IKULU, Dar es Salaam
Rais Dk. John Magufuli amemtumia Salamu za rambirambi Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad kilichotokea Jijini Dar es Salaam, leo.
Katika salamu hizo, Rais Magufuli amemuomba Rais Mwinyi kufikisha salamu za pole kwa familia ya Marehemu, Wazanzibari wote, Wanachama wa ACT – Wazalendo, ndugu, jamaa na marafiki wote walioguswa na kifo hicho.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar. Natoa pole kwa Rais wa Zanzibar Mhe. Dkt. Mwinyi, Familia, Wazanzibari, wanachama wa ACT-Wazalendo na Watanzania wote. Mungu amuweke mahali pema peponi, Amina” amesema Rais Magufuli.
Amewataka wafiwa wote kuwa na moyo subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi na amemuombea Marehemu apumzike mahali pema.
Kufuatia msiba huo, Rais Magufuli ametangaza siku 3 za maombolezo ya Kitaifa kuanzia leo tarehe 17 Februari, 2021 ambapo bendera zote zitapepea nusu mlingoti.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇