Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiongea na wananchi wa Kata ya Kizota (hawapo pichani) katika mkutano uliondaliwa ili wawasilishe malalamiko yao kuhusu migogoro ya ardhi
Mzee Michael Masaka mmoja kati ya wananchi wanaolalamika maeneo yao yamevamiwa katika Kata ya Kizota
Mhe. William Lukuvi (aliyeshika mic) akifafanua kitu katika mkutano na wananchi wa Kata ya Kizota walipokuwa wanawasilisha malalamiko yao kuhusu migogoro ya ardhi. Kulia kwake ni Dkt. Suleiman Selewa, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Kushoto ni Mhe. Antony Mavunde mbunge wa Jiji la Dodoma
Bwana Lokeli Urio mmoja kati ya wananchi waliovamia maeneo katika Kata ya Kizota anayetuhumiwa kuwafukuza wananchi wenzake kwa mapanga
Bibi Mwantum Makundi, Mkazi na mwenyeji wa Kata ya Kizota akiwasilisha malalamiko yake mbele ya Waziri Lukuvi (hayupo pichani)
Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Dodoma Thadei Kabonge akipokea nyaraka za malalamiko kutoka kwa Mzee Josepahat Makwaya, mmoja kati ya wananchi wanaolalamika katika Kata ya Kizota
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi, akikagua nyaraka za umiliki kutoka kwa Bariki Kamota anayelalamika kuuziwa na Mafinga Timbers Supply Ltd maarufu kama eneo la viwanda.
……………………………………
Na Eliafile Solla, WANMM DODOMA
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi amesema ataanza kuzifanyia uchunguzi taarifa zote za migogoro ya ardhi anazopatiwa na wataalamu wake ama wananchi kabla ya kuzitolea maamuzi kwa lengo la kujiridhisha.
Alisema hawezi kuuziwa mbuzi kwenye gunia kwa kusikiliza taarifa za migogoro ya ardhi kutoka aidha kwa watalaamu wake ama wananchi na kuzitolea maamuzi ni lazima ajiridhishe kwa kuzifanyia uchunguzi yeye mwenyewe.
Lukuvi alitoa kauli hiyo tarehe 06 Februari, 2021 Jijini Dodoma alipofanya mkutano na wananchi wa eneo la Mbuyuni Viwandani Kata ya Kizota kama alivyoagiza Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 04 Februari alipokuwa katika ufunguzi wa majengo ya jeshi la Magereza.
“Nimekuja kuwasikiliza kero zenu kama nilivyoelekezwa na Mhe. Rais, lakini ni lazima na mimi nifanye uchunguzi wa haya mnayolalamikia ili nijiridhishe kabla sijafanya maamuzi kama Waziri mwenye dhamana kwa maana katika hayo maamuzi kila mtu atatendewa haki kulingana na uchunguzi nitakaoufanya’’ alisema Lukuvi.
Aidha Lukuvi aliwaambia wananchi wa Kata ya Kizota kuwa, ataunda timu maalum ya uchunguzi na atafungua ofisi katika eneo la Mbuyuni ambayo itajumuisha maofisa wa Serikali ili kumsaidia kukusanya taarifa muhimu anazozihitaji kutoka kwa wananchi hao na hatimae kutoa maamuzi yatakayomaliza migogoro yao kabisa maana bila kuchunguza migogoro hiyo haitaisha.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Wiliam Lukuvi aliwasikiliza baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo malalamiko yao yale ya jumla yanayohusu watu wengi ama makundi ya watu ambapo aliwaambia wananchi hao wawe tayari kushirikiana na timu atakayounda ambayo itafanya kazi kwa muda wa wiki mbili na kisha watampatia taarifa kwa ajili ya kuitolea maamuzi na ndani ya mwezi mmoja migogoro yao itabaki kuwa historia.
“Najua hapa kuna mtu mmoja amewauzia zaidi ya wananchi 20 viwanja na huyo mtu tunataka tumjue na uzuri timu yangu ina masikio mapana lazima itamuibua tuu kwa sababu ardhi ya Tanzania siyo mali ya mwenye nguvu wala fedha bali ni haki ya kila mtu’’ alisema Waziri Lukuvi
Lukuvi aliwataadharisha wananchi wa Kata ya Kizota kuwa, kila mtu atakufa kivyake hivyo kila anaedhani ana haki basi awe tayari kutoa taarifa sahihi kwa timu atakayounda maana hata wakitoa taarifa za uongo watapata haki katika huo uongo hivyo kila anayetaka haki itendeke ni lazima aseme ukweli ili historia ya umiliki wake ijulikane isaidie kufanya maamuzi wakati wa utatuzi wa migogoro hiyo ya ardhi.
Kizota ni miongoni mwa maeneo yaliyotwaliwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Sura Na. 113 ya Mwaka 1923 na Sheria ya Utwaaji Ardhi ya Mwaka 1967 na kuandaliwa Mpango Kabambe (master plan) mnano mwaka 1976 na kutangazwa mwaka 1978 kisha kumilikishwa kwa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) kwa Hati Na. 4585 –DLR ya mwaka 1987.
Katika kata hiyo ya Kizota, kuna maeneo ambayo yamepangwa na kupimwa kwa matumizi mbalimbali yakiwemo makazi ambayo yapo kwenye mtaa wa Kizota Relini na Mahungu, matumizi ya viwanda ambavyo vinapatikana katika eneo la Western Industrial Area (WIA) (Mbuyuni) pamoja na maeneo ya Taasisi (Eneo la Mifugo).
Eneo la viwanda ndilo ambalo Bi. Mwantumu Mussa alitoa malalamiko kwa Mh. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo eneo analolilalamikia ni kiwanja namba 172/1 lililomilikishwa kwa Mafinga Timbers Supply Ltd na ndani yake kuna wavamizi tisa ambapo watano wamefanya maridhiano na mmiliki, wanne akiwemo mlalamikaji wamegoma kufanya maridhiano na bado wanaishi ndani ya kiwanja hicho.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi amewaambia wananchi wa Kizota kwamba taarifa ya utatuzi wa migogoro yao ataitoa kwao mara timu atakayounda itakapomaliza kazi ya kuchunguza hitoria ya kila mkazi na mmiliki wa kiwanja katika maeneo yote yanayolalamikiwa na ana uhakika ndani ya mwezi mmoja atakuwa ameshatoa maamuzi yake kama Waziri mwenye dhamana ya ardhi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇