WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa muongozo mpya kuhusu kodi za majengo, ushuru wa mabango na vitambulisho vya wajasiliamali leo Februari 1,2021 jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwanaidi Hamis akitoa msisitiza kwa wafanyabiashara kuhakikisha wanalipa kodi stahiki kwa Serikali leo Februari 1,2021 jijini Dodoma.
Baadhi ya waandishi na watumishi wa TAMISEMI wakifatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo (hayupo pichani) wakati akitoa muongozo mpya kuhusu kodi za majengo, ushuru wa mabango na vitambulisho vya wajasiliamali leo Februari 1,2021 jijini Dodoma.
…………………………………………………………………………………..
Serikali imetoa muongozo mpya ambapo kuanzia sasa kodi za majengo, ushuru wa mabango na vitambulisho vya wajasiriamali vitasimamiwa na wakurugenzi wa Halmashauri husika tofauti na awali ambapo vilikuwa vikisimamiwa na Mamlaka ya mapato TanzaniaTRA, ikiwa ni lengo kuimarisha ukusanyaji wa mapato.
Wakitoa kauli ya pamoja kati ya Wizara ya Fedha na Mipango na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na serikali za mitaa TAMISEMI, Waziri wa OR TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo amesema kuwa serikali imeamua kutoa madaraka kwa wakurugenzi wa Halmashauri kusimamia vitengo hivyo kwa kuwa hao ndio wenye wigo mpana zaidi hadi ngazi za Mitaa.
Amesema wakurugenzi wa Halmashauri sasa watakusanya kodi za majengo yote ikiwa na lengo la kuongeza wigo wa kukusanya mapato kutokana na uwanda wa sarikali za Mitaa kuwa mpana zaidi na kuyafikia majengo yaliyokusudiwa.
“Tumeamua kukubaliana Wizara hizi mbili kuwa sasa mapato yote yakusanywe na Wakurugenzi wa Halmashauri ili wigo uwe mpana zaidi kodi za majengo yote zitakusanywa na Wakurugenzi na kuziingiza Serikalini” amesema Waziri Jafo.
Amewataka wakurugenzi kuwashirikisha Maafisa biashara, na watendaji wa ngazi zote kuhakikisha wanasimamia vizuri zoezi hilo liweze kuleta tija kuhakikisha majengo yote yanalipiwa kodi inayositahili na Serikali inapata mapato stahili.
Kuhusu ushuru wa mabango amesema Wakurugenzi watakusanya ushuru wa mabango yote yaliyopo katika maeneo yao yaliyokuwa yakikusanywa na Mamlaka ya mapato TanzaniaTRA, isipo kuwa mabango yanayosimamiwa na Wakala za bara bara TANROADS na TARURA.
“Mabango yote yaliyokuwa yanasimamiwa na TRA sasa yote yatakuwa chini ya wakurugenzi tunaamini ufanisi utaongezeka kwa kuwa Wakurugenzi wanayajua mabango yote yaliyokatika maeneo yao kila aina ya bango na sehemu lilipo katika eneo hilo tunataka kuona ufanisi mkubwa wa ukusanyaji wa mapato” amesema.
Kuhusu vitambulisho vya wajasiliamali Waziri Jafo amesema vitambulisho vipya vya wajasiliamali tayari vimechapishwa na kupelekwa katika ofisi za TRA kote nchini na sasa vitakuwa chini ya Wakuu wa Mikoa na sasa Wakurugenzi wakachukue tayari kuwafikia wajasiliamali kote nchini.
Mhe.Jafo amesema kuwa vitambulisho hivyo sasa vitasimamiwa na wakurugenzi wa Halmashauri katika kufikisha kwa wajasiliamali na kutaka usimamizi madhubuti kuhakikisha zoezi hilo linakwenda vizuri na Serikali inapata mapato.
Amesema vitambulisho hivyo vilivyoboreshwa vitapatikana kwa bei ile ile ya shilingi elfu ishirini (20,000) kwa kitambulisho kimoja kitachomuwezesha kufanya biashara mwaka mzima, na hakuna mjasiliamali yeyote hapa nchini kufanya biashara bila kuwa na kitambulisho.
Hata hivyo Mhe.Jafo amesema kuanzia sasa serikali haitarajii mfanyabiashara kufanya biashara bila kuwa na Cheti cha kulipa kodi ya TRA, leseni ya biashara ya Halmashauri au kitambulisho cha wajasiliamali, sheria kali zitachikuliwa kwa watu kama hao.
Aidha ameonya kwa wafanyabiashara wakubwa wanaokwepa kodi kwa kutoa vitu kwenye maduka kwenda kwa wajasiliamali bila kuwa na lisiti ya bidhaa hizo, na kuwa Serikali imeweka mkazi mkali na kuwataka wafanyabiashara kutoa lisiti na mteja anayenunua bidhaa kuhakikisha anadai lisiti.
Amewataka wakurugenzi wa Halmashauri zote kuhakikisha wanasimamia vizuri zoezi hilo kuhakikisha maagizo yote yaliyotolewa na Serikali yanasimamiwa kikamilifu kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa wa kukusanya mapato ili kuwahudumia wanchi, huku akibainisha maelekezo maalumu ya maagizo hayo watapatiwa katika vikao kazi.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwanaidi Hamis amewasisitiza wafanyabiashara kuhakikisha wanalipa kodi stahiki kwa Serikali ili Serikali iweze kujiendesha, na kuwataka wasimamizi katika kodi za majengo, Mabango na Vitambulisho vya wajasiliamali kusimamiwa kikamilifu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇