LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 7, 2021

MKURABITA YATINGA KIKAZI ZANZIBAR, KUKUTANA NA RAIS DKT HUSSEIN MWINYI

 

KAMATI  ya Uongozi ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA), inatarajia kukutana na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein  Ali Mwinyi wakati wa  ziara ya kikazi ya siku nne  Zanzibar  inayoanza  tarehe 8 hadi 11 Februari 2021.

 


Wajumbe wa Kamati pamoja na menejimenti ya MKURABITA wanaoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi,  Balozi mstaafu Daniel Ole Njoolay watapata fursa ya kukutana na Rais wa Awamu ya Nane na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa ajili ya kumpongeza na kuelezea jinsi MKURABITA ilivyojipanga katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi , 2025 kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 143.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurabita

kwa vyombo vya habari, ziara hiyo ni mwendelezo wa ziara iliyofanyika mwezi Januari 2021 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Mbarali na Mji Njombe kwa upande wa Tanzania Bara. Timu hiyo inaondoka leo kwenda Zanzibar.

 

Taarifa hiyo iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano cha Mkurabita, inaeleza kuwa lengo la ziara ni kufuatilia na kujionea utekelezaji wa shughuli za urasimishaji nchini ili kamati iweze kushauri na kutoa maelekezo kwa ajili ya kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa ajenda ya uwezeshaji wananchi kiuchumi kupitia urasimshaji rasilimali ardhi na biashara.

 

Ikiwa Zanzibar, Kamati inatarajia kukutana na watendaji wanaotekeleza na kusimamia shughuli za urasimishaji, kushiriki zoezi la utoaji wa hati za matumizi ya ardhi katika Wilaya ya Kaskazini A, kutembelea kituo jumuishi cha urasimishaji na uendelezaji biashara kilichopo Darajani, Wilaya ya Mjini pamoja na kuwatembelea baadhi ya wananchi walionufaika na shughuli za urasimishaji na kusikia shuhuda zao kuhusu tija na manufaa yaliyopatikana.

 

 

Baadhi ya shughuli ambazo zimetekelezwa na MKURBITA Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara za Kisekta pamoja na taasisi mbalimbali za umma ni pamoja na upimaji wa jumla ya viwanja 8,552 vimetambuliwa, hati za matumizi ya ardhi 7,625 zimesajiliwa na zinaendelea kutolewa kwa wananchi. Aidha, MKURABITA kwa kushirikiana na wizara inayohusika na masuala ya biashara imetoa mafunzo kwa wafanya biashara 2,600 na kurasimisha jumla ya biashara 1,289. 

 

Shughuli za urasimishaji ardhi na biashara zinaendelea ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa vituo jumuishi vya urasimishaji na uendelezaji biashara Zanzibar na kutoa mafunzo ya kujenga uwezo wa wananchi waliorasimisha ardhi ili kuwawezesha kuunganishwa na huduma za ukuzaji wa mitaji yao na fursa mbalimbali za kiuchumi ikiwemo uwekezaji nje na ndani ya Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages