Umetimia muongo mmoja sasa tangu Saudi Arabia ilipotuma majeshi yake huko nchini Bahrain.
Ilikuwa tarehe 14 Machi 2011 wakati Saudia ilipotuma askari wake nchini Bahrain kwa minajiili ya kukabiliana na harakati ya wananchi wa nchi hiyo ya kutaka mageuzi. Swali linaloulizwa na wadadisi wa mambo ni hili kwamba, je hatua hii ya Saudia imekuwa na matokeo gani hasi ndani ya nchi hiyo na katika eneo hili la Asia Magharibi?
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, hatua hiyo ya utawala wa Aal Saud imekuwa na matokeo hasi ndani ya Saudia na Bahrain pia. Hatua hiyo imeshadidisha matatizo ya ndani ya Saudi Arabia, kwani utawala wa Aal Saud umelazimika kutumia vyanzo vyake vya fedha kwa ajili ya kuusaidia utawala wa Aal Khalifa wa Bahrain. Hii ni katika hali ambayo, katika muongo mmoja wa hivi karibuni, matatizo ya kiuchumi ya Saudia yameongezeka mno, kiasi kwamba, nchi hiyo imelazimika kupunguza ruzuku na kuongeza kodi ili kufidia nakisi kubwa ya bajeti. Utendaji huu umepelekea kuibuka malalamiko makubwa ndani ya nchi hiyo.
Fauka ya hayo, hatua ya Aal Saud ya kutuma majeshi huko Bahrain imeshadidisha mpasuko baina ya ukoo huo na jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini humo, kwani uingiliaji wa Saudia katika masuala ya ndani ya Bahrain kabla ya chochote una utambulisho wa kuzusha mifarakano na unalenga kukabiliana na jamii ya Waislamu wa madhehebu ya Shia katika nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo, kumekuweko na maingiliano na mafungamano baina ya Mashia wa Bahrain na wa Saudia.
Kwa upande wa uga wa ndani nchini Bahrain, hatua hiyo ya Saudia ilikuwa na matokeo hasi pia. Kutuma askari Saudia huko nchini Bahrain kulishadidisha pengo baina ya utawala wa kifalme wa nchi hiyo wa Aal Khalifa na wananchi, ambapo akthari ya wananchi wa nchi hiyo wanaamini kuwa, utawala wa Aal Khalifa umekiuka mamlaka ya kujitawala nchi hiyo baada ya kuruhusu nchi yao ivamiwe na kukaliwa kwa mabavu na Saudia.
Suala jingine ni kuwa, hatua ya Saudia ya kutuma askari na vikosi huko Bahrain imekuwa na nafasi muhimu katika kuchukua muda mrefu mchafuko na ukosefu wa uthabiti huko Bahrain. Lau kama utawala wa Aal Khalif ungekuwa wenyewe unakabiliana na malalamiko ya wananchi wa Bahrain bila ya msaada kutoka nje, kulikuwa na uwezekano wa kuandaliwa mazingira ya kufikiwa utatuzi wa kisiasa kwa ajili ya kuhitimisha malalamiko na maandamano ya wananchi. Hatua ya Saudia ya kutuma majeshi huko Bahrain iliandaa uwanja pia wa kuendelea na kuongezeka makabiliano baina ya wananchi na na utawala wa Manama ambapo hivi sasa utawala wa Aal Khalifa unakabiliwa na mgogoro wa kutokubaliwa kisheria na wananchi.
Hatua ya Saudia ya kutuma askari huko Bahrain ilikuwa na matokeo hasio pia katika uga wa kieneo. Moja ya matokeo hayo hasi ni ni kwamba, uamuzi huo uliandaa uwanja wa uingiliaji zaidi wa masuala ya ndani ya nchi nyingine katika ulimwengu wa Kiarabu. Tunaweza kusema kuwa, hatua ya Saudia ya kutuma askari huko Bahrain iliandaa uwanja wa kuishambulia kijeshi Yemen. Kwani watawala wa Aal Saud walikuwa na dhana hii kwamba, kama ilivyokuwa huko Bahrain ambapo kwa himaya yake wameweza kuubakkisha madarakani utawala wa Manama, kushambulia kijeshi Yemen kutapelekea pia kubakia madarakani Rais kibaraka Abdu-Rabuh Mansour Hadi na kuisambaratisha harakati ya wananchi ya Ansarullah. Hata hivyo hilo lilikuwa kosa la kimahesabu ambalo watawala wa Riyadh hawana budi kulistahamili hata baada ya kupita miaka 6 tangu kuanza hujuma hiyo ya kijeshi dhidi ya Yemen.
Nukta nyingine ni kuwa, utawala wa Saudia umekuwa na nafasi muhimu katika makubaliano baina ya Bahrain na utawala ghasibu wa Israel ya kuanzisha uhusiano wa kawaida baiana yao. Ari Shavit, mchambuzi wa masuala ya kisiasa katika Kanali ya 13 ya utawala haramu wa Israel ameashiria mchango na nafasi ya Saudia katika makubaliano baina ya Bahrain na Israel na kusisitiza kwamba, kwa kuzingatia kwamba, Manama ipo chini ya udhibitii kamili wa Saudia na si yenye kujichukulia maamuzi yake yenyewe, hii ina maana kwamba, Bahrain isingechukua uamuzi wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala bandia wa Israel pasi na kupata ridhaa ya Saudia.
Licha ya kuwa Saudia ilituma askari huko Bahrain na kuanzisha hujuma ya kijeshii dhidi ya Yemen kwa shabaha ya kuimarisha ushawishi wake wa kisiasa na kiuchumi katika eneo, lakini ushahidi unaonyesha kuwa, nafasi ya leo ya utawala wa Aal Saud ni yenye kulegalega zaidi katika eneo kuliko huko nyuma. Uingiliaji wa Saudia katika masuala ya ndani ya nchi nyingine za Kiarabu sio tu kwamba, haujaimarisha nafasi ya Riyadh, bali umepelekea nafasi yake hiyo itetereke na kulegalega zaidi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇