******************************************
Ndoa za utotoni, ukeketaji na mimba za utotoni, ni changamoto zinazowakuta watoto wengi wa kike kutoka jamii ya wamaasai.
Mkoa wa Arusha ni mkoa ambao sehemu ya mkoa huu wenyeji wake ni wamasai.
Wasichana wa jamii hii idadi kubwa imeathiriwa na mila potofu ambazo zinawafanya wengi wao wasitimize ndoto zao za elimu.
Kufuatia hali hiyo wadau mbalimbali wakishirikiana na serikali wamekuwa wakipambana kufikisha elimu itakayosaidia kubadili mitazamo hasi ya jamii hii kuhusu mtoto wa kike, pia kuwaelimisha watoto wa kike wa jamii hii ili waweze kusoma na kupinga vitendo vya ukatili dhidi yao.
Taasisi ya CWCD, yaani Center for Women and Children Development, inaendesha mradi wa klabu za watoto wa kike mashuleni ,mradi ambao unafadhiliwa na Taasisi ya Foundation for Civil Society, lengo likiwa ni kuwaweka karibu watoto wa kike hasa wa jamii ya kimasai au jamii za kifugaji, ili watambue umuhimu wa elimu, lakini zaidi ni kuwasimamia kuhakikisha wanamaliza masoamo salama.
Katika shule ya sekondari ya Elkiding’a manispaa ya Arusha shule inayomilikiwa na serikali, kuna Klabu ya wanafunzi, ambapo mmoja wa walimu walezi wa klabu hiyo mwalimu John Mduma anaeleza kuwa, shule hiyo ni kama imepata bahati ya kupata mradi huo kutoka CWCD, kwani watoto wa kike jamii ya kimasai wanachangamoto nyingi kama vile ukeketaji, mimba za utotoni na ndoa za utotoni.
Anasema kupitia klabu hizo, wasichana hao wanajengewa uwezo, kujitambua na kuthamini utu wao na zaidi ni kuhakikisha wanasoma na kumaliza salama.
“Mabinti walio katika klabu wamekuwa mabalozi wa wenzao kwani wakiona au kusikia mtoto wa kike anafanyiwa ukatili, wanatoa taarifa hapa shule, ofisi za serikali za mitaa na vijiji au kwenye nyumba za ibada” anasema mwalimu Mduma.
Baadhi ya wasichana wanaounda klabu hiyo ambayo ina wasichana wapatao 30 wanasema wamepata manufaa makubwa baada ya kujiunga na klabu hiyo kwani kwa sasa wanajitambua na wanajua aina zote za ukatili, hivyo hawako tayari kukatisha masomo yao.
“Nashauri klabu hizi zienee mashuleni hasa kwenye maeneo ya watu wa kabila la wamasai, ili wasichana wasaidike , na waweze kujilinda na kulinda wenzao dhidi ya vitendo vyovyote vinavyokatisha masomo yetu” anasema Happy Loishiye mwanafunzi wa kitado cha tatu katika shule hiyo.
naye mwanafunzi wa kidato cha kwanza katika shule hiyo ya Elkiding;a Salma Zuber, ansema alipojiunga na klabu hiyo alienda kumfahamisha mama yake na alifurahi baada ya mama yake kuridhia, maana hofu yake ilikuwa huenda mzazi wake angepingana nae.
Mwalimu Emmy Matee ambaye naye ni mlezi wa klabu hiyo anasema club hiyo imesaidia sana kuwafanya watoto wa kike na wasichana shuleni hapo kuwa majasiri.
Anasema cha kufurahisha zaidi ni namna wasichana wa shule hiyo wanavyofanya vizuri katika masomo na kwamba hii inashihirisha kwamba mtoto wa kike akihakikishiwa usalama wake na akawezeshwa kusoma , ana uwezekano mkubwa wa kufanya vizuri kwenye masomo.
Mbali na kupewa elimu na mbinu za kujitambua pia wasichana hao wanafundishwa kazi za mikono kama vile kilimo cha mbogamboga, pamoja na utengenezaji wa sabuni za maji ili kuwaandaa kujiajiri.
Mwalimu Emmy anasema mara kadhaa wamekuwa wakikumbana na changamoto za kutofautiana na wazazi au walezi kuhusu masuala ya ukeketaji au ndoa za utotoni.
Anasema wao huwa na lengo la kumuokoa mtoto lakini mzazi anaona unamuingilia katika maisha yake na utamaduni wake.
kwa upande wake Mkurugenzi wa Taasisi ya CWCD, Bi Hindu Mbwego anasema kwa kiasi kikubwa mradi umefanikiwa, kwa kuwa umeweza kupunguza matatizo hayo kwa kiasi kikubwa, na zaidi ni Serikali ya mkoa imeungana na Taasisi zisizo za kiserikali ikiwemo CWCD, katika kukomesha mila kandamizi kwa watoto wa kike wa jamii za kifugaji hali iliyoongeza ufanisi katika kufikia lengo la mradi huo.
Sheria ya mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 imelenga kuimarisha ulinzi , matunzo na haki za watoto Tanzania Bara.
Sheria hii imeaninisha haki ya kulelewa na wazazi, Haki ya kupewa jina, Haki ya kuwa na Utaifa, Haki ya kupata mahitaji ya msingi kama vile Chakula, malazi, mavazi, matibabu,chanjo, elimu, pamoja na haki ya kucheza na kuburudika.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇