Na Richard Mwaikenda, Dodoma
WAKAGUZI wa Mazingira wametakiwa kuzingatia taratibu na miiko ya utumishi wa umma wanapotekeleza majukumu yao.
Hayo yamezungumzwa na Meneja wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kati,Dk. Frankline Rwezimula wakati wa hafla ya kuwakabidhi vitambulisho maalumu kwa Wakaguzi wa Mazingira 34, jijini Dodoma leo.
"Wakaguzi ni sawa na watumishi wengine wa umma. Hawako juu ya sheria. Hivyo, wakaguzi wanapaswa kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa mujiu wa taratibu za serikali,"amesisitiza Dk. Rwezihula.
Aidha, Dk. Rwezihula amesema kuwa wakati wa kutimiza wajibu wao ni vyema wawe na vitambulisho vyao ili kuepusha kudhaniwa kuwa ni wakaguzi feki.
Amewataka wakaguzi hao kuhakikisha wanafanya kazi kwa uwazi na siyo kwa kificho na wakati wa ukaguzi wawe wanashirikisha wadau wakiwemo viongozi wa serikali za mitaa, wananchi walengwa hasa wakati wa kuchukua sampuli.
"Faini itozwe kwenye kosa kubwa na liwe linalipika kulingana na uwezo wa kiuchumi wa mtenda kosa.Mlengwa anayetozwa faini lazima akubali ndiyo mwandikishiane anatakiwa kusaini lakini faini iwe inalipika. epuka kutumia vitisho na ubavu," amesema Rwezihula.
Naye, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara ya Maji, Ndugu Barnabas Ndunguru ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga, amesema kuwa baada ya wakaguzi hao kupatiwa vitambulisho watakuwa na nafasi nzuri ya kutekeleza majukumu ya ukaguzi wa mazingira kwa weledi kwa kufuata sheria.
"Nitumie fursa hii kuwakumbusha kuwa wajibu wenu wa msingikama wakaguzi wa mazingira ni kuhakikisha katika taasisi zenu masuala yenu ya mazingira yanasimamiwa na kutekelezwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004," amesema Mhandisi Ndunguru.
Wakaguzi hao waliopatiwa mafunzo ya uweledi kabla ya kukabidhiwa vitambulisho wametoka makao makuu ya wizara, mamlaka za maji, Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini ()Ruwasa, Ofisi za maji za mabonde na Ewura.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇