LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 7, 2021

SH. MILIONI 400 ZILIVYOJENGA HOSTELI KATIKA SHULE TANO ZA SEKONDARI, SONGEA MKOANI RUVUMA

Na Albano Midelo, Afisa Habari Mkoa wa Ruvuma
Halmashauri ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma imetumia kiasi cha shilingi milioni 400 kujenga hosteli tano katika shule za sekondari ili kuwapunguzia kero wanafunzi wa kike.

Afisa Mipango wa Halimashauri hiyo Athumani Nyange amesema  kila hosteli imegharimu sh. 80 na kwamba fedha zilizotumka kutekeleza mradi huo zimetolewa na serikali kwa ajili ya kujenga hosteli katika shule za sekondari Matimira, Kilagano, Maposeni, Mpitimbi na Mhalule.

Nyange amesema Halmashauri ilipokea fedha hizo Agosti 2020  kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ambapo ujenzi umekamilika kwa asilimia 100 na kwamba hivi sasa kinachosubiriwa ni kuweka vitanda na hosteli kuanza kutumika rasmi.
 
“Kila hosteli  ina uwezo wa kubeba wanafunzi 80,kila hosteli ina vyumba 20, kila chumba kinachukua wanafunzi wanne kwa niaba ya wananchi tunaishukuru sana serikali kwa sababu hosteli hizi ni ukombozi kwa watoto wa kike’, alisema Nyange.

Selestin Mlelwa ni Kaimu Mkuu wa shule ya sekondari  Mhalule  amesema mradi wa hosteli katika shule hiyo umekamilika na kusisitiza kuwa hosteli hiyo itakuwa ukombozi kwa watoto wa kike ambao wamekuwa wanatembea kilometa tisa kila siku kwenda na kurudi shuleni.

Patrick Matembo ni Mkuu wa shule ya sekondari Mpitimbi  anaishukuru serikali kwa kuipatia shule hiyo zaidi ya shilingi milioni 106 kwa  ajili ya kutekeleza miradi mitatu ambayo ni hosteli moja imegharimu sh. milioni 80,darasa moja sh. milioni 20 na ujenzi wa choo matundu sita uliogharimu sh.milioni sita.

Elizabeth Mwakyusa ni mwanafunzi wa kidato cha sita sekondari ya Mpitimbi anatoa shukrani kwa serikali kwa kuwajengea hosteli kitendo ambacho amesema kitawaongezea wanafunzi ari ya kusoma na kuongeza ufaulu sanjari na kupunguza utoro ambao ulikuwa  unachangiwa na kutembea kwa  umbali  mrefu kutoka kwenye makazi yao.

Halmashauri ya wilaya ya songea ina jumla ya shule za sekondari   21 kati ya hizo sekondari 16 zinamilikiwa na serikali na  sekondari tano zinamilikiwa watu  binafsi na Taasisi ya dini.


Mkuu wa shule ya sekondari Mpitimbi Patrick Matembo akiwa akizungumzia mradi wa hosteli ambao umekamilika.

Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Mhalule Selestini Mlelwa akieleza mradi wa hosteli.

Mradi wa hosteli katika shule ya Sekondari Mpitimbi ambao umekamilika kwa gharama ya shilingi milioni 80

No comments:

Post a Comment

ANDIKA MAONI (COMMENTS) HAPO👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages