LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 3, 2021

TCRA TANGAZA NEEMA KWA WATUMIAJI WA HUDUMA ZA MAWASILIANO YA SIMU ZA MIKONONI TANZANIA

Mkurungezi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi James Kilaba.


CCM Blog, Dar es Salaam

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa mwongozo wa kanuni ndogo 12 ambazo zitasaidia kutatua kero za watumiaji wa huduma za mawasiliano ya simu za mkononi hapa nchini.


Akizungumza jijini Dar Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Mhandis James Kilaba amesema hatua hiyo imekuja baada ya TCRA kupokea jumla ya maoni 3,278 ya malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali ikijumuisha watumiaji, watoa huduma, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.


Alisema utekelezaji wa kanuni hizo unatarajia kuanza Aprili 2, mwaka huu na ili kutanzua mambo mbalimbali yanalolalamikiwa na wateja.


Mhandisi Kilaba amesema kwa kuzingatia maoni na ushauri wa wadau TCRA imeweza kuandaa kanuni hizo ambazo zitasaidia kutatua kero.


Amesema, baadhi ya mambo yaliopo katika kanuni hizo ni pamoja na mtoa huduma hatatoa huduma za vifurushi bila kibali cha mamlaka.


Mhandisi Kilaba amesema, mtoa huduma anapaswa kuhakikisha kwamba bei za vifurushi zinazingatia bei husika ya chini na ya juu zilizowekwa na mamlaka, pamoja na kutumia lugha rahisi na vigezo na masharti yaliyo wazi kuhusu vifurushi vinavyotolewa.


Amesema, vifurushi vinavyotolewa kwa mtumiaji havitaondolewa, havitarekebishwa au kubadilishwa ndani ya miezi mitatu baada ya kuidhinishwa, mtoa huduma ataweka utaratibu au mfumo wa kumuwezesha mtumiaji mwingine ndani ya mtandao wake kwa masharti.


"Mtumiaji wa huduma ataweza kuhamisha kifurushi cha MB kwa watumiaji wasiozidi wawili, lakini pia mtumiaji aliyeamishiwa unit za kifurushi hataruhusiwa kumhamishia mtumiaji mwingine uniti hizo au sehemu za uniti hizo," amesema.


Amesema, mtoa huduma hataruhusiwa kupunguza kasi ya data kwenye kifurushi cha mteja ndani ya muda wa kifurushi husika, mtoa huduma hatafanya promosheni zaidi ya tatu au kutoa ofa maalum zaidi ya tatu kwa wakati mmoja kupitia huduma za sauti, sms na data.


Mhandisi Kilaba amesema, kanuni hizo zitakapoanza kutumika zitasaidia kujibu malalamiko mengi ya wateja kwa sasa na kusisistiza watumiaji kuendelea kufuatilia mabadiliko hayo kwa umakini na kwa mtazamo chanya.


"Kupitia kanuni hizi zitaboreeha huduma za vifurushi kutokana na maoni ya wengi kuwa vifurushi vimekuwa vikiwasaidia,"amesema.


Katika hatua nyingine, Mhandisi Kilaba amewataka Watanzania kuendeleza kupambana na masuala ya utapeli mtandaoni na kuwataka kuendelea kusoma mwongozo wa TCRA kwa watumiaji wa huduma na bidhaa za mawasiliano.


"Usikubali kutapeliwa kwa kutekeleza maelekezo yanayohusu mhamala wowote wa kifedha katika simu yako, kwa kupigiwa simu na mtu yeyote anayejifanya mfanyakazi wa kampuni yoyote ya simu au wakala wake," amesema Mhandisi Kilaba.


Pia amesema, ikitokea mtumiaji wa simu amepigiwa simu au kutumiwa ujumbe mfupi wowote wa kitapeli asiutekeleze badala yake autume ujumbe huo kwa namba 15040 na namba iliyoutuma ujumbe hiyo kwa ajili ya kuchukua hatua.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages