KATIKA jitihada za kukabiliana na tatizo la mmomonyoko wa maadili kwa vijana,wazazi na walezi wilayani kahama mkoani Shinyanga wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika malezi ya watoto wao ili kuwaanda kuwa viongozi wa baadae watakaolisaidia taifa katika ujenzi wa uchumi.
Kauli hiyo imetolewa leo na mjumbe wa halmashauri kuu ya taifa ya chama cha mapinduzi (CCM), Suleiman Juma Kimea (MNEC) kupitia jumuia ya wazazi taifa wakati akizungumza na wazazi na walezi kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya wazazi wilayani humo.
Amesema kuwa jukumu la malezi ya vijana ni la wazazi,walezi hivyo ni budi likasimamiwa kikamilifu ili kuleta tija na kuliepusha taifa na vijana wasiokuwa na maadili ambao wamekuwa wakishindwa kufikia malengo yao kutokana na kujiingiza katika makundi yasiyokuwa na staha kwenye jamii.
“Jumuia ya wazazi taifa mwaka huu tunaadhimisha wiki maalum ya wazazi kwa kanda mbalimbali,ili kuwakumbusha wazazi kuhusiana na jukumu la malezi ya vijana,ili taifa liwe na vijana wazalendo na wanaoipenda nchi yao,”alisema Kimea.
Amefafanua kuwa vijana kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya ama ngono katika umri mdogo huchangiwa na kukosekana kwa malezi bora kwenye ngazi ya familia na jamii hivyo ni budi kulidhibiti suala hilo haraka ili kuwapatia fursa za kuzitambua mila na desturi za kitanzania.
Nae mwenyekiti wa jumuia ya wazazi mkoa wa shinyanga, Alhaj Salim Abdala Simba amesema kuwa watahakikisha wanawakumbusha wazazi kuhusiana na wajibu wao wa malezi kwa vijana ili kuzuia tatizo la kuporomka kwa maadili kwenye jamii.
“Jumuia yetu ndio yenye jukumu la kusimamia malezi ndani ya chama hivyo tutahakikisha tunayatekeleza maagizo ya viongozi wetu wa kitaifa ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na vijana wenye malezi bora,”alisema Simba.
Kwa upande wake mwenyekiti mstaafu wa (CCM) mkoa wa Shinyanga Hamis Mgeja amesema kuwa wazazi hususani wanaume wanajitoa kwenye jukumu la malezi ya watoto na kuwaachia akinamama hali ambayo wengi wao huwashinda.
“Wanawake wanaachiwa jukumu la kulea baba hana muda katika malezi hali hii husababisha watoto kukosa malezi ya pande zote hali ambayo husababisha kuujingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na ngono nzembe,”alisema Mgeja.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇