Mwanasiasa nguli wa siku nyingi Dk. Muhammed Seif Khatib amefariki Dunia, leo asubuhi katika Hospitali ya Arhama Unguja mjini Zanzibar. Emmanuel Mohamed mtoto wa Khatib, amethibitisha.
Amesema, msiba upo nyumbani kwa marehemu eneo la Magomeni Zanzibar na mazishi yanatarajiwa kufanyika kesho saa nne asubuhi.
Wakati wa uhai wake Khatibu aliyezaliwa Januari 10, 1951, amewahi kuhudumu katika nafasi mbalimbali katika Chama Cha Mapinduzi na Serikalini, ikiwemo kuwa Mbunge wa Jimbo la Uzini Zanzibar kwa tiketi ya CCM mwaka 1995 na pia amewahi kuwa Waziri katika wizara mbalimbali.
Khatibu atakumbukwa kwa kuwa miongoni mwa waasisi wa kwanza wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) ambapo kati ya mwaka 1978 hadi 1983 alikuwa Mwenyekiti wa UVCCM na kati ya mwaka 1978 na 2002 Khatibu alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Pia amewahi kuwa Katibu wa NEC, Oganaizesheni Makao Makuu ya CCM.
Kabla ya kuwa mjumbe wa NEC alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Habari, na baadaye January 4, 2006 aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo na February 12, 2008 akateuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano.
Msimamizi Mkuu wa Blog ya Taifa ya CCM, Bashir Nkoromo na Waendeshaji wote wa Blog hii tunatoa pole za dhati kwa Ndugu, Jamaa, Marafiki na wote walioguswa kwa namna moja au nyingine na msiba huu.
Ina Lilah Waina Ilayh Rajiuun.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇