Donald Trump at rally in front of White House

Hivi ndivyo urais wa Trump unavyokamilika kwa kishindo kibaya.

Kwa wiki kadhaa, Donald Trump amekuwa akitaja Januari 6 kama siku ya masiku. Ilikuwa siku ambayo aliwaambia wafuasi wake kwenda Washington DC, na kushinikiza Congress - na Makamu wa Rais Mike Pence - kutupilia mbali matokeo ya uchaguzi mkuu wa Novemba na kuacha urais usalie mikononi mwake.

Jumatano asubuhi, rais na wafuasi wake wakaanza kutimiza azma yao.

Wakili wa Bw. Trump Rudy Giuliani, alisema mzozo wa uchaguzi utasuluhishwa kupitia "mapigano".

Donald Trump Jr, mwana mkubwa wa rais Trump alikuwa na ujumbe kwa wafuasi wa chama chake ambao "hawatampigania" rais wao.

"Chama cha Republican sio chao tena," alisema. "Hiki ni chama cha Republican cha Donald Trump."

Halafu rais mwenyewe akazidi kuhamasisha vurugu kwa kundi la watu ambalo lilizidi kuongezeka na kuimba kwa nguvu "komesheni wizi" na "upuuzi" huku rais akiwashawishi kuandamana kutoka ikulu ya White House hadi bungeni Katika jengo la Capitol Hill.

"Hatutarudi nyuma. Hatutakubali," rais alisema. "Nchi yetu haitakubali tena. Hatuwezi kuvumilia tena."

Section divider

Rais alipokuwa anakamailisha kauli yake, sarakasi nyingine ilikuwa inaendelea ndani ya bunge, wakati wa kikao cha pamoja cha kujumuisha matokeo ya kura ya wajumbe kutoka majimbo yote.

Kwanza, makamu wa rais Pence - alikataa takwa la rais la kutupilia mbali matokeo kutoka katika majimbo yanayoshindaniwa akisema hana nguvu hiyo.

Protesters outside the Capitol

Kiongozi wa wengi katika bunge la Seneti Mitch McConnell kutoka chama cha Republican , aliyekuwa amevalia suti nyeusi sawa na ya kwenda mazishini, alikuwa anamzika Donald Trump, sio kumsifu.

"Ikiwa huu uchaguzi ungelifutwa kutokana na maneno ya upande ulioshindwa, demokrasia yetu ingelikuwa imeingia katika mtego wa kifo," McConnell alisema. " Tusingeliona tena nchi nzima ikikubali matokeo ya uchaguzi. Kila baada ya miaka minne tungelishuhudia jinsi watu waking'ang'ania madaraka kwa gharama yoyote."

Seneta huyo wa Kentucky, ambaye atakuwa kiongozi wa wachache baada ya chama chake kushindwa hivi karibuni huko Georgia, alisema bunge lilibuniwa " kukomesha matamanio ya muda mfupi ambayo yanaweza kuhujumu msingi wa nchi yetu".

Wakati matamshi yakiwa yanagonga vichwa vya wenzake nje ya bunge hali ilikuwa imebadilika baada ya wafuasi wa Trump ambao huenda walikuwa wamehamasika na hotuba za awali, kuamua kuvamia bunge.

Waandamanaji walipambana na maafisa wachache wa usalama waliokuwa langoni na kufanikiwa kuingia ndani ya bunge. Vikao vilisitishwa ghafla huku wabunge, wafanyakazi wa bunge na wanahabari wakilazimika kujificha kwa kuhofia usalama wao.

Maafisa wa usalama wakijihami kwaa bunduki dhidi ya waandamanaji ndani ya bunge la seneti
Maelezo ya picha,

Maafisa wa usalama wakijihami kwaa bunduki dhidi ya waandamanaji ndani ya bunge la seneti

Sarakasi iliendelea kushuhudiwa bungeni huku vituo vya Televisheni vikionesha picha za waandamanaji wakicheza densi nje ya bunge huku wakipeperusha bendera.

Picha za waandamanaji waliokuwa ndani ya bunge zilianza kusambazwa katika mitandao ya kijamii, baadhi yao wakijaribu kuvunja madirisha na kuingia katika ofisi za wabunge; huku maafisa wa usalama wakionekana wakiwaelekezea bunduki ndani ya bunge la wandamanaji nyuma ya milango iliokuwa imefungwa.

Section divider

Huko Wilmington, Delaware, Rais Mteule Joe Biden aliahirisha hotuba yake kuhusu masuala ya uchumi iliokuwa imepangwa na kulaani kile alichokiita "uasi" mjini Washington.

"Wakati huu demokrasia yetu iko chini ya shambulio lisilokuwa la kawaida ambalo hatujawahi kuliona katika historia yetu ya hivi karibuni , "alisema." Shambulio dhidi ya ngome ya uhuru, Bunge lenyewe. "

Alikamilisha hotuba yake fupi kwa kumtaka Trump kujitokeza katika televisheni ya kitaifa kulaani ghasia hizo: ''agiza kukomeshwa kwa vurugu hizi".

Dakika chache baadaye, Trump alitoa ujumbe wake kwa taifa - lakini sio kama Biden alivyopendekeza .

Badala yake, alijumuisha malalamiko yake kuhusu madai ya kura "kuibwa",aliwaambia wafuasi wake "nendeni nyumbani, tunawapenda, ninyi ni watu maalum sana".

President-elect Joe Biden speaks amid protests in Washington

Alisema nao kwa upole jinsi ambavyo rais amekuwa akijibu ukosoaji dhidi ya wafuasi wake.

Trump aliweka ujumbe kwenye Twitter mara mbili akiwasifu wafuasi wake, japo baadaye uliondolewa na Twitter, ilipoamua kuchukua hatua isiyokuwa ya kawaida na kufungia kwa muda akaunti ya rais kwa saa 12.

Facebook pia ilifuata mkondo na kumpiga marufuku Trump kwa siku nzima.

Kwa mara ya kwanza katika urais wake na kwa mara ya kwanza katika uhusiano wake wa karibu na mitandao ya kijamii Donald Trump alikuwa amenyamazishwa.

Baada ya taharuki ya mchana hadi jioni maafisa wa polisi hatimaye walifanikiwa kudhibiti hali ya usalama katika jengo la Capitol Hill, huku kauli za kulaani vurugu hizo zikitolewa kutoka pembe mbalimbali duniani.

Wanasiasa wa chama cha Democratic, kama vile kiongozi mtarajiwa wa wengi katika Seneti Chuck Schumer, alielekeza lawama kwa rais.

"Januari 6 itakumbukwa kwa masikitiko makubwa katika historia ya Marekani," alisema. " hili ni onyo la mwisho kwa nchi yetu kwa kukubali kuwa na rais wa aina hii, watu walivyomwezesha na vyombo vya habari vinavyoangazia madai yake ya uongo na watu wanaomuunga mkono katika jaribio la kuiweka Marekani mashakani."

Wanasiasa wa Republican pia walifuata mkondo na kulaani kitendo hicho.

"Tumevamiwa bungeni muda mfupi uliopita katika jaribio la kutuzuia kutekeleza majukumu yetu ya kikatiba," aliandika kwenye Twitter mbunge Lynne Cheney, mkosoaji wa mara kwa mara wa rais.

"Bila Shaka rais alikiunda kikundi hiki, rais alichochea kundi hili, rais alihutubia kundi hili."

Rais pia alikosolewa na washirika wake wa karibu kama vile Seneta Tom Cotton wa Arkansas, ambaye alisema: "Wakati umewadia kwa rais kukubali matokeo ya uchaguzi, akome kuwapotosha Wamarekani na kuzua vurugu," alisema.

Mkuu wa utumishi wa mke wa rais, Melania Trump, Stephanie Grisham na naibu msemaji wa Ikulu ya White House Sarah Matthews walijiuzulu kupinga vurugu hizo huku ripoti zikiashiria kuwa maafisa zaidi wanatarajiwa kujiuzulu ndani ya saa 24.

CBS imeripoti kwamba mawaziri katika utawala wa Trump wanajadili kifungu cha 25 cha marekebisho ya katiba ya Marekani, ambacho kinaelezea jinsi makamu wa rais na mawaziri wanavyoweza kumuondoa rais madarakani kwa muda.

Ikiwa Pence na mawaziri wataamua kuchukua hatua hiyo au la, urais wa Trump hatahivyo utafikia tamati ndani ya wiki mbili zijazo.

Baada ya hapo viongozi wa chama cha Republican watasalia na machungu ya kupoteza udhibiti wa Congress, seneti na White House na kuwa na rais wa zamani ambaye aliharibu sifa ya chama chao.

Section divider