Msigwa akimuonesha Mwenyekiti wa Bodi ya Mkurabita, Balozi mstaafu Daniel Ole Njoolay moja ya nyumba zake za kisasa alizojenga eneo la Ubaruku kwa kutumia mkopo huo.
Balozi mstaafu Njoolay na Mratibu wa Mkurabita, Dkt. Seraphia Mgembe (kulia) wakitoka kutembelea Ghala la Mnufaika wa Mkurabita, Anuar Almas ambaye alikopa fedha benki kwa kutumia hakimiliki za kimila na kuamua kujenga ghala hilo ambalo ndani yake kuna mashine za kukomoa mpunga eneo la Ubaruku viwandani.
Ghala hilo linavyoonekana kwa nje huku kukiwa na lori tayari kupakia magunia ya mchele.
Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Gabriel Mfune akisoma taarifa ya wilaya kuhusu mafanikio ya Mkurabita wilayani humo.
Afisa Ardhi na Maliasili wa Wilaya ya Mbarali, Geofrey Mwaijobele akisoma risala ya wilaya kuhusu mafanikio na changamoto za urasimishaji mali za wanyonge wilayani humo.
Mratibu wa Mkurabita, Dkt. Seraphia Mgembe akitoa maneno ya utangulizi kabla ya kumkaribisha kuzungumza, Mwenyekiti wa Bodi, Balozi mstaafu Njoolay.
Balozi mstaafu Njoolay akizungumza wakati wa kikao hicho ambapo alifurahishwa na mafanikio waliyoyapata wanufaika wa Mkurabita wilayani humo.
Wanufaika wa Mkurabita wakiwa katika picha ya pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya Mkurabita, Balozi mstaafu Njoolay (kushoto waliokaa), Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Mfune, Makamu Mwenyekiti wa Mkurabita, Immaculate Senje na Mratibu wa Mkurabita, Dkt. Mgembe.
Na Richard Mwaikenda, Mbarali
ZAIDI ya sh bil. 19 zimetolewa mkopo kwa wananchi 988 kwa kutumia Hati za Hakimiliki za Kimila Kama dhamana benki wilayani Mbarali, Mbeya.
Wananchi hao walionufaika na Mpango wa Kurasimisha Ardhi na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita), wamekopeshwa na benki za Nmb, CRDB pamoja na Access.
Taarifa hiyo imetolewa na Afisa Ardhi na Maliasili wa Wilaya ya Mbarali, Geofrey Mwaijobele, alipokuwa akisoma hivi karibuni taarifa ya wilaya wakati wa kikao cha wadau na Kamati ya Uongozi ya Mkurabita, mjini Mbarali.
Walionufaika na mikopo hiyo ni wamiliki wa Ardhi,mifugo na wenye nyumba zenye Hati za Hakimiliki za Kimila ambapo wengi wao fedha wamezitumia kuwekeza katika kilimo ikiwemo kununua pembejeo na stakabadhi ghalani pamoja na kulipia ada za watoto wao shuleni.
Mwaijobele amesema kuwa wanufaika hao wa Mkurabita baadhi yao wamefikia kukopa hadi sh. Mil. 70 kwa kutumia hati hizo ambazo zimeanza kukubalika na taasisi za fedha.
Pia, alitaja baadhi ya vikundi vya wakulima vilivyonufaika na mikopo hiyo kuwa ni; Herman Group cha Kata ya Ihahi, Motombaya Irrigation System cha Kata ya Mahongole na Kongolo Mswisi Irrigation System kutoka Kata ya Kongolo.
Alieleza kuwa hali ya urejeshaji wa mikopo ni ya kuridhisha Sana ambapo ni asilimia 95 kwa kila Mwaka.
"Licha ya kuwepo kwa fursa hizi za mitaji bado Kuna changamoto za mwamko ndogo wa wananchi na vikundi kuchangamkia fursa hizi adhimu," alisema Mwaijobele.
Mratibu wa Mkurabita, Dkt. Seraphia Mgembe amewaasa wanufaika kuacha uchoyo kutoa elimu waliyopata kwa wenzao ili nao wanufaike na fursa ya Hati za Hakimiliki za Kimila kukopea mikopo benki kama dhamana wapate fedha za kuanzishia miradi ili nao waondokane na umasikini.
"Inatakiwa nyie mliopata msiwe wachoyo, inatakiwa mtoe elimu kwa wenzenu, unapozidi kumuelimisha mwenzio na wewe pia unazidi kuelimika," alisema Dkt Mgembe.
Aidha, Dkt Mgembe alisema kuwa Serikali kazi yake ni kuweka miundombinu kama ilivyo Mkurabita kuhakikisha kila mtu huko aliko anapata huduma anafanyiwa jambo ambalo naye atajiona ana thamani katika nchi yake. lakini inatakiwa na wao wawe na uthubutu.
Naye, Balozi mstaafu Njoolay aliwapongeza viongozi wa Wilaya ya Njombe kwa ushirikiano walionao wa kuhamasisha wananchi katika suala la urasimishaji ardhi na nyumba jambo ambalo liwewafanya watu wengi wawe na Hati za Hakimiliki za Kimila wanazozitumia kukopea fedha kwenye mabenki.
"Nimefurahi sana kuona wanufaika walivyotoa ushuhuda mzuri jambo ambalo linaonesha kazi nyingi imefanyika matokeo mengi yamonekana ingawa watu wengi hawajui,hivyo inatakiwa uhamasishaji mkubwa sana ufanyike," alisema Mwenyekiti wa Bodi ya Mkurabita Balozi mstaafu Njoolay.
Wadau waliopata fursa ya kuzungumza katika kikao hicho waliishukuru sana Mkurabita kwa kuanzisha suala la urasimishaji wa mali za wanyonge kiasi cha kupata hakimiliki za mali zao na kunufaika nazo kwa kupata mikopo benki.
Baada ya kikao hicho kumalizika, Kamati ya uongozi wa Mkurabita ikiongozwa na Balozi mstaafu Njoolay waliondoka kwenda kuangalia baadhi ya miradi ya wadau wanufaika wa Mkurabita akiwemo Paulinus Msigwa ambaye aliwaonesha pembejeo za kisasa ikiwemo matrekta, mitambo ya kulimia na kupandia mpunga. Pia aliwanonesha moja ya nyumba zake aliyojenga eneo la Ubaruku.Alianza kukopa sh. milioni 20, hivi sasa anakopa hadi sh. mil. 70.
Ujumbe huo ulikwenda pia kuona mradi wa stakabadhi ghalani eneo la viwanda Ubaruku ambapo mnufaika Anuary Almas ambaye pia alikopa benki kwa kutumia hakimiliki ya kimila na kujenga ghala ambamo aweka mashine za kuchakata mpunga pamoja na kuhifadhi mchele kwa malipo kabla haujaenda kwa walaji.
Pia kati ya wadau walionufaika na hati hizo ni wafugaji wa jamii ya kimasai,Tirike Sandetwa na Taras Taikoo ambao wamekopa fedha fedha benki na kuanzisha miradi ikiwemo mashamba eneo la Mogelo na kusaidia kulipia ada za watoto wao sekondari na vyuoni.
IMEANDALIWA NA;
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇