Katibu wa MAREMA Tawi la Mirerani Rachel Njau akitoa salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Rais wa awamu ya tano hayati John Magufuli.
Katibu wa MAREMA Mkoa wa Manyara Tariq Kibwe akizungumza wakati wa dua na sala ya kumuombea hayati John Magufuli apumzike kwa amani.
………………………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi wetu, Mirerani
Katibu wa chama cha wachimbaji madini Mkoani Manyara (MAREMA) Tawi la Mirerani, Rachel Njau amesema Rais wa awamu ya tano hayati John Magufuli amesababisha mchimbaji mdogo kuonekana na kutambulika tofauti na awali ilikuwa sekta isiyo rasmi.
Njau ameyasema hayo kwenye sala na dua ya kumuombea apumzike kwa amani Rais wa awamu ya tano hayati John Magufuli iliyofanyika kwenye lango la kuingia ndani ya ukuta unaozunguka migodi ya madini ya Tanzanite.
Amesema hivi sasa mchimbaji mdogo wa madini anatambulika na anathaminika tangu hayati Magufuli alipoingia madarakani kupitia Serikali ya awamu ya tano.
“Wachimbaji madini tunathaminika mno ndiyo sababu hayati Rais Magufuli alitenga kila mwaka ikifika Januari 22 alikuwa anakutana na wachimbaji madini na kusikiliza changamoto zao tofauti na awali,” amesema Njau.
Hata hivyo, amesema baada ya wachimbaji kupatiwa elimu ya kulipa kodi, waliondokana na tabia ya kukwepa Kodi ndiyo sababu hivi sasa mapato ya madini yanapanda Serikalini kutokana na kulipa kodi baada ya elimu kutolewa.
Amesema wachimbaji madini wanamwamini na wanamuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha nchi inasonga mbele kupitia sekta ya madini.
“Wanawake tunaweza na wachimbaji madini tuna imani kubwa kwa Rais wetu mama Samia atavaa viatu vya hayati Magufuli na atatufikisha Kaanani kwani yeye ni Joshua aliyenyanyuliwa baada ya Mussa,” amesema Njau.
Katibu wa MAREMA Mkoa wa Manyara, Tariq Kibwe amesema hayati Magufuli alikuwa na mchango mkubwa mno kwa wachimbaji hivyo watamuenzi na kumkumbuka kwa kutekeleza yale yote yanayopaswa kufanyika kwa upande wao.
Amesema hivi sasa sekta ya madini imepiga hatua kubwa na watahakikisha inaendelea kutambulika tofauti na awali wachimbaji walikuwa hawathaminiki.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇