Rais Dk. John Magufuli akizindua Soko Kuu la Kisasa la Manispaa ya Morogoro, leo na kulipa jina la Chifu Kingalu wa mkoa huo. Wanaomsaidia kuzindua ni Mkuu wa mkoa huo Loata Ole Sanare na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo.👆Rais Dk. John Magufuli akisikiliza kero mbalimbali za wafanyabiashara katika Soko Kuu la Kisasa la Manispaa ya Morogoro, lbaada ya kuzindua rasmi soko hilo na kulipa jina la Chifu Kingalu wa mkoa huo.👇
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 11 Februari, 2021 amezindua Soko Kuu la Manispaa ya Morogoro na kuagiza soko hili liitwe Soko Kuu la Chifu Kingalu ikiwa ni kutambua mchango wa kiongozi huyo wa kimila (Kabila la Waruguru) katika masuala mbalimbali ikiwemo utunzaji wa mazingira.
Soko hilo lenye ukubwa wa meta za mraba 9,897, vibanda vya biashara 304, vizimba 900, eneo la kuegesha magari 200 na lenye uwezo wa kuchukua wafanyabiashara 2,500 limejengwa katikati ya Manispaa ya Morogoro baada ya kuvunja soko la awali lililojengwa mwaka 1953 ambalo lilikuwa dogo na chakavu.
Ujenzi wa soko hilo umekamilika kwa asilimia 100 kwa gharama ya shilingi Bilioni 17.656 na ni miongoni mwa masoko 22 hapa nchini yaliyojengwa katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano kwa gharama ya shilingi Bilioni 361.033.
Baada ya kulizindua, Mhe. Rais Magufuli amewatembelea wafanyabiashara ndogondogo wanauza bidhaa mbalimbali ndani ya soko na kusiliza kero zao ambapo wamelalamikia kutozwa ushuru mara 2 na kwa kiwango kikubwa, na wengine kupangishwa vizimba/vibanda vya biashara na watu binafsi wakiwemo wafanyakazi wa Manispaa ya Morogoro ambao wanawatoza gharama kubwa ikilinganishwa na gharama halisi iliyowekwa na Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Rais Magufuli ameeleza kutofurahishwa kwake na vitendo hivyo, ameipiga marufuku Manispaa ya Morogoro kukusanya ushuru kwa mazao yasiyozidi tani moja kwa mujibu wa sheria, ameagiza wafanyakazi wa Manispaa ya Morogoro waliowapangisha vizimba/vibanda wafanyabiashara wadogo kwa kuwafanyia udalali wa kuwatoza fedha nyingi ikilinganishwa na kiwango kilichowekwa na Manispaa kurejesha fedha za juu zote kwa wahusika na kwamba kuanzia sasa wafanyabiashara waliopo kwenye vizimba/vibanda hivyo ndio watambauliwe kuwa wamiliki halali na walipe moja kwa moja Manispaa.
Amewaonya viongozi wa Mkoa wa Morogoro na taasisi zote zilizopaswa kuchukua hatua dhidi ya vitendo hivyo na amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo.
Mhe. Rais Magufuli amewataka Madiwani wa Manispaa ya Morogoro na halmashauri zingine nchini kuacha mara moja kutunga Sheria ndogo zinazokinzana na Sheria mama zinazotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ambavyo Manispaa ya Morogoro imetunga Sheria ndogo ya kukusanya ushuru wa mazao ya wakulima yanayoingia sokoni hapo hata kama ni kifurushi cha chini ya gunia moja ilihali Sheria ya Bunge inaagiza mazao yasiyozidi tani 1 yasitozwe ushuru.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameitaka Manispaa ya Morogoro kutozizuia Bodaboda na Bajaji kuingia katika Soko Kuu la Chifu Kingalu kwa kuwa vyombo hivyo ndivyo vinatumika kuwaleta wananchi na bidhaa katika soko hilo na pia soko limetengewa eneo la pikipiki na Bajaji.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Morogoro kwa kuongoza kitaifa katika kujitokeza kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020 ambapo asilimia 77.4 ya waliojiandikisha walipiga kura, na amewashukuru wananchi wa Mkoa huo kwa kuongoza kumpigia kura nyingi ambapo asilimia 92.3 ya waliojiandikisha walimchagua yeye wakiongozwa na Manispaa ya Morogoro iliyompa kura za Urais kwa asilimia 99.6.
Amewahakikishia kuwa atasimamia kwa nguvu zote utekelezaji wa ahadi alizozitoa na Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM (2020/25) na pia amepokea maombi ya Wabunge Mhe. Aziz Abood (Mbunge wa Morogoro Mjini) na Mhe. Innocent Kalogeris (Mbunge Morogoro Kusini) juu ya kuimarishwa kwa huduma ya maji katika Manispaa ya Morogoro, ujenzi wa barabara ya lami ya Kisaki – Bigwa na barabara ya Malinyi.
Mhe. Rais Magufuli kesho ataendelea na ziara yake hapa Morogoro ambapo atafungua kiwanda cha kusafisha na kufungasha mazao jamii ya kunde (Mahashrii Agro Processing Industry of Tanzania) katika eneo la Mikese, atafungua kiwanda cha kukoboa mpunga (Murzar Wilmar Rice Mills) katika eneo la Kihonda na atafungua kiwanda cha ngosi (Ace Lether Tanzania Limited) katika eneo la Kihonda.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇