***********************************
Na. Paschal Dotto- Maelezo
Kwa Mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 18, kila mwananchi ana haki ya kupata habari na kuwa na uhuru wa kutoa maoni, lakini pia Mkataba wa kimataifa wa haki za Kisiasa na Kiraia wa mwaka 1966, Ibara ya 19 pia unaeleza haki ya mwananchi kupata habari.
Katika zaira yake ya Februari 25, 2021 Jijini Dar es Salaam, wakati wa kuzindua ofisi za kituo cha televisheni cha “Channel Ten” zilizopo katika jengo la “Jitegemee” na kuweka jiwe la msingi katika soko la Kisutu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alieleza umuhimu wa wananchi kupata habari kutokana na kile Serikali yao inachokifanya kwenye taasisi, Mamlaka na Wizara mbalimbali na kuwasisitiza watendaji kulingana na nafasi zao kutoa habari za utekelezaji wa shughuli za Serikali kwa wanahabari ili wananchi waweze kupata haki yao ya msingi ya kikatiba.
“Watendaji wa Serikali wawe wepesi kutoa taarifa sahihi kwa waandishi wa habari, utakuta yamefanyika mambo mazuri lakini hayatolewi na wananchi hawayafahamu, tusiogope kukosolewa, lakini vyombo vya habari toeni taarifa za ukweli bila kuweka chumvi, zingatieni ukweli,” alisema Rais Magufuli.
Katika Hotuba yake, Rais Magufuli alisisitiza kwa Watendaji wa Serikali kutoa taarifa za utendaji wa Serikali katika maeneo yao, sambamba na vyombo vya habari kutoandika habari zisizo za ukweli, hivyo jambo hilo likitekelezwa na taasisi, Mamlaka na Wizara kupitia vitengo vya Habari litaleta Muunganiko mzuri kati ya Serikali na wananchi
Aliongeza kuwa licha ya Wizara na Taasisi za Serikali kuwa na Wasemaji katika ofisi zao bado kumekuwepo na changamoto ya utoaji taarifa kwa waandishi wa habari, na kuwataka Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi kufuatilia suala hilo.
“Wizara ya Habari bahati nzuri Waziri uko hapa na Katibu Mkuu wa Wizara husika kafuatilieni hili, sisi ndani ya Serikali tuwe wepesi kutoa taarifa mapema ambazo zinaleta faida kwa Watanzania” alisema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli alibainisha kuwa Watanzania wanatakiwa kuwa wazalendo licha ya Tanzania kuwa mojawapo wa nchi zenye vyombo vingi vya habari duniani ambapo mwaka 2015 kulikuwa na vituo 106 vya redio vilivyosajiliwa, vituo vya televisheni 25, ambapo Februari 2021, kumekuwepo na vituo vya redio vilivyosajiliwa 195 na vituo vya televisheni 46, redio za mtandaoni 23, televisheni za mtandaoni 440 pamoja na magazeti na majarida 247 vimesajiliwa hadi kufikia Februari 2021.
Aliongeza kuwa, “Vyombo vya habari mnajitahidi kutoa habari, lakini mtangulize sana uzalendo na haki kwa yule anayeandikiwa habari, kumekuwepo na uzushi sana mara fulani kafa ni mambo ya ajabu, lakini pia katika habari ambazo taifa letu linaandikwa vibaya watu wanashabikia, uzalendo umepungua tutangulize uzalendo wa nchi yetu, niwaombe Watanzania wote tutangulize maslahi ya taifa, wajenga nchi ni sisi na wabomoa nchi ni sisi”.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Bashiru Ally, alisisitiza kuwepo kwa usimamizi imara wa sekta ya habari kimawasiliano kwani ndiyo sekta inayounganisha Serikali na Wananchi.
Alieleza jinsi Sekta na Habari kimawasiliano inavyoweza kuunganisha Serikali kupitia utumishi wa umma na kufanya kazi kama timu moja, lakini pia habari zinazotolewa na taasisi, Idara, Wizara na Mamlaka mbalimbali kwenda kwa wananchi ili wajue Serikali inafanya nini katika maeneo yao.
“Mhe, Rais jambo ambalo umekuwa ukilisisitiza tangu uchaguliwe na kuanza ziara ni umuhimu wa mawasiliano ndani ya Serikali na mawasiliano kati ya Umma na Serikali, na hii inakuja baada ya Idara, Taasisi, Mamlaka na Wizara mbalimbali kutoa taarifa zilizo sahihi kwa wananchi kupitia vyombo vya habari ili wananchi wajue Serikali yao inafanya nini katika maeneo mbalimbali nchini”, alisema Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Bashiru.
Katika Kikao cha Wahariri Waandamizi wa vyombo vya Habari kulichoandaliwa na Kuratibiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, alisema kuwa, “Maelekezo ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuhusu utoaji wa habari za Serikali kwa umma yanatekelezwa kwa kasi na ofisi au mtendaji yeyote wa ofisi ya umma atakayekaidi asitafute wa kumlaumu”, Alisema Dkt. Abbasi.
Alibainisha kuwa Wizara ya Habari, kupitia Waziri wa Habari Mhe Innocent Bashungwa, imeshasaini barua yenye maelekezo ya kuzijulisha taasisi zote za umma nchini kuhusu tathmini itakayofanyika.
Shirika la TANESCO limeanza utekelezaji wa agizo la Mhe Rais Magufuli ambapo liliandaa semina mkoani Morogoro ya Wahariri Waandamizi kuhusu Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere Hydroelectric Power Project (JNHPP).
Dkt. Abbasi, “alisema utoaji wa habari kwa umma ni jambo la kisheria na kikatiba hivyo hata maelekezo ya Rais yako sahihi na atakayekaidi amekaidi mamlaka, amekaidi sheria na amekaidi katiba, ndiyo maana TANESCO imeanza na kasi hii”
Aliwataka Wahariri na Waandishi nchini kuenzi misingi ya weledi na uzalendo katika kazi zao ikiwemo kufanya utafiti kwanza kuliko “kufakamia” mawazo na maoni ya watu wasioitakia nchi mema.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇