyanga Zainab Rajab Telack kuwa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, kuchukua nafasi ya Godfrey Zambi ambaye amestaafu.

Taarifa imesema, aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Geita Robert Gabriel Luhumbi ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, huku aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Katavi Juma Zuberi Homera akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mbeya.

Pia aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Tanga Martin Reuben Shigella ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro na anachukua nafasi ya Loata Erasto Ole Sanare ambaye amemaliza muda wake.

Taarifa imesema, aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Kagera Brig. Jen. Marco Elisha Gaguti ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara na anachukua nafasi ya  Gelasius Gasper Byakanwa ambaye atapangiwa majukumu mengine na Albert Chalamila aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Mbeya kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Pia Rais amemteua aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Aboubakar Mussa Kunenge kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani na anachukua nafasi ya Mhandisi Evarist Welle Ndikilo ambaye amestaafu huku Rais akimteua aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Manyara Joseph Joseph Mkirikiti kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kuchukua nafasi ya Joachim Leonard Wangabo ambaye amestaafu.

Naye aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk. Binilith Satano Mahenge ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Singida kuchukua nafasi ya Dk. Rehema Nchimbi ambaye amestaafu huku aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Tabora Dk. Philemon Rugumiliza Sengati akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.


Taarifa imesema, aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Mwanza John Vianney Mongella amekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu na aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Salim Hapi akipelekwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, naye Adam Kigoma Malima akitoka kuwa Mkuu wa mkoa wa Mara na kwenda kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga.


Katika uteuzi huo, Kada wa CCM David Zacharia Kafulila Rais amemteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha akichukua nafasi ya Idd Hassan Kimanta ambaye amestaafu. Kafulila ameshika wadhifa huo ikiwa ndiyo mara yake ya kwanza.


Pia aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Katavi zamani Amos Gabriel Makalla ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, akichukua nafasi ya Aboubakar Mussa Kunenge ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani.


Taarifa imesema, Rosemary Staki Senyamule ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kuchukua nafasi ya Robert Gabriel Luhumbi ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, huku Queen Cuthbert Sendiga akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa kuchukua nafasi ya Ali Salim Hapi ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa Tabora.


Na Mej. Jen. Charles Mbuge ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera kuchukua nafasi ya Brig. Jen. Marco Elisha Gaguti ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, huku Mwanamvua Mrindoko akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi kuchukua nafasi ya Juma Zubeir Homera ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.


Taarifa imesema, Katibu wa Bunge Stephen Kagaigai ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kuchukua nafasi ya Anna Elisha Mghwira ambaye amestaafu, huku Brig. Jen. Wilbert Augustine Ibuge akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma kubeba mikoba ya Christine Mndeme ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).


Pia Rais amemteua Omary Tebweta Mgumba kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe kuchukua nafasi ya Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ambaye amestaafu, naye mtoto wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, Makongoro Nyerere akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara kuchukua nafasi ya Mkirikiti ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.


Taarifa imesema, Mkuu wa mkoa wa Kigoma wa sasa Thobias Emir Andengenye ameteuliwa na Rais kuendekea kuwa Mkuu wa Mkoa huo wa Kigoma, huku Marwa Mwita Rubirya akiteuliwa kuendelea kuwa Mkuu wa Mkoa aliopo sasa wa Njombe.


Katika Uteuzi wa Watendaji Wakuu wa Taasisi, Taarifa imesema Rais amemteua Balozi Joseph Edward Sokoine kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. kuchukua nafasi ya Mej. Jen. Ibuge ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.


Rais pia amemteua Nenelwa Mwihambi kuwa Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchukua nafasi ya Stephen Kagaigai ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro. 


Pia Dk. Edwin Paul Mhede ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) kuchukua nafasi ya Mhandisi Ronald Muberwa Lwakatale ambaye uteuzi wake umetenguliwa, huku Sylvester Antony Mwakitalu akiteuluwa kuwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuchukua nafasi ya Biswalo Mganga ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu.


Taarifa imese, Rais amemteua Joseph Pande kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka (DDPP) kuchukua nafasi ya Edson Athanas Makallo ambaye atapangiwa majukumu mengine.


Rais amemteua pia Kamishna Msaidizi wa polisi (ACP) Salum Rashid Hamduni kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuchukua nafasi ya Mej. Jen. John Mbungo ambaye atapangiwa majukumu mengine. Pamoja na uteuzi huo Rais Samia amempandisha cheo ACP Hamduni kuwa Kamishna wa Polisi (CP) na pia Rais amemteua Neema Mpembe Mwakalyelye kuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.


Taarifa ya Ikulu imemalizia kwa kueleza kuwa Uteuzi wa viongozi hao unaanza leo tarehe 15 Mei, 2021 na wataapishwa tarehe 18 Mei, 2021 kuanzia saa 9:00 alasiri, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages