Bodi ya Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE) imemkaribisha Rais mstaafu wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete kuwa Mwenyekiti mteule wa Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Shule ya Uchumi na Sayansi ya Siasa ya London, Dk. San Liautaud kuwa, Makamu Mwenyekiti mteule.
Dk. Kikwete na Makamu wake wanatarajia kuanza kutekeleza rasmi majukumu yao Septemba 15, 2021.
Uthibitisho wa Dk. Kikwete umeonyesha umuhimu ambao GPE inaweka juu ya uongozi wa nchi washirika na ushiriki.
Katika kipindi chote cha utumishi wa Dk Kikwete, katika serikali ya Tanzania na mashirika ya kimataifa na ya kikanda, alijitolea kuendeleza sera zinazoendelea za elimu na afya ya wanawake na watoto.
Mwenyekiti wa Bodi ya GPE na Waziri Mkuu wa zamani wa Australia Julia Gillard amewakaribisha viongozi hao wawili na kueleza namna alivyofurahishwa na uteuzi wao.
"Nimefurahi kuwakaribisha Dk. Jakaya Kikwete na Dk. Susan Liautaud sote tunafahamu kuwa Dk. Kikwete ni kiongozi anayeheshimika juu ya elimu na afya ya umma barani Afrika na kwingineko, ambaye uzoefu na taaluma yake ya utumishi wa umma itasimamia kazi ya GPE katika miaka ijayo lakini pia ustadi mkubwa wa Dk. Liautaud katika utawala na maadili utaimarisha mfano wa ushirikiano wa GPE kwa faida ya mamilioni ya watoto ulimwenguni, " amesema.
Kwa upande wake Dk. Kikwete amesema, “Ninaamini hakuna mabadiliko makubwa zaidi ambayo kiongozi anaweza kufanya ili kutumikia watoto walio katika mazingira magumu na waliotengwa zaidi ya elimu. Nimeheshimiwa kuongoza Bodi ya Ushirikiano wa Kimataifa wa Elimu, shirika ambalo linajishughulisha na kushughulikia shida ya kujifunza ambayo imezidishwa na janga la corona," amesema Kikwete.
Naye Makamu Mwenyekiti mteule wa bodi hiyo, Susan Liautaud amesema "Elimu ni ufunguo wa kutatua changamoto nyingi sana ulimwenguni kutoka kwenye haki za binadamu na afya hadi kufikia malengo ya maendeleo endelevu na kutokomeza viwango visivyokubalika vya ukosefu wa usawa ulimwenguni.
Nimeheshimiwa kuchukua jukumu hili la Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya GPE," amesema.
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇