Waandishi wa habari wakisikiliza kwa makini wakati Sebasyian Kitiku akizungumza katika mkutano huo ambao pia walipata wasaa wa kuuliza maswali.
Wizara
ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
MAADHIMISHO YA SIKU YA
KIMATAIFA YA KUPINGA UKEKETAJI DHIDI YA MWANAMKE NA MTOTO WA KIKE TAREHE 6
FEBRUARI, 2021
Ndugu Wanahabari,
Awali
ya yote namshukuru Mwenyezi
Mungu, kwa kutujalia afya njema na
kutuwezesha kukutana mahali hapa
kwa nia ya kuongea na wananchi hususan wazazi, walezi na jamii kupitia ninyi
ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji kwa
Mwanamke na Mtoto wa Kike.
Ndugu Wanahabari,
Maadhimisho haya hufanyika tarehe 6 Februari ya kila
mwaka. Hii inatokana na Azimio la Umoja
wa Mataifa la mwaka 2003 na nchi yetu kuridhia lililoelekeza nchi zote
wanachama wa Umoja wa Mataifa kukomesha vitendo vya ukeketaji kwa wanawake na
watoto wa kike. Tangu kipindi hicho Tanzania kama nchi mwanachama wa Umoja wa
Mataifa imekuwa ikifanya kumbukizi ya siku hii kwa kuelimisha jamii inayofanya
ukeketaji madhara ya mila na desturi ya ukeketaji ili jamii iiache hasa wakati
wa sherehe za uvushaji rika kwa watoto wa kike. Hivyo, maadhimisho haya
yanatupa fursa ya kujipima ni kwa namna gani tumeweza kukabiliana na ukeketaji
na kushughulikia changamoto zilizojitokeza katika mapambano haya ili kubuni
mikakati mipya ya kutokomeza ukeketaji nchini.
Ndugu Wanahabari,
Taarifa ya utafiti wa Hali ya Watu, Afya na viashiria vya
Malaria Tanzania (TDHS) ya mwaka 2015/16 inaonyesha kuwa mwanamke 1 kati ya 10
amekeketwa. Aidha, mikoa inayoongoza kwa ukeketaji ni Manyara (58%), Dodoma
(47%), Arusha (41%), Mara (32%) na Singida (31%). Takwimu
za kitaifa za ukeketaji ni asilimia 10. Takwimu katika Mikoa hiyo zinaonyesha kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya
katika kutokomeza ukeketaji nchini. Sababu zinazotajwa
kusababisha wanawake na wasichana kukeketwa ni pamoja na mila na desturi za
baadhi ya Jamii zinazoamini kwamba ukeketaji unazuia au unatibu magonjwa ya
mfumo wa uzazi, hifadhi ya ubikira au usafi wa moyo, heshima katika familia,
hofu ya kutengwa kijamii pamoja na wanawake wengi kuamini kwamba wasipokeketwa
hawajakamilika kuchukua majukumu ya familia anapoolewa.
Ndugu Wanahabari
Ukeketaji una athari kubwa kwa wanawake na watoto wa kike kijamii na
kiafya. Athari katika kijamii zinahusisha kuendeleza ukatili dhidi ya watoto
ikiwa pamoja na kuchochea ndoa za utotoni, kwa kuwa baada ya kukeketwa mtoto
yupo tayari kuolewa. Aidha, Mwanamke asiye keketwa hutengwa na jamii hivyo
kusababisha unyanyapaa na kuongezeka kwa idadi ya wanawake na watoto wenye
msongo wa mawazo ambapo watoto hushindwa kushiriki vema katika masomo na hatimaye
kushindwa kutoa mchango katika ujenzi wa Taifa.
Vilevile, ukeketaji
kufanywa kwa kutumia vyombo au vifaa kama vile visu au nyembe zisizotakaswa ambapo
kifaa kimoja huweza hutumika kukeketa zaidi ya msichana mmoja jambo ambalo linaweza
kusababisha maambukizi ya magonjwa ya zinaa na Virusi Vya UKIMWI (VVU). Madhara
mengine ni pamoja na kutokwa na damu nyingi katika jeraha ambapo huweza
kusababisha kifo, uharibifu wa mfumo wa nje wa sehemu za uzazi pamoja na matatizo
wakati wa kujifungua ambayo yanaweza kusababisha ugonjwa wa fistula.
Ndugu Wanahabari
Kaulimbiu
ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji kwa mwaka 2021 ni “Wakati
ni huu: Tuungane kutokomeza Vitendo vya Ukeketaji”
Kaulimbiu ya mwaka
huu, inahimiza umuhimu wa Jamii na Wadau wote kuunganisha nguvu ili kushiriki
katika kutokomeza ukeketaji nchini. Wadau
hao wanajumuisha Serikali katika ngazi zote, Mashirika Yasiyo ya Serikali, Mashirika
ya Umoja wa Mataifa, viongozi wa dini, viongozi wa kimila, watu mashuhuri,
wazazi na jamii kwa ujumla ili kila mmoja aone ana wajibu katika kutokomeza
ukeketaji. Aidha, ushirikiano huu unahitajika zaidi sasa, kipindi ambacho mila
ya ukeketaji inaenea kwa kasi katika baadhi ya Mikoa niliyoitaja.
Ndugu Wanahabari;
Mwaka 2017 Serikali kwa kushirikiana na wadau iliandaa
Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto
(2017/18-2021/22). Mpango unalenga kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya
wanawake na watoto katika jamii yetu kwa asilimia 50 ifikapo 2022. Katika
Mpango kazi huu, vitendo vya ukeketaji vimeainishwa kuwa ni ukatili dhidi ya
watoto wa kike na hivyo vinapaswa kutokomezwa.
Katika kushughulikia
tatizo la ukeketaji nchini, Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza
Ukeketaji Tanzania (2019-2022), kupitia mkakati huu, Serikali kwa kushirikiana
na wadau mbalimbali itaendelea kutoa
elimu kuhusu athari za ukeketaji, kuimarisha mifumo ya kushughulikia ukeketaji na
kuboresha huduma kwa waathirika wa vitendo vya ukeketaji.
Ndugu Wanahabari;
Hatua nyingine ambazo Serikali imechukua ni pamoja na kuandaa
Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008, Sera ya Maendeleo ya Wanawake na
Jinsia ya mwaka 2000 na kutunga Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 kwa lengo
la kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili ukiwemo ukeketaji ikiwa pamoja
na kudumisha utu na heshima ya mwanamke nchini. Aidha, Serikali imefanya
marekebisho katika Sheria ya Kanuni za Adhabu Sura ya 16 ya mwaka 2002, kifungu
cha 158(1) (a) ambayo inazuia ukeketaji kwa mtoto wa kike.
Ndugu Wanahabari;
Kuna changamoto ya
ukeketaji wa kuvuka mipaka kwa nchi zetu za ukatanda wa Afrika Mashariki na
pembe ya Afrika ambapo Jamii ya nchi mmoja huvuka mipaka kwa ajili ya ukeketaji
katika nchi nyingine na kurudi ili kukwepa mkono wa sheria. Kwa kutambua hilo,
mwaka 2019, Serikali za nchi za Uganda, Kenya, Somalia na Ethiopia ziliingia
makubaliano ya kukabiliana na ukeketaji wa kuvuka mipaka kwa kutekeleza Mpango
Kazi wa pamoja wa Kuzuia Ukeketaji Kupitia Mipakani. Mpango huo ulianzishwa
kuzuia watoto wasisafirishwe kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine kwa lengo la
kukeketwa.
Tanzania
tumetekeleza makubaliano hayo kwa kuzijengea uwezo Kamati za Usalama katika
Wilaya ilivyopo vituo vya mipakani vya Sirari (Tarime), Holili (Rombo), Namanga
(Longido) na Horohoro (Kilindi) ili kuelewa mbinu zinazotumika kuwasafirisha
watoto hao na hatua za kuchukua punde tukio hilo linapotokea. Pia, Wizara kwa
kushirikisha Halmashauri zilizopo mipakani zimeandaa jumbe mahsusi za
kuelimisha jamii kuhusu madhara ya ukeketaji na athari za kusafiri kwa kuvuka
mipaka bila vibali. Jumbe hizo zitawekwa sauti ili kutumika katika redio za
Kijamii zinazopatika katika maeneo yenye ukeketaji katika mipaka.
Ndugu Wanahabari;
Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya ukeketaji
kwa mwaka 2021 yatafanyika Kimkoa; ambapo Wizara itaungana na Mkoa wa Arusha tarehe
19 Februari, 2021 katika kufanya shughuli zifuatazo;
1. Kongamano la Wadau wa masuala ya ukeketaji kujadili mbinu
za kukabiliana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto ikiwa pamoja na mimba,
ndoa za utotoni na ukeketaji.
2. Uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Kutokomeza Ukeketaji (2019-2022)
Mwisho,
Ni matarajio yangu
kuwa Wazazi au Walezi, Jamii na Wadau wote wanaoshughulika na masuala ya watoto
wataunga mkono juhudi za Serikali katika kuwalinda watoto wetu dhidi ya
ukeketaji. Aidha, niwaombe wanahabari kuendelea kuelimisha jamii kuhusu madhara
ya ukeketaji ili jamii iweze kufahamu na kushiriki katika kuchukua hatua za
kutokomeza mila na desturi hii yenye madhara kwa wanawake na watoto wa kike. Niwaombe kwa mara nyingine, muendelee kufichua
vitendo vyote vya ukatili dhidi ya watoto ili hatua stahiki zichukuliwe.
Naomba nitoe wito
kwa wananchi hasa wale waliopo kwenye mikoa yenye kiwango cha juu cha Ukeketaji
kuzingatia kuwa jukumu la kutokomeza ukeketaji ni la kila mtu na si la Serikali
peke yake, hivyo kila mtu atimize wajibu wake kama kauli mbiu ya Siku ya
Kimataifa ya Kutokomeza Ukeketaji inavyotuelekeza kwamba
“Wakati ni huu: Tuungane kutokomeza Vitendo
vya Ukeketaji”
Nawashukuru sana kwa kunisikiliza
Ndugu Mdau nakuomba uendelee kusikiliza clip hii ya video wakati Kitiku akielezea masahibu wanayopata wanaokeketwa...
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇