Na Bashir Nkoromo na Vyanzo vya Habari
Kila April 12 ya kila mwaka Tanzania imekuwa ikifanya kumbukizi ya kifo cha aliyekuwa Waziri wake Mkuu Edward Moringe Sokoine aliyefariki Dunia kwa ajali ya gari, na katika wiki hii, Jumatatu, Aprili 12, 2021, ndiyo ilikuwa siku ambayo miaka 37 ya kumbukizi hiyo ilijiri tangu utokee msiba huo mkubwa wa Kitaifa.
Tarehe hiyo kama ya juzi (Aprili 12) mwaka1984, ndiyo siku ambayo Edward Moringe Sokoine anayeelezewa kuwa mmoja wa viongozi bora sana kuwahi kutokea nchini, alifariki dunia katika ajali ya gari iliyomkumba katika eneo la Dakawa, ndani ya Wilaya ya Mvomero, mkoani Morogoro.
Kama ilivyo ukweli kwamba binadamu wanayo hulka ya kusahau waliotangulia mbele ya haki hata kama walikuwa watu muhimu kwa jamii kiasi gani, ndiyo sababu ikaja hekima kwamba uwepo utaratibu au tabia mahsusi ya kuifanya tarehe aliyoiaga dunia mhusika kuwa siku ya kumbukizi yake ingawa inafaa kumkubuka siku zote kila aliyetangulia mbele za haki.
Pamoja na kwamba kila binadamu anastahili kufanyiwa kumbukizi, lakini ukweli ni kwamba kumbukizi hizi zinafanywa kwa namna na hadhi tofauti tofauti kutegemeana na hazina ya matendo na nafasi aliyokuwa nayo mtu kati yake na ndugu, jamaa hadi Taifa na Kimataifa.
Toauti ya kumbukizi hizi ni kwamba kuna ambao kufanywa kwa ajili ya kumrehemu tu aliyetangulia mbele ya haki lakini wapo ambao kumbukizi zao hufanywa siyo kwa ajili ya kuwarehemu tu, bali hufanyiwa pia kwa ajili ya kukumbuka matendo na mambo yenye tija waliyoacha wamefanya kwa ndugu, jamaa, marafiki na kwa taifa lao kabla ya kufikwa na umauti.
Mbali na kumrehemu, hili la kuacha mambo yenye tija, ndilo linalosababisha Hayati Moringe Sokoine kufanyiwa kumbukizi hadi kitaifa kwa namna mbalimbali, lengo zaidi likiwa ni kuwezesha vizazi na vizazi kuyajua kwa lengo la kuyaiga au kuyaenzi matendo bora yenye tija aliyoacha ameyatenda kabla ya umauti kumchukua.
Hivyo, kwa kuwa ni muhimu vizazi na vizazi kuyajua ili kuyaiga na kuyaenzi yale yenye tija ambayo Hayati Sokoine alilifanyia Taifa, inabidi kutumia namna mbalimbali kuviwezesha vizazi hasa vipya kuyajua mambo hayo na pia kumjua Sokine mwenyewe kupitia maandiko ya kwenye vitabu au makala kama hii.
Hili la kuandika kwenye vitabu na kwenye mitandao kama hivi, ni njia ambayo inawezesha zaidi vizazi vipya kupata fursa ya uhakika kumjua Sokoine, na kwa sasa ni muhimu zaidi kwa kuwa kizazi kipya kilichopo wengi waliofikia umri wa miaka 37 mwaka huu, ambao ni vijana wanaotarajiwa kuwa wazalendo kwa nchi yao hawamfahamu wala kujua vilivyo sifa za Hayati Sokoine na kama wapo ni wachache sana ambao wamebahatika kusimuliwa au kujisomea vitabuni.
Ni kutokana na muktadha huo tumeona ni vema kuitumia kumbukizi hii, kukumbusha kupitia njia hii ya kuandika makala, japo kwa ufupi historia ya Mzalendo huyu Edward Sokoine.
KUZALIWA
Siku ya Jumatatu ya Agosti 1, 1938, katika Kitongoji cha Kilasho kilichopo Jijiji cha Emairete, Monduli Juu mkoani Arusha, Sokoine Ole Severe na Mkewe Napelel Sinyai Noomayaki walipata mtoto wa Kiume ambaye ndiye Edward Moringe Sokoine.
ELIMU/SIASA
Kati ya mwa 1949 na 1953 Edward Moringe Sokoine
alisoma Shule ya Msingi Monduli na kisha akajiunga na Monduli Middle School kunzia mwaka 1953 hadi 1956.
Mwaka 1956 alijiunga na shule ya Sekondari ya Umbwe baada ya kufaulu vema mtihani wa kuhitimu 'midle school'.
Mnamo Januari 1,1961, Edward Moringe Sokoine alijiunga na chama cha Tanganyika African National Union (TANU), ikiwa ni miezi michache kabla Tanganyika haijapata Uhuru.
Akiwa tayari ni mwanachama wa TANU, Mwaka 1962, alienda Ujerumani Magharibi kusomea mambo ya Utawala na kurejea mwaka 1963 na baada ya kurejea toka huko alipangiwa kazi kama District Executive Officer (DEO) wa Masai.
Septemba 30, 1965, akiwa kijana mdogo tu wa miaka 27 lakini mwenye akili na ubunifu mkubwa, aligombea Ubunge jimbo la Masai na kumshinda Mpinzani wake Edwarf Carli Boniface Ole Mbarnote aliyekuwa Chifu wa Wamasai. Sokoine alijizolea kura 6,977, Chifu Mbarnote akiambulia kura 871.
Akiwa Bungeni baada tu ya kuapishwa Bungeni, Edward Moringe Sokoine aliweza kuonyesha uzalendo wake na jinsi alivyo na hekima na utayari wa kutetea wasioweza kujitete wenyewe, kwa mfano katika maswali yake ya kwanza kabisa bungeni aliuza: 1."Kwanini Wamasai wa Ngorongoro wanazuiwa kulima, wakati hawana mifugo ya kuwapatia chakula?" .2 "Kwakuwa tangu kuanza kwa Taifa hili, kuna makabila yamepata maendeleo sana na mengine yapo nyuma sana, je serikali ina mpango gani wa kuwaelimisha walioko nyuma kimaendeleo ili wawe sawa na wenzao?"
Katika hali iliyoonyesha kuaminika mwaka 1967, Mwalimu Nyerere alimteua kuwa Naibu Waziri, Wizara ya Mawasiliano, Usafirishaji na Kazi n Mwaka 1970, akamteua kuwa Waziri wa Nchi, na Mwaka 1972, Mwalimu Nyerere akamteua kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa.
Baada ya vyama vya TANU na Afro Shiraz Party (ASP) kuungana na kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Februari 5, 1977, Sokoine akawa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Februari 13, 1977 Mwalimu Nyerere alimteua kuwa Waziri Mkuu, cheo alichodumu nacho hadi anafariki dunia.
Katika vita vya Kagera mwaka 1979, akiwa Waziri Mkuu, Sokoine alikuwa kiungo muhimu, Mwanzoni mwa vita hivyo aliwaagiza Wakuu wa mikoa wote wakusanye nyenzo zote tayari kwa vita ya kupambana na Nduli Idi Amin Dada wa Uganda.
Januari 23, 1979, alitembelea Mtukura jukagua hali ya usalama wakati sa vita hivyo na inaelezwa kwamba wakati wote wa vita Sokoine alikuwa ni nadra kulala usingizi hali inayoekezwa kwamba ilisababisha hadi hali ya afya yake kutetereka.
Novemba 1980, Sokoine aliomba na kukubaliwa kujiuzulu Uwaziri Mkuu, baada ya kujiuzuku alienda Yugoslavia kwenye matibabu na nafasi yake ikashikwa na Cleopa David Msuya na baada ya kurejea, Mwalimu Nyerere alimteua tena kuwa Waziri Mkuu Februari 24, 1983 na mwaka huo huo wa 1983, Sokoine akaanza kusomea shahada ya "Political Science".
JINA LA DALADALA
Katika miaka ya 1980, sh. 500 ilikuwa imepachikwa jina la Dala, na wakati huo usafiri wa jijini Dar es Salaam ulikuwa ni wa mabasi ya Shirika la Umma la Usafiri Dar es Salaam ambalo kwa kifupi liliitwa UDA, wakati huo hakuna magari ya binafsi yaliyokuwa yakiruhusiwa kusafirisha abiria katika jiji hilo. Ikafika wakati UDA imehemewa katika utoaji huduma, Sokoine akiwa ndiye Waziri Mkuu akaamuru magari binafsi yaanze kuisaidia UDA kubeba abiri kwa nauli ya sh. 500.
Naam, kwa kuwa sh. 500 iliitwa Dala, wapigadebe wa hayo mabasi madogo ya binasi wakawa wanaita abiria kwa kusema " haya twende, Kariakoo (na kwingine) Dala dala", ikaendelea hivyo hadi mabasi hayo nayo nayo yakaitwa Daladala, kwa hiyo kwa namna nyingine mabasi ya daladala yaliyopo hadi leo hadi nje ya Dar es Salaam yaliasisiwa na Sokoine.
VITA VYA UHUJUMU UCHUMI
Aprili 5, 1983, Mwalimu Nyerere alizindua kampeni ya kupambana na wahujumu uchumi baada ya kupitishwa kwa Sheria ya "The Economic Sabotage Act No. 9 of 1983" na kampeni hiyo ambayo ilikuwa ya kufa na kupona akamkabidhi Waziri Mkuu Sokoine kuiendesha na kuisimamia.
Sheria hii ilimtaka mtu aeleze mali aliyokutwa nayo aliipata wapi. Zilianzishwa Mahakama Maalum na Mawakili hawakuruhusiwa kuingia, watu walitakiwa wajitetee wenyewe bila shaka Mwalimu Nyerere aliona kuwa wahalifu wangeweza kutumia ujuzi wa mawakili na kuachiwa.
Katika kutekeleza kamoeni hii watu walimuogopa sana Sokoine kiasi kwamba baadhi ya watu katika sehemu nyingi nchini hasa Dar es Salaam, walitupa barabarani na mitaroni vitu vya thamani vilivyokuwa vimeingizwa nchini kinyemela kama Tv na hata Mahindi, maharage na bidhaa nyingine.
Mbali ya bidhaa, wengine walitupa hadi mabunda ya fedha na wapita njia waliogopa kuokota vitu na fedha hizo kwa kumuogopa Sokoine, hivyo Polisi walikuwa wakiziokota fedha hizo na kuzipeleka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na bidhaa kupelekwa kwenye maghala ya Serikali.
Ikumbukwe wakati huo, sheria za nchi zilikuwa haziruhusu mtu binafsi kuwa na duka ka bidhaa yoyote hata vyakula, maduka ya vyakula na bidhaa nyingine yalimilikiwa na Serikali, na yalikuwepo maduka ya Shirika la Biashara la mkoa yaliyoitwa Regional Trading Company (RTC) na hata kwenye usafiri lilikuwepo Kampuni ya Usafiri Tanzania (KAMATA).
Wakati huo ilikuwa ni kosa la kisheria mtu kukutwa na bidhaa kama nguo, sabuni, dawa za kupigia mswaki, mswaki wenyewe na vitu vingine kama hivyo.
Mshike mshike aliofanya Sokoine katika mpambano huu dhidi ya wahujumu uchumi ulimjenga sana kisiasa na kumfanya Sokoine kipendwa nchini kote.
Hata hivyo, kulikuwa na malalamiko kutokana na jinsi oparesheni lilivyoendeshwa ambayo yalipelekea Salmin Amour ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani aombe radhi kwa niaba ya Serikali.
Baada ya kifo cha Sokoine, Sheria hii ilifutwa na ikatungwa "The Economic & Organized Crimes Control Act, 1984" ambapo mambo mbalimbali kama uwepo wa mawakili kwenye kesi yalirekebishwa.
KIFO
Mnami Aprili 1984 Sokoine alihudhuria Kikao cha Bunge mkoani Dodoma.
Jumatatu ya April 9, 1984, Sokoine alikwenda kusali katika Kanisa la Mtakatifu Paul Dofoma. Usiku wa Jumanne, April 10, 1984, aliandaa karamu ya chakula cha jioni kwa Mawaziri na Wakuu wa Mikoa ambapo inaelezwa alionekana kuongea na kila Waziri na kila Mkuu wa Mkoa.
Jumatano, April 11, 1984, aliandaa chakula cha jioni kwa Wabunge wote wa mkoani kwake Arusha ambapo aliwasihi wafanye jitihada kuwaondoa wananchi wao kwenye lindi kubwa la ufukara.
Siku ya Jumatano April 11, 1984, akilivunja Bunge, aliasa kwa uchungu akisema "Ndugu Spika, ningependa kumalizia kwa kukubaliana na Wabunge wote waliosema na ambao hawakusema lakini wana mawazo haya kwamba jambo hili la kutumia fedha bila idhini ya Bunge lazima tutafute kila njia ya kulikomesha".
Baada ya kulivunja Bunge, katika hali ya kiimani inayoonyesha kuwa Mungu alikuwa ameshapanga jambi lake, Sokoine alipangiwa kusafiri kwa ndege kurudi Dar es Salaam, lakini akakataa, akaamua kusafiri kwa njia ya barabara na sababu ya kufanya hivyo aliiainisha bungeni.
"..Mungu akipenda tutakutana tena kwenye kikao kijacho cha bunge. Mimi nasafiri kwa njia ya barabara ili nijionee hali ya mazao ya wakulima...", Sokoine akaliambia Bunge.
Alhamisi ya April 12, 1984, saa 4:30 asubuhi Sokoine aliondoka na msafara wake kutoka Dodoma, akiwa ndani ya Mercedes Benz ambapo msafara huo ukiongozwa na msafara wa Polisi ambao walikuwa wakihakikisha magari yote yaliyokuwa yakikutana na msafara huo yanaki pembeni kuupisha msafara.
Msafara wa Sokoine ulikuwa na mwendo wa kasi; kama "Minutes" za CC ya CCM ya April 17, 1984 zinavyoeleza na kwa kweli ni jambo la kawaida jwa misafara ya viongozi kwenda mwendo wa kasi kwa sababu za kiusalama na pia huwa kuna uhakika kwamba hakuna kikwazo njiani kwa kuwa Polisi hutangulia 'kusafisha' njia.
Msafara wa Sokoine baada ya kuondoka Dodoma inaekezwa kuwa ulikuwa ukienda kwa spidi ya kilomita 154 kwa saa. Msafara ulipofika eneo la Dakawa mkoani Morogoro, ghafla kilisikika kishindo kikubwa.
Kishindo chenyewe, Hamad! Gari la Waziri Mkuu Edward Moringe Sokoine lilikuwa limegongana na gari aina ya Toyota Land Cruiser lililokuwa likiendeshwa na mtu aliyetambuliwa kuwa ni Dumisan Dube, kijana wa umri wa miaka 23, mpigania Uhuru wa Chama cha ANC cha Afrika Kusini, aliyekuwa akiishi Mazimbu, Morogoro.
Ilielezwa kuwa Kijana Dube licha ya kusimamishwa na Polisi, hakusimama kwani nae alikuwa kwenye mwendo wa kasi katika gar lake akuwa na abiria wawili wanaume Boyce Moye na Perce George.
Sokoine ambaye alikuwa ni mtu wa miraba minne, alikuwa amekaa kiti cha nyuma na iliekezwa kuwa hakuwa amefunga mkanda! Masikini, alirushwa toka nyuma hadi akagonga kioo cha mbele na hivyo kusababisha aumie sana na hivyo kufariki dunia kabla ya kufikishwa hospitali ya mkoa wa Morogoro ambako madaktari walithibitisha kifo chake.
Kwa mujibu wa 'Postmortem Report' iliyowasilishwa mbele ya Kamati Kuu ya CCM, mbavu na mifupa ya mikononi na miguuni vilivunjika. Mbavu zilizovunjika zilisababisha kuchoma mapafu!
Naam, ajali hiyo ilichukua maisha ya Sokoine tu kwani wengine wote walisalimika na kupata majeraha ya wastani, na ilielezwa kuwa Yusto Chuma, aliyekuwa mlinzi wake ambaye alikaa kiti cha mbele kulia, na Ally Abdalka aliyekuwa dereva wake, walijeruhiwa kiasi.
Alasiri ya siku hiyo, Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD) ghafla ilisitisha matangazo yake na ukapigwa wimbo wa Taifa, Mwalimu Nyerere baada tu ya wimbo huo, kwa uchungu mkubwa, akalitangazia Taifa msiba huo wa kihistoria akasema;
"Ndugu wananchi, leo hii ndugu yetu, kijana wetu, Edward Moringe Sokoine, Waziri Mkuu wa Tanzania, alipokuwa akirejea Dar es Salaam toka Dodoma, gari lake lilipata ajali na amefariki. Ndugu Watanzania naomba muamini Edward amefariki kwa ajali na si kitu kingine", na baada tu kutoa taarifa hiyo alibubujikwa na machozi kutokana na uchungu.
Baada ya taarifa hiyo jutolewa na Mwalimu Nyerere vilio na simanzi kubwa vilitamalaki nchi nzima. Kwenye maofisi, vyuoni, mashuleni, kwenye mabaa, mabarabarani, kote huko wananchi walionekana dhahiri wamevurugwa!.
Kikao cha UWT kilichokuwa kikifanyika Ofisi Ndogo ya Nakao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Sakaam, kilisambaratika ghafla bila hata Mwenyekiti wake, Mama Soohia Jawass, kukiahirisha kwani mara tu baada ya taarifa hiyo iliyoleta huzuni, kinamama waliokuwa kwenye kikao hicho waliangua vilio visivyomithilika.
Serikali ilitangaza wiki mbili za maombolezo na kuamuru bendera nchi nzima kupeperushwa nusu mlingoti.
Mwili wa Sokoine uliwasili Ikulu, Dar es Sakaam ku toka Morogoro saa 11 jioni siku hiyohiyo ukiwa umefunikwa kwa bendera ya Taifa.
Mwalimu Nyerere akiongozana na mkewe Mama Maria waliusogelea mwili huo kisha akaufunua bendera na kuweka mikono yake kwenye paji la uso wa Sokoine. Mwalimu Nyerere na Mama Maria, aliyekuwa na kitambaa cheupe, walilia kwa uchungu sana hadi kuondolewa na walinzi wao.
Mwili wa marehemu Sokoine ukapelekwa kuhifadhiwa Hospital ya Lugalo, shughuli ya kutengeneza jeneza la akapewa Gdorge Christos aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari Tanzania chotara ambaye baba yake alikuwa ni Mgiriki na mama yake Msukuma akiitwa Maria, aliyekuwa mmoja wa mabinti wa Chifu Kidaha.
Saa 12 jioni ya siku hiyo, Christos na mkewe, Elizabeth Walker naPsul Mkanga aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, walienda hospitali kuchukua vipimo vya mwili wa Sokoine. Kisha wakaenda Chang'ombe kilipo Kiwanda cha HEM-SINGH ambako bahati nzuri mwenye kiwanda alikuwa hajafunga.
Kazi ya kutengeneza Jeneza ikaanza mara moja na kumalizika usiku wa manane. Kisha, Walker akalipamba jeneza hilo na likapelekwa hospitalini. Siku ya Ijumaa, Aprili 13, 1984, maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam na mikoa ya jirani walifurika "Karimjee Hall" kumuaga mpendwa wao, marehemu Sokoine. Kwa hakika, umati uliokuwepo uliweka rekodi iliyokuja kuvunjwa na umati uliojitokeza Octoba 21,1999 kufuatia kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa wakati huo.
Jumamosi ya Aprili 14, 1984, mwili wa marehemu Sokoine ulipelekwa Uwanja wa Ndege kwa ajili ya kusafirishwa kwenda Arusha kwenye mazishi na inaekezwa kuwa katika hali isiyokuwa ya kawaida, Daladala zote jijini zilipeleka abiria bure uwanja wa ndege kumuaga mpendwa wao. Kaburi la aina yake lilijengwa huko Monduli na Meja John Warden 'Black mamba', Mtanzania chotara, na aliifanya kazi hiyo kwa kushirikiana na askari wa Jeshi ka Ulinzi ka Wananchi ws Tanzani (JWTZ).
Mazishi ya marehemu Sokoine yalipewa heshima zote na yaliyohudhuriwa na umati wa watu wakiongozwa na Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, baadhi ya waliohudhuria ni pamoja na Oliva Tambo aliyekuwa Rais wa ANC na Alfref Nzo aliyekuwa Katibu Mkuu wa ANC ambao inaelezwa kuwa walie lezea kusikitishwa sana na kifo hicho kilichosababishwa na raia mwenzao wa Afrika Kusini. Kufuatia kifo hicho Sokoine aliacha wajane wawili Naponi na Nakiteto na watoto 11.
Mei 17, 1984, Dube alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Morogoro ambako kesi yake iliahirishwa. Juni 12, 1984, upande wa mashaka ukiongozwa na Johnson Mwanyika (SSA) ulifika mahakamani na mashahidi 21. Hata hivyo, Dube aliposomewa mashtaka 7 alikiri yote, Hakim Simon Kaji (PRM) akampa kifungo cha miaka mitatu.
Kwa jumla ni kwamba kifo cha Sokoine kiliacha kishindo kikubwa sana, sababu yake kubwa ikiwa ni kwamba ni kiongozi ambaye alikuwa amejipambanua katika kujitoa kulitumia taifa la Tanzania kwa uzalendo wa hali ya juu.
Kulingana na wanaomwelezea Sokoine ni kwamba alikuwa mchspakazi, mkweli na muwazi asiyependa uzembe tena mzalendo kwa nchi nchi yake, na uhalisia wake ulijitanabahisha kwa kauli zake mbalimbali anapozungumza na wananchi au viongozi katika matukio mbalimbali kama haya aliyowahi kunukuliwa akisema.
1. "Ole wake kiongozi asiye na nidhamu na mzembe ntakaemkuta. Viongozi wazembe na wabadhilifu wahesabu siku zao".
2. "Vijana wengi siku hizi wana mali kuliko wazazi wao waliofanya kazi kwa miaka zaidi ya 40 lakini wazee hao wanataka Serikali ndio iwaulize watoto hao wamepata wapi mali hizo. Mzazi unashindwa nini kumuuliza mwanao?".
3."Katika nchi inayojali haki na usawa, majeshi hayana budi kuwa chombo cha kulinda haki na maslahi ya wengi. Kamwe hayaruhusiwi kuwa chombo cha wachache wenye kujali nafsi zao".
4."Viongozi wanaoteuliwa lazma wawe wazalendo wa hali ya juu. Naskia huko mikoani kuna viongozi wanagombania magari na nyumba. Mambo hayo si muhimu. Viongozi wanatakiwa kugombania juu ya Maendeleo ya wanavijiji. Huu ni ugomvi mtakatifu".
"Mimi nilikuwa Kamishina wa Planning. Nilikuwa nafanya kazi na makamisha wengine na Sokoine mara nyingine hadi usiku wa manani kisha anatusindikiza ye anarudi kuendelea na kazi. Asubuhi tunakuta ameishatoa mafaili. Marehemu Sokoine alikuwa Mfanyakazi hodari, Mwaminifu na Muungwana sana". alisema mtu mmoja wa akaribu yake na kunukuliwa katika gazeti moja la Kiingereza la hapa nchini wakati huo.
Hayati Sokoine, japokuwa alipenda maisha bora, lakini hakupenda tajiri,
"Edward hakuwa na mali yoyote ukiachilia ng'ombe wa urithi. Alikuwa na suti tatu na viatu pea mbili tu", alinukuliwa Baba wa Taifa akisema kwenye Msiba wa Sokoine ambao aliongoza wakati huo
Pia Sokoine alikuwa mbunifu wa mambo mbalimbali yenye tija, kwa mfano alianzisha kitu alichokiita Presidential Trust Fund, Ikulu ambapo alikuwa akiweka sehemu ya mshahara wake ili kuwasaidia kina mama kuweza kukopa. Mshahara wa Waziri Mkuu wakati huo inaelezwa kuwa ulikuwa ni Sh. 3, 000 (Elfu tatu tu),
"Kwenye sherehe ya siku yangu ya kutimiza miaka 80 niliwaambia marafiki zangu kuwa nilipokuwa Waziri Mkuu nilikuwa napokea mshahara wa Sh. 3,000 tu, hawakuamini." amekaririwa Waziri Mkuu Mstaafu Cleopa David Msuya akizungumza wakati wa Berthday yake. Msuya maarufu kama CD Msuya alikuwa Waziri Mkuu kuanzia 1980 hadi1983.
Halikadhalika, inaelezwa kwamba Sokoine alikuwa mchamungu sana, alikuwa Mkristo Mkatoliki na inasemwa kwamba aliipenda sana dini yake na alikuwa mwanachama wa utawa wa tatu wa Mt. Fransisca na alipendelea zaidi kusali Kanisa la Mt. Joseph, Oysterbay Dar es Salaam.
Pamoja na upendo kwa watu wengine na kuwa mchamungu, lakini Sokoine alikuwa 'mhogo mchungu' dhidi ya mafisadi na wahujumu uchumi, mfano ni kama vile wakati akiwa Waziri Mkuu aliamuru aliyekuwa Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Edward Barongo kuwekwa kizuizini kwa miezi minne hadi alipoachiliwa na Mwalimu Nyerere. Hata hivyo hatukuweza kupata kisa kamili cha tukio hilo, lakini inaelezwa akwamba Mkuu huyo wa mkoa alikuwa amejihusisha na ubadhirifu wa fedha za umma.
Aliyekuwa Rais wa Tanzania hayati Dk. John Magufuli alikuwa miongoni mwa viongozi walimkubali sana Sokoine. "Aprili 12, 1984 Sokoine alipofariki ilikuwa ni huzuni kubwa sana. Mimi nilikuwa kwenye mafunzo ya lazima JKT Mpwapwa 'Operesheni Nguvukazi'. Sokoine Kamwe hatasahaulika kwani alipiga vita rushwa, wizi na unyonyaji. Alikuwa Mzalendo wa kweli hivyo ni mwito wangu kwa Watanzania tumuige na tumuishi." aliwahi kusema Dk. Magufuli wakati akizungumza Aprili 12, 2018.
Huyo ndiye Hayati Edward Moringe Sokoine, mmoja wa viongozi bora kabisa kuwahi kutokea nchini, hivyo nilivyotangulia kueleza hapo awali kwamba pamoja na kurehemu, lengo lingine la kumbukizi ni kuwezesha waliobaki kuiga mema yaliyofanywa na marehem wakati wa uhai wake, bila shaka kila Mtanzania hasa vijana, wenye dhamira ya ukweli ya kuijenga Tanzania bora hawana budi kujitahidi kumuishi hayati Sokoine ili kuwa wazalendo wa ukweli.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇