Rais Joe Biden wa Marekani amelalamikia vikali mashambulizi ya silaha moto na mauaji ya kiholela nchini humo na ametaka uhalifu huo ukomeshwe mara moja. Amesema, mashambulizi ya silaha moto Marekani ni sawa na ugonjwa wa kuambukiza na ni aibu kwa nchi hiyo kimataifa.
Rais huyo wa Marekani alisema hayo Alkhamisi wakati akitangaza amri 6 za utekelezaji za kukabiliana ma machafuko ya kutumia silaha na kuhimiza amri hizo zipasishwe kuwa sheria.
Alisema, watu 316 wanapigwa risasi nchini Marekani na 106 wanauawa kwa risasi kila siku nchini humo. Biden amesema: "Bendera yetu ilikuwa ndio kwanza inapepea nusu mlingoti kutokana na ukatili wa kuuliwa Wamarekani 8 wenye asili ya Asia huko Georgia, ghafla moja watu wengine 10 wamepigwa risasi na kuuawa kwa umati huko Colorado." Ameongeza kuwa, katika matukio hayo mawili na kwenye kipindi cha wiki moja tu, zaidi ya kesi 850 za ufyatuaji risasi zimeripotiwa nchini Marekani na watu 250 wameuawa na 500 wengine wamejeruhiwa katika matukio hayo.
Sasa hivi kuna mgogoro mwingine umeongezeka katika uhalifu wa utumiaji silaha kiholela huko Marekani, nao ni mgogoro wa silaha zisizoonekana, yaani silaha za kutengeneza kienyeji ambazo hazina nambari za serikali. Hivyo hata kama kutawekwa sheria kali za kupiga marufuku kununua silaha katika maduka rasmi, lakini silaha zisizoonekana zitakuwa hazidhibitiki.
Kiujumla ni kwamba mgogoro wa mauaji ya kiholela na utumiaji silaha moto una historia sawa na ya kuasisiwa nchi ya Marekani. Uhuru wa kutembea na silaha katika nchi kubwa ya kibepari duniani, umekuwepo muda wote tangu kuundwa nchi hiyo na unachangia sana uhalifu na mauaji ya kiholela katika jamii ya Marekani.
Ni kwa sababu hiyo ndio maana mara kwa mara kunaripotiwa mauaji ya umati na ya kiholela nchini humo. Miongoni mwa visingizio vinavyotumiwa na wahalifu hao ni ima kukata tamaa ya maisha, ugomvi wa kifamilia, masuala ya kazi, kuathiriwa na filamu za mauaji na ukatili pamoja na michezo ya kompyuta. Mara kwa mara utaona kunaripotiwa mtu kubeba silaha na kufanya mauaji ya umati katika maeneo ya uma tena bila kisisi nchini humo. Tab'an kuna uhalifu mkubwa zaidi ya huo unaotokea kila siku huko Marekani nao ni ule wa magenge ya wahalifu na wafanya magendo ya madawa ya kulevya ambao wanaongeza kwa kiwango kikubwa mauaji ya kiholela ya kutumia silaha moto huko Marekani.
Agnès Callamard, Mkurugenzi Mkuu wa Amnesty International amesema: Serikali ya Marekani haitekelezi jukumu lake la kulinda haki ya kuishi wananchi wake kama zinavyosema sheria za kimataifa za kuzuia machafuko na uhalifu wa kutumia silaha.
Takwimu rasmi zilizotolewa na serikali ya Marekani kuhusu mauaji ya silaha za moto pamoja na watu kujiua zinaonesha kuwa, mwaka 2020 zaidi ya watu 43,000 walipoteza maisha yao kwa njia hizo huko Marekani.
Ripoti ya tovuti ya "uhalifu wa silaha" ya Marekani inaonesha kuwa, mashambulizi ya kiholela ya silaha moto nchini Marekani yaliongezeka kutoka 417 mwaka 2019 hadi 611 mwaka 2020. Aidha takwimu za hivi karibuni kabisa zinaoensha kuwa Wamarekani 4,000 wameshauawa kwa kupigwa risasi tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2021 hadi hivi sasa.
Serikali ya Barack Obama ilijaribu sana kuzifanyia marekebisho sheria za kubeba silaha huko Marekani, lakini serikali iliyoingia madarakani baadaye yaani ya Donald Trump ilikwenda mkondo mwingine kabisa na iliunga mkono uhuru wa kubeba silaha mitaani huko Marekani. Aidha, wamiliki wa viwanda vikubwa vya kutengeneza silaha na wenye ushawishi kila mahali hasa katika Baraza la Congress hawaruhusu kabisa kubanwa uhuru wa kubeba silaha kiholela nchini humo.
Muda wote wabunge wa chama cha Republican wamekuwa wakipinga vikali juhudi za wabunge wa chama cha Democratic za kufanyia marekebisho sheria za kubeba silaha nchini humo.
Hata hivyo wananchi wa Marekani wanazilalamikia serikali na Baraza la Congress kwa kutojali roho zao na kukwamisha juhudi za kudhibiti umilikaji silaha kiholela ambao kimsingi ndiyo sababu kuu ya mauaji ya mfululizo ya umati na ya kila siku katika jamii ya Marekani, dhidi ya watu wasio na hatia.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇