LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Feb 19, 2021

KANISA HALISI LAANDAA IBADA MAALUM YA SIKU MBILI YA KUFUTA HOFU NA TAHARUKI DHIDI YA KORONA KATIKA TAIFA LA TANZANIA

Kiongozi wa Kanisa Halisi la Mungu Baba, Baba wa Uzao Halisi alipokuwa akiendesha Ibada Maalum ya kuifunga Corona katika Taifa la Tanzania, ugonjwa huo ulipongia kwa mara ya kwanza hapa nchini. Ibada hiyo Maalum ilifanyika Jumapili Machi 15, 2020 katika Makao Makuu ya Kanisa hilo, Tegeta. Wakati huo Ibada na maombi yalifanywa na dini mbalimbali baada ya Rais Dk. John Magufuli kuwaelekeza Watanzania wote kufanya hivyo ambapo baadaye ugonjwa huo ulitoweka kabla ya kurudi tena mwaka huu.(Picha ya Maktaba ya CCM Blog).


CCM Blog, Dar es Salaam

WAKATI Rais Dk. John Magufuli alipokuwa akiongoza kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi Balozi John Kijazi, Jijini Dar es Salaam, leo amewataka Watanzania kuondoa hofu katika kipindi hiki ambacho dunia inapitia wakati mgumu wa kukabiliana na janga la Korona na badala yake wachukue tahadhari na kumtanguliza Mungu na pia Rais huyo kutangaza siku tatu za maombi na kufunga kuanzia leo, Kanisa Halisi la Mungu Baba, limeandaa Ibada Maalum ya kufuta hofu na taharuki dhidi ya ugonjwa huo wa Korona katika Taifa la Tanzania.


Taarifa iliyotolewa leo na Mkuu wa Kanisa hilo lenye Makao yake Makuu Tegeta jijini Dar es Salaam anayetambuliwa na Kanisa hilo kwa jina la Baba wa Uzao Halisi, imesema Ibada hiyo Maalum itafanyika kwa siku mbili kuanzia kesho Jumamosi na keshokutwa Jumapili katika Katika Makao Makuu ya Kanisa hilo na amewaomba Waumini wa Kanisa hilo na Watanzania wengine wote bila kujaii itikadi au Dini zao wenye mapenzi mema na Taifa wahudhurie Ibada hiyo.


"Katika taharuki na hofu ambayo imeletwa na dunia, Ushindi uko katika kuendesha Ibada ya kuliinua Taifa zima na Rais wake Dk. John Pombe magufuli ili tusiwe na hofu, huku tukijua aliyetuumba na kutuvusha wakati wote, hawezi kutuacha kamwe.


Kwa ufupi, lazima tumwinue Rais na Wasaidizi wake wote kisha Wananchi ili mlango wa hofu ufungwe milele Wote.  TUMEPONA SOTE TUSHANGILIE, aliyetuumba anaonekana kwa sura ya Taifa la Tanzania.", amesema Baba wa Uzao Halisi katika taarifa hiyo na kuongeza;-


"Hata kwa upande wa Tanzania ni Taifa la Watendao kwa Haki, maana ni Chanzo cha Baraka. Mataifa ambayo walidhani kuwa ni wao, wanachukia na kutumwagia vitu vibaya hewani kwa chuki zao.  Kwa nguvu za kawaida ni wakubwa, ila kwa Sauti hii, tumpishe aliyeumba kila kitu ili asababishe wao kwa wao kukatana mapanga.  Sisi tutaokota nyara tu. Hakuna aliyejiumba, aliyeumba kila kitu yupo, na yuko tayari kuingilia kati ili kufuta hofu iliyotanda.  Tusiogope tufute hofu".


Ifuatayo ni Taarifa Kamili ya Baba wa Uzao Halisi akidokeza somo litakaloendesha Ibada hiyo Maalum, Tafadhali isome hapo👇

 

IBADA MAALUM YA KUFUTA HOFU, MASHAKA, WASIWASI NA WOGA WA KORONA KATIKA TAIFA LA TANZANIA 18-19 Kisleu, Vol.2 (20-21 Februari, 2021)

     

UFUNGUO

Lango la 11 Kisleu, Vol.2 (13 Februari, 2021) nilienda Kigoma kufanya mazungumzo na Viongozi wa Mji wa Kigoma–Ujiji na Wazee wa Mji huo, kuhusu HIJA YA CHANZO HALISI, itakayofanyika mwezi ujao nikakuta hofu ya matangazo ya shirika la Afya Duniani.

 

Baada ya Mkutano ule nilirejea Dar-es-Salaam kupitia Dodoma na kukuta Binti aliyenipokea, na kunisalimia kwa lugha inayosema kuwa “Baba angani wamemwaga sumu nyingi tuna hofu.”  Nilifanya Ibada asubuhi ya kufuta kifo na mauti kupitia 1Wakorintho 15:26 na nikaacha Amani, Furaha na Utulivu kwa mujibu wa Isaya 35:10.

 

Nilipofika Dar-es-Salaam, nilimuuliza askari pilosi ninayefuatana naye safarini kuwa baada ya kufika Mjini ameona kitu gani? Alinieleza kuwa hofu ya korona  kutokana na kuondokewa na Viongozi wao ( hata kama si kwa sababu ya korona) ni kubwa.

 

KUFUTA HOFU NA TAHARUKI KATIKA TAIFA

Katika Kitabu, tunafunguliwa hofu, wasiwasi, mashaka na woga kwa kusoma vifungu vifuatavyo:

·                  2Wafalme 6:8-23;

·                  2Nyakati 20:1-26; na

·                  1Wafalme 20:1-34

 

(A)        2Wafalme 6:8-23

Katika Kifungu hiki, tunajifunza kuwa kuna kipindi Mfalme wa Shamu, ambaye alikuwa analichukia Taifa la Watendao kwa Haki, alishangaa kwa nini kila akitaka kushambulia Watendao kwa Haki katika Taifa hilo hafanikiwi?

 

Ndipo akauliza kama kuna anayepeleka yale anayoongea kinyume. Wakamueleza kuwa kuna Nabii ambaye huwa anajua mabaya anayonuia kuwafanyia Wanaotenda kwa Haki. Mfalme wa Shamu, anayechukia Taifa la Watendao kwa Haki, aliagiza wapeleke majeshi kumzingira Nabii ili akiamka wamkamate!

 

Msaidizi wake Nabii, Geazi aliamka asubuhi akakuta Jeshi la Shamu limezingira Nyumba ya Nabii. GEAZI ALIOGOPA SANA NA KUMWELEZA NABII KUWA OLE WETU, MAJESHI YA SHAMU YAMETUZINGIRA!  NABII ALIMWAMBIA KUWA “USIOGOPE WALIO UPANDE WA TAIFA LINALOTENDA KWA HAKI NI WENGI MNO KULIKO MAADUI ZETU”

Ndipo Nabii aliona haitoshi, akaomba Geazi afunguliwe macho ili na yeye aone walioupande wa wenye haki ili awe na ujasiri kama Nabii alivyo na ujasiri.

 

UFAFANUZI

Dunia inamchukia  Rais Dkt Magufuli kwa sababu ya kuishi kwake Moyo na hawataki Sifa za Moyo zinazoendelea katika Taifa la Tanzania kupitia yeye, kwa maana ya:

+   Uchumi wa Kati; 

+   Umeme kila mahali;

+   Barabara kila mahali;

+   Madaraja;

+   Barabara za juu kwa juu (flyovers);

+   Watoto kwenda Shule bure, Darasa la Kwanza hadi Kumi na Mbili;

+   Mvua kunyesha;

+   Vyakula tele;

+   Kuponywa bure korona na Aliyetuumba; na

+   Mengine mazuri, kama vile Amani na Utulivu katika Taifa kwa ujumla.

 

Kuna Taharuki kubwa ambayo imeleta Hofu kama ilivyotokea kwa Geazi,  baada ya kuondokewa na viongozi kadhaa wanaopendwa na wananchi. Kilichomponya Elisha na Geazi, ni Elisha kufanya Ibada ya kumfungua macho Geazi ili aone kama Nabii. KANISA HALISI LA MUNGU BABA, TUMEANDAA IBADA YA KUFUTA HOFU NA TAHARUKI ili kila mmoja katika Taifa ajue MUNGU BABA aliyeumba kila kitu anatupenda mno.

 

Baada ya Geazi (yaani Wananchi) kuona kuwa walioko upande wa Tanzania kutoka kwa Aliyetuumba ni wengi kuliko Mataifa yanayotuonea wivu, shida iliishia pale.

 

SILAHA ALIYOTUMIA NABII ELISHA

Aliwasamehe bure wale waovu kwa mujibu wa Ayubu 42:10 na Isaya 43:25, hawakurudia tena kulishambulia taifa la watendao kwa haki. Soma vizuri 2Wafalme 6:16-23, utaona hiyo hoja.

 

(B)        2Nyakati 20:1-26

Katika mistari hii kuna Mataifa matatu Makubwa ambayo yalivamia “physically” Taifa la Watendao kwa Haki. Mfalme Yehoshefati aliogopa, ikabidi aite Nchi nzima kuuliza afanye kitu gani?  Maana kwa kuangalia kwa macho ilionekana nguvu ya Mataifa yaliyokuwa yamemvamia ni kubwa, akajiona hawezi.

 

Nguvu na uweza wa MUUMBA WA KILA KITU vikaingia ndani ya Nabii katika lile Kusanyiko lililoitwa na Mfalme Yohoshefati na kumwambia kuwa “Asiogope maana vita si yake bali ni ya Yeye Aliyempaka mafuta, yaani Muumba wake.

 

Katika mstari wa 20, Mfalme Yehoshefati alikubali na kutii na kuwaeleza watu wake kuwa “Wamwamini Aliyewaumba wathibitike pia waamini na Nabii aliyetamka ili wafanikiwe.” yaani washinde.

 

Yehoshefati aliandaa Waimbaji ambao waliimba kwa Uzuri na Utakatifu, kisha Malaika waviziao wakaingia kazini, yale Mataifa Makubwa yaliyokuwa yamevamia Taifa la Watendao kwa Haki walikatana mapanga wao kwa wao.

 

UFAFANUZI

Hata kwa upande wa Tanzania ni Taifa la Watendao kwa Haki, maana ni Chanzo cha Baraka. Mataifa ambao walidhani kuwa ni wao, wanachukia na kutumwagia vitu vibaya hewani kwa chuki zao.  Kwa nguvu za kawaida ni wakubwa, ila kwa Sauti hii, tumpishe Aliyeumba kila kitu ili asababishe wao kwa wao kukatana mapanga.  Sisi tutaokota nyara tu. Hakuna aliyejiumba, Aliyeumba kila kitu yupo, na yuko tayari kuingilia kati ili kufuta Hofu iliyotanda.  TUSIOGOPE, TUFUTE HOFU.

 

(C)        1Wafalme 20:1-34

Hapa ni patamu zaidi katika Somo hili la kupata ufahamu wa Faida ya Kufuta Hofu na Taharuki.  Mfalme wa Shamu, akiwa na wenzake 32, alimtishia Mfalme wa Taifa la Watendao kwa Haki.  Akamwambia kuwa “Fedha, dhahabu, wakezo na watoto wako na kila kitu chako kizuri ni changu.” Mfalme wa Shamu alituma Jeshi lake ili liende kuchukua vitu hivyo!

 

Mfalme wa Shamu alipoona kuwa Mfalme wa Taifa Linalotenda kwa Haki amekubali tishio la kwanza, akamtumia ujumbe mwingine kuwa “Si hivyo tu hata vitu vya Mawaziri wako na Wasaidizi wako wote na kila kitu kizuri, nitakujakuchukua.”

 

Hapo Mfalme wa Taifa la Watendao kwa Haki akashituka kwa kuita Baraza lake la Mawaziri kuwaeleza alivyoambiwa na Mfalme wa Shamu.  Baraza lake la Mawaziri wakasema “hata lile la kwanza ulilokuwa umekubaliana nalo lifute– USIKUBALI.”

 

Mfalme wa Taifa la Watendao kwa Haki akatuma ujumbe kwa Mfalme wa Shamu kuwa ameghairi yale yote. Yule Mfalme wa Shamu alituma ujumbe wa viapo vikali vya miungu yake kwa kuwa alijua, Mfalme wa Taifa la Watendao kwa Haki yuko peke yake, wakati yeye anaungwa mkono na Wafalme wengine 32!

 

Mfalme wa Taifa la Watendao kwa Haki alipopata nguvu, alijibu katika mstari wa 11 kuwa “mwambieni Mfalme wa Shamu kwamba avaaye asijisifu kama avuaye.”  Moyo wa Mfalme wa Taifa la Watendao kwa Haki ukawa umeinuliwa juu ili ushindi upatikane kwa ajili ya taifa zima.

 

Baada ya Moyo wa Mfalme wa Taifa la Watendao kwa Haki kwenda juu, Nabii aliinuka na kumweleza Mfalme anayepigwa vita kuwa “usiogope Aliyekuumba anawatia mkononi mwako hawa Mataifa yote 33.” Mfalme wa Taifa la Watendao kwa Haki aliuliza kuwa, “Kwa jinsi ipi?” nani atapigana na Mataifa haya yenye nguvu?  Nani atapanga vita?

 

Nabii alimjibu kuwa “tena usitumie majemadari wakubwa, bali wale vijana wadogo wa kule wilayani na vita utapanga wewe mwenyewe.”

 

Nguvu ilikuwa ni kubwa kwa Mfalme wa Taifa la watendao kwa Haki kwa kuwa Moyo wake yule Mfalme, uliinuliwa.   Matokeo ni kwamba Majeshi ya Mataifa 33 yote yaliangamziwa na vijana wadogo wa Wilayani na Mfalme wa Shamu na wenzake 32 wakashindwa.  Waliishia kumwangukia yule Mfalme wa Taifa la Watendao kwa Haki ambaye mwanzoni walikuwa wamemdharau–Amani, utulivu, furaha maisha vikaendelea tena katika Taifa la watendao kwa haki.

 

UFAFANUZI

Katika Taharuki na Hofu ambayo imeletwa na dunia, Ushindi uko katika kuendesha Ibada ya Kuliinua Taifa zima na Rais wake ili tusiwe na Hofu, huku tukijua Aliyetuumba na kutuvusha wakati wote, hawezi kutuacha kamwe.

 

Kwa ufupi, lazima tumwinue Rais na Wasaidizi wake wote kisha Wananchi ili mlango wa Hofu ufungwe Umilele Wote.  TUMEPONA SOTE TUSHANGILIE Aliyetuumba anaonekana kwa Sura ya Taifa la Tanzania.

Imekwishakuwa (Ufunuo 21:6)

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages