LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Mar 22, 2021

RAIS SAMIA AWATAKA WATANZANIA WASIWE NA MASHAKA NA UONGOZI WAKE, ASEMA AMEPIKWA VEMA NA DK. MAGUFULI, HAKUNA KITAKACHOHARIBIKA

Na Mwandishi wa CCM Blog, Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewaambia Watanzania viongozi waliobakia wajifunza , wamepikwa na wameiva vizuri kutokana na kufanya kazi chini ya aliyekuwa Rais Hayati Dk.John Magufuli.


Rais Samia ameyasema hayo wakati akitoa hotuba yake katika tukio la kutoa heshima na kuaga mwili wa kipenzi cha Watanzania Dk. John Magufuli lililofanyika Kitaifa katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma, leo. Dk. Magufuli amefarikii Dunia Machi 17 mwaka huu katika Hospitali ya Mzena, Dar es Salaam.


“Tunashukuru tumejifunza mengi, tumepikwa na tumeiva vizuri, wakati tunakwenda kumpumzisha mpendwa wetu kwa wale ambao wana mashaka na mwanamke nataka kumwambia niliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nataka kurudia niliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwenye maumbile ya kike,” amesema Rais Samia.


Amesema kuwa Tanzania tumepoteza kiongozi jasiri, kiongozi mchapakazi, jasiri, mwanamwema wa Afrika, mwanageuzi mahiri na mtetezi wa kweli.”Tumekusanyika hapa kwa umoja wetu na mshikamano wetu.


“Watu wamejaa, nimeshuhudia upendo mkubwa wa Watanzania kuanzia pale Dar na leo hapa Dodoma na najua na huko kwingine nako itakuwa hivyo hivyo.Hali hii ya watu kujitokeza kwa wingi kumuaga  haishangazi maana amegusa maisha ya wengi


“Hili jambo ni  la nadra kwa maisha ya mwanadamu na Mungu alimjalia kuwa na karama kuwa tutamkumbuka.Alisema siku nikifariki mtanikumbuka na kweli leo na milele tutamkumbuka, tunakumbuka sana na vizazi na vizazi vitakukumbuka,”amesisitiza.


Aidha amesema alipata nafasi ya kumjua Dk.Magufuli wakati anahudumu Wizara ya Ofisi Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, nilivutiwa na utendaji wake, alizijua barabara zote za nchi hii kwa majina , urefu na gharama zake.


“Alijua hadi idadi ya samaki walioko kwenye maziwa yetu makuu, daima nitamshukuru kwa imani kubwa kwangu na wanawake watanzania, kupitia yeye(Magufuli)Tanzania ilipata Makamu wa Kwanza wa Rais na sasa ndio Rais wa Tanzania


“Walinipa nafasi ya kuonesha uwezo wangu na wanawake tunaweza, kwa miaka sita nilihudumu kama msaidizi wake, alikuwa anapenda utani sana, kazi zikimpungukia anauliza wasaidizi wake, alikuwa anapiga simu na kuuliza wasaidizi wake mumeo yupo au mkeo yupo, hii ilitufanya tuwe karibu naye.


“Kwa tuliofanya naye kazi saa 24 kwake hazikumtosha, alipenda kuona matokeo na matokeo ndio jibu la pekee na sio lawama, alisema amejitoa maisha yake sadaka kwa ajili ya watanzania.Sote tuliohofia sana kama anapata muda wa kupumzika na kuwa na familia yake,”amesema Rais Samia.


Akimuelezea zaidi, amesema Dk.Magufuli alikuwa mtu asiye na makuu na alikuwa mtu wa wote, alijikita kujenga uchumi wa ndani unaotegemea mapato ya ndani, alijikita kufufua na kuwekeza katika miradi ya kimkakati, azma yake ilikuwa kuwa na Tanzania ya viwanda.


Ameongeza mbali ya miradi ya kimkakati alifungamanisha maendeleo ya vitu na watu, kwa maamuzi yake hayo hakuyumbishwa na watu na ilifikia hatua akawa anaitwa tingatinga na wengine wakimuita Chuma.


“Kwa wengi Magufuli alikuwa mtu mwema na mnyenyekevu, Mungu kwake alikuwa mdomoni mwake muda wote, hakuwahi kukosa kuabudu hata akiwa kwenye ziara, alikuwa na hofu Mungu wakati wote.Aliamini kutetea haki za wanyonge na masikini.


“Msemo wake ulikuwa atasema nini kwa Mungu kuhusu watu waliomchagua na kwa tuliojua na kuwa karibu tuliona upendo, huruma na unyenyekevu uvunguni ilijificha na taaswria ya ukali iliyojificha kwenye matamshi yake,amesema.


Rais Samia amesema , Dk.Magufuli hakuwa mtu wa kusafiri kwani aliamini kutumia muda wake mwingi kuwatumikia wananchi, mbali na kutosafiri haikumzuia kushiriki na kutekeleza majukumu yake katika nchi mbalimbali, aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alitaka Sudani Kusini kuingia kwenye jumuiya hiyo.


“Alikuwa Mwenyekiti wa SADC , ambapo alitaka nchi zote kuiombea Zimbabwe kuondolewa kwenye vikwazo, alifananisha jumuiya ya SADC kama mtu, kiungo kimoja kikiumwa basi mwili wote unaumwa, hivyo alitenga siku maalum kwa nchi zote za jumuiya kupaza sauti Zimbabwe iondolewe vikwazo.


“Akiwa Mwenyekiti wa SADC aliweza kushawishi lugha ya Kiswahili itumike katika jumuiya hiyo.Hayati Magufuli alithamini mchango wa marais walimtangulia na kumlea, alitoa sif zao hadharani.


 “Niwaombe marais wastaafu na wazee wangu wa pande zote mbili pamoja na viongozi wote mimi ni kijana wenu na nipo tayari kushirikiana katika kuijenga Tanzania,nitumie fursa hii kuwaambia hakuna jambo litakaloharibika, nchi iko katika mikono salama, mimi na mwenzangu Dk.Hussein Mwinyi tutaendeleza pale alipotamani kufika, tutaulipa wema.


“Tanzania itaendelea kuwa jirani mwema na mahusiano yetu yataendelea kuwa salama na kuimarika zaidi chini ya uongozi wangu, bila kujali tofauti zetu tutumie nafasi hii kumshukuru Mungu kwa maisha yake na kuongozwa naye, tutafakari miongozo, dira ya maono yake katika kuijenga Tanzania tunayoihitaji.


“Ameondoka mapema lakini ameshamaliza kazi ambayo ilimleta duniani, ameonesha kazi zinavyotakiwa kufanya, hatuna budi kufuata njia yake, amefunga hesabu yake hapa duniani, kinachoweza kumrehemu ni sadaka alizoacha,”amesema Rais Samia. 


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akilihutubia Taifa katika Viwanja vya Jamhuri Mjini Dodoma wakati wa tukio la kutoa heshima na kuaga mwili Hayati Dk.John Magufuli aliyefariki Dunia Machi 17 mwaka huu katika Hospitali ya Mzena ,Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages