Na Asteria Muhozya na Steven Nyamiti, Dodoma
Kiswahili kimekubalika kuwa moja ya Lugha ya Mawasiliano zitakazotumika katika Umoja wa nchi Zinazozalisha Madini ya Almasi Afrika na hivyo kuongeza idadi ya lugha zilizokuwa zikitumika awali katika umoja huo za Kiingereza, Kireno na Kifaransa.
Hayo yamesemwa Aprili 8, na Waziri wa Madini Doto Biteko wakati akifunga Mkutano wa 7 wa Mawaziri wa nchi zinazozalisha Madini ya Almasi Afrika ( African Diamond Producers Association- ADPA) uliofanyika kwa njia ya Video Conference na kutanguliwa na Mkutano wa Wataalam wa jumuiya hiyo ambapo Tanzania ilikuwa mwenyeji wa mkutano huo.
Aidha, Tanzania imekabidhiwa Uenyekiti wa Jumuiya hiyo nafasi ambayo itadumu nayo kwa kipindi cha miaka 2 ikipokea kutoka kwa nchi ya Jamhuri ya Namibia ambayo ilikuwa Mwenyekiti kwa muda wa mwaka mmoja. Pia, nchi ya Zimbabwe imekubalika kuwa Makamu Mwenyekiti na inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano wa 8.
Akieleza kuhusu yaliyojadiliwa na kukubaliwa katika mkutano huo, Waziri Biteko amesema kuwa mkutano huo umekubaliana kuwa Kamati Tendaji ya umoja huo kupitia upya mifumo ya kiutendaji ya umoja huo ndani ya kipindi cha miezi sita na kutoa mrejesho.
Aidha, Waziri Biteko ametumia fursa ya Uenyekiti wa jumuiya hiyo kuzisisitiza nchi wanachama kutumia masoko ya madini yaliyoanzishwa maeneo mbalimbali nchini, akilenga kuzifanya nchi wanachama kuyatumia masoko hayo kufanya biashara ya madini ili manufaa ya madini hayo yaendelee kubaki Afrika na kwa wanachi wenyewe.
Awali, Waziri Biteko amewaeleza mawaziri walioshiriki mkutano huo kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Madini kufuatia Marekebisho yaliyofanywa kwenye Sheria ya Madini ambayo pamoja na mambo mengine, yalipelekea kuanzishwa kwa masoko ya madini katika mikoa mbalimbali nchini ambapo hadi sasa, Tanzania ina jumla ya Masoko ya Madini 39 na Vituo vya Ununuzi wa Madini 41.
Naye, Waziri wa Madini na Nishati wa Jamhuri ya Namibia, Tom Alweendo wa nchi ambayo imemaliza uenyekiti wake, ameutaka umoja huo kupata viongozi shupavu wa kamati tendaji watakaosaidia kuweka msukumo katika utekelezaji wa malengo ya jumuiya hiyo.
Ameongeza kuwa, kama wanachama ni lazima wachochee na kuweka mikakati ya kupigania maslahi ya Afrika kwa madini ya Almasi ikiwemo kuzitaka nchi hizo kuhakikisha zinalipa michango yao kwa mujibu wa sheria.
Pia, Ametumia fursa hiyo kuelezea yale ambayo yalifanywa na nchi hiyo wakati ikishikilia kiti cha Uenyekiti na kueleza kuwa, pamoja na kipindi chake kukabiliwa na changamoto za janga la ugonjwa wa Corona, ilifanikiwa kuunda kamati ya uendeshaji ya jumuiya hiyo.
Mkutano wa 7 wa Mawaziri wa Nchi zinazozalisha madini ya Almasi Afrika, umehudhuriwa na nchi zote 19 wanachama wa umoja huo zikiwemo Nchi za Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Afrika Kusini, Namibia, Tanzania, Zimbabwe, Cameroon, Afrika ya Kati, Ghana, Togo, Guinea na Sierra Leone. Nchi waangalizi zilizoshiriki ni Algeria, Jamhuri ya Congo, Cote Divore, Gabon, Liberia, Mali na Mauritania pia zimeshiriki.
Waziri wa Madini Doto Biteko akizungumza na Waandishi wa habari wakati akifunga Mkutano wa Saba wa Mawaziri wa Nchi za Afrika Zinazozalisha Madini ya Almasi (ADPA) uliofanyika kwa Njia ya Video tarehe 8 Aprili, 2021 Jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇