Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari, Alice Wairimu Nderitu, na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Michelle Bachelet, wametahadharisha kuhusu hatari ya ukatili mkubwa unaoendelea kufanywa nchini Myanmar, baada ya siku nyingine ya umwagaji damu ya ukandamizaji unaotekelezwa na jeshi la nchi hiyo lililotwaa madaraka ya nchi kwa nguvu.
Katika taarifa yao ya pamoja, maafisa hao wawili wakuu wa Umoja wa Mataifa wamelaani vikali mashambulio mabaya na yanayozidi kuongezeka yanayotekelezwa na jeshi la Myanmar dhidi ya waandamanaji wanaoandamana kwa amani na pia ukiukaji mwingine mkubwa wa haki za binadamu tangu jeshi hilo lilipochukua madaraka mnamo tarehe Mosi Februari, 2021.
Jumamosi ilikuwa siku ya umwagaji damu mkubwa zaidi nchini Myanmar tangu maandamano dhidi ya mapinduzi yalipoanza ambapo vikosi vya usalama viliua watu wasiopungua 107 wakiwemo watoto 7 kulingana na ripoti kadhaa za kuaminika za vyombo vya habari.
Michelle Bachelet na Alice Wairimu Nderitu wametoa wito kwa wanajeshi kuacha mara moja kuwaua wale ambao wana jukumu la kuwatumikia na kuwalinda.
Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia amelaani vikali mauaji ya raia wakiwemo watoto na vijana wadogo yanayofanywa na wanajeshi na askari wa Myanmar.
Jeshi la Myanmar lilitwaa madaraka ya nchi Februari Mosi ya mwezi uliopita baada ya kumkamata Rais wa nchi hiyo, Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi mkubwa, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo.
Kisingizio cha jeshi cha kufanya mapinduzi hayo ni madai yake ya kutokea wizi na udanganyifu katika zoezi la uchaguzi wa Bunge wa Novemba mwaka jana (2020), ambapo kwa mujibu wa matokeo, chama tawala cha National League for Democracy (NLD) kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kiliibuka na ushindi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇