Na Mwandishi Maalum
Mpanda-KATAVI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Profesa Sifuni Mchome, ametoa ahadi ya kuchangia shilingi milioni tano ukiwa ni mchango wake wa kusaidia kukamilisha Zahanati ya Jeshi la Polisi Wilayani Mpanda, Mkoani Katavi.
Afisa Mkuu wa Nawasiliano ya Umms Wizara y Sheria na Katiba, Maura Mwingira, amesemsa Katibu Mkuu ametoa mchango huo baada ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi ACP Benjamin E. Kuzuga kuelezea kwamba, Jeshi la Polisi Mkoani humo limekamilisha ujenzi wa Zahanati yake, lakini bado haijaanza kutoa huduma kutoka na ukosefu wa vifaa tiba, madawa na samani.
Aidha Kamanda Kuzunga alieleza kwamba kama Zahanati hiyo ingeanza kutoa huduma basi pia kituo cha mkono kwa mkono ( one stop center) ambacho pamoja na mambo mengine kingeweza kutoa huduma na faragha kwa akina mama na watoto wahanga wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Hayo yamejili wakati wa kikao kilichofanyika mwishoni mwa wiki wilayani Mpanda , Mkoani Katavi kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria , Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na baadhi ya Maafisa na Askari wa Jeshi la Polisi mkoani Katavi. Kikao hicho kilichofanyika katika Bwalo la Polisi kilikuwa ni cha kubadilishana mawazo kuhusu hali ya utoaji wa Hakijinai kwa upande wa Jeshi la Polisi.
“Changamoto moja kubwa ni ya kutokuwa na kituo cha mkono kwa mkono ( one stop center) kutoka na kutokuanza kufanya kazi kwa Zahanati yetu ambayo ujenzi wake umetokana na michango ya askari na maafisa na kuchangiwa pia na Mkuu wa Jeshi la Polisi ( IGP) na baadhi ya wadau wengine, hata hivyo jengo limeshindwa kuanza kazi kutokana na kutokuwa na vifaa tiba, madawa na samani” akasema ACP Kuzunga.
Amebainisha kwamba ujenzi wa Zahanati umegharimu takribani shilingi Milion 70. Na kwamba zinahitajika shilingi milioni 24 kwaajili ya ununuzi wa vifaa tiba na mambo mengine na tayari wameshanunua baadhi ya vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 3.
“Katika hili la Zahanati, kwanza niwapongeze kwa juhudi zenu hizi, basi mimi nitachangia shilingi Milioni Tano ili zisaidie mambo fulani fulani kwasababu jambo mmlilolibuni ni jema” akaahidi Katibu Mkuu Profesa Mchome.
Katibu Mkuu Profesa Sifuni Mchombe akiambatana na Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii , Jinsia, Wazee na Watoto, walipata fursa ya kuitembelea Zahanati hiyo wakiongowa na Kamanda wa Polisi ambaye aliwaeleza kwamba, Zahanati hiyo ina vyumba vya madaktari vitatu, chumba cha maabara, chumba cha kuhifadhia dawa na chumba wa akina Mama na chumba cha watoto.
Kuhusu upatikanaji wa madaktari, Kamanda ACP Benjamin Kuzuga amesema Mganga Mkuu wa Mkoa pia ameahidi kuangalia uwezekano wa kusaida katika eneo hilo.
Wakati Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria Profesa Mchombe akiahidi kutoa milioni Tano, kwa upande wake Katibu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. John Kingu ameahidi kuisaidia zahanati hiyo gari pamoja na vifaa vingine ili hatimaye zahanati iweze kuanza kazi haraka iwezekanavyo.
Awali Katika kikao hicho cha Makatibu Wakuu na Maafisa na Askari wa Jeshi la Polisi ,RPC pia alielezea ukosefu wa majengo ya Kituo vya Polisi karibu katika wilaya zote za mkoa huo pamoja na ukosefu wa nyumba za askari .
Akasema hata Ofisi yake ipo katika Jengo ambalo ni Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Mpanda.
“Waheshimiwa Makatibu Wakuu, kwa kuwa Mkoa huu ni mpya, tunashida sana ya Majengo ya Vituo vya Polisi , hata askari wetu wanaishi uraiani ama katika nyumba za kupanga au walizojenga wenyewe. Kiutendaji wa majukumu yetu hali hii si salama sana, kwa sababu ikitokea dharura tu itakuwa shida sana kukutana na kukusanyika mara moja. Na ndiyo maana kiutaratibu askari wanatakiwa kuishi kambini ili kukitokea dharura yoyote inakuwa rahisi kuwasiliana” .
Aidha RPC Kuzuga pia ameeleza kwamba hali hiyo ya kutokuwa na Vituo vya Polisi kumepelekea kutokuwapo kwa vyumba maalumu vyenye mazingira mazuri ya kusikiliza na kuchukua maelezo ya wahanga waliohujumiwa kijinsia na kwamba katika baadhi ya maeneo imebidi askari na wahanga hao kukaa chini ya miti ili kuchukua maelezo yao au kuwapatia huduma nyingine stahiki.
Wakati huo huo Katibu Mkuu Profesa Mchome, amesema Jeshi la Polisi ni sehemu ya mnyororo wa mchakato wa kuijenga Tanzania iliyobora na wananchi wake kutekeleza majukumu yao bila hofu na hivyo kujiletea maendeleo yao binafsi na maendeleo ya taifa lao.
Na kwa sababu hiyo, amelitaka Jeshi la Polisi Mkoani Katavi, kama chombo cha utoaji wa HakiJinai kutekeleza majukumu yake kwa weledi, kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu ambazo Jeshi hilo limejiwekea pamoja na Sheria za Utumishi wa Umma.
Akasema Jeshi la Polisi pamoja na changamoto mbalimbali bado limeweza kutekeleza majukumu yake ya utoaji Hakijinai, na akalitaka kutumia sheria ya ufifishaji wa makosa hasa yale makosa madogomadogo ambayo yanaweza kuishia au kumalizwa katika Kituo cha Polisi na hivyo kujipunguzia wenyewe mzingo wa mafaili ya upelelezi lakini kuvisaidia pia vyombo vingine vya utoaji hakijinai mzigo wa kuendesha mashataka na kesi na mlundikiano wa wafungwa na mahabusu.
Amebainisha kwamba, katika mnyororo wa utoaji Hakijinai, Serikali ya awamu ya Sita ambayo inaongozwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan imeelekeza mambo ya kutekeleza na Jeshi la Polisi kama sehemu ya Serikali mnaowajibu pia wa kuyatekeleza.
Akayataja baadhi ya mambo hayo kuwa ni pamoja na kutenda haki kwa kila kosa na kwa weledi, uadilifu, kujiamini kuwajibika na kwa mujibu wa kanuni, sheria na taratibu na kumaliza baadhi ya mashauri kwa njia ya upatanishi na utoaji wa adhabu mbadala badala ya kukimbilia mahakamani pasipo ulazima wa kufanya hivyo, mahakama iwe chombo cha mwisho kabisa.
“Ujumbe wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hasani kuhusu eneo la utoaji haki katika maeneo mbalimbali ni kutenda haki, tusimbambikie watu kesi, anataka haki itendeke kwa wakati na kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu, Jeshi la Polisi ni sehemu ya mnyororo wa utoaji wa haki lakini pia mnao mchango mkubwa sana katika kuijenga nchi yetu kiuchumi” akasisitiza Katibu Mkuu Mchome.
Akalipongeza pia Jeshi hilo la Polisi kwa kazi nzuri inayofanya kupitia Dawati la Jinsia, Dawati ambalo limekuwa kimbilio na faraja wahanga wa matukio mbalimbali hasa ya udhalilishaji wa kijinsia wanaotafuta haki zao.
Makatibu Wakuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wapo katika Ziara ya Kikazi ya Kawaida ambayo imewafikisha katika Mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi na katika mikoa hiyo yote Makatibu Wakuu hao wamekuwa na vikao mbalimbali na Wadau wa Mnyororo wa Utoaji Hakijinai na Watumishi wa Serikalini
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇