LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Apr 8, 2021

GUTERRES ATAKA DUNIA IPATE FUNZO KUTOKANA NA MAUAJI YA KIMBARI YA RWANDA

 

  • Guterres  ataka dunia ipate funzo kutokana na mauaji ya kimbari ya RwandaKatibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema wakati huu dunia inapojiunga katika mshikamano na watu wa Rwanda katika kumbukumbu ya mauaji ya kimbari, kuna ulazima wa kuhakikisha kwamba tunazingatia masomo ambayo wanadamu waliyapata kutokana na tukio hilo la miaka 27 iliyopita ambapo zaidi ya watu milioni moja waliuawa.

Guterres ameyasema hayo Jumatano kupitia ujumbe kwa njia ya video kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Tafakari kuhusu Mauaji ya Kimbari ya mwaka 1994 Dhidi ya Watutsi nchini Rwanda.

“Leo, kote ulimwenguni, watu wanatishwa na vikundi vyenye msimamo mkali vilivyoazimia kujiimarisha kupitia mgawanyiko wa kijamii na ulaghai wa kisiasa na kiutamaduni. Harakati hizi zenye msimamo mkali zinawakilisha tishio kuu la usalama katika nchi nyingi. Wakati teknolojia na mbinu wanazotumia wenye itikadi kali zinabadilika, ujumbe mbaya na chuki vinabaki vile vile. Kuziondolea utu jamii, habari potofu na matamshi ya chuki yanachochea moto wa vurugu.” 

Bwana Guterres akiendelea kusisitiza umuhimu wa ulimwengu wa leo kujifunza kutokana na historia, amesema, “tuliona kile kilichotokea Rwanda mwaka 1994, na tunajua matokeo mabaya wakati chuki inaporuhusiwa kutamalaki.” 

Guterres akieleza namna Rwanda ilivyoweza kupona na kuibuka tena kutoka katika maumivu na madhara ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, amesema, “baada ya kukumbwa na unyanyasaji na ubaguzi wa kijinsia ambao hausemeheki, wanawake wa Rwanda sasa wanashikilia zaidi ya asilimia 60 ya viti vya bunge na kuifanya Rwanda kuwa kiongozi wa ulimwengu. Watu wa Rwanda wametuonesha nguvu ya haki na upatanisho, na uwezekano wa maendeleo. Katika Siku hii adhimu, sote tujitolee kujenga ulimwengu unaoongozwa na haki za binadamu na hadhi kwa wote.” 

Mwaka huu ni miaka 27 imepita tangu zaidi ya watu milioni moja wauawe kwa utaratibu maalumu chini ya miezi mitatu nchini Rwanda. Kwa kiasi kikubwa waliouawa walikuwa Watutsi, lakini pia Wahutu wenye misimamo ya wastani waliuawa pamoja na wengine ambao walipinga mauaji ya kimbari. 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages