***************************************************
Na Woinde Shizza ARUSHA
Kamishna mkuu wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) Dkt Edwin Mhede amesema kuwa mamlaka hiyo haiongezi muda wa wafanyabiasha kuboresha mashine za EFD badala yake itachukua hatua za kisheria kwa ambao bado hawajaboresha.
Dkt Mhede aliyasema hayo wakati akifungua mkutano mkuu wa nusu mwaka wa mamlaka hiyo ambapo alipokea dodoso la kuombwa kuongezwa muda wa wafanyabiasha kuboresha mashine za EFD .
Alisema kuwa jambo la kuongeza muda haliwezekani kwani zoezi hilo linaweza kufanyika kwa muda mfupi na walipewa muda wa kutosha kuanzia Desemba 7, 2020 hadi Januari 7,2021.
Alieleza kuwa ombi hilo amelikataa na wafanyabiashara wote ambao bado wachukuliwe hatua kwani wakianza kutengeneza mazingira ya kuongeza muda watakuwa wanacheza na hawatafikia lengo la uboreshaji huo.
“Suala la EFD mashine zenye protocol 2.1 sio chagua la mfanyabiashara bali ni lazima kila mfanyabiashara awe amefanya maboresho haya maboresho ni lazima yaendane na aina ya mashine tunazozitumia hivi sasa na upatikanaji wake ni wa dakika chache kwahiyo nasema kuongeza muda ni jambo ambalo haliwezekani inajulikana wazi kuwa utiifu wakati mwingine lazima watu walazimishwe,” Alisema Dkt Mhede.
Alifafanua kuwa kama upatikanaji EFD hauzidi masaa mawili au matatu na waliwapa mwezi mzima ni kwanini waongeze muda, ambapo aliagiza baada ya kutoka katika mkutano huo wakachukue hatua kwani hawatakuwa na namna nyingine zaidi ya kwenda kuwapa motisha watii kwa mujibu wa sheria lakini suala la kuongeza muda hicho kitu hakitakuwepo.
Naye naibu kamishina wa mamlaka ya mapato Tanzania ,(TRA) Msafiri Mbibo alisema kuwa mkutano huu utasaidia kuweza kujua namna ya kutatua matatizo yaliopo katika sekta yao ,pamoja na kupanua mikakati itakayo saidia kupata mapato mengi yatakayo wezesha kufikia malengo waliojiwekea.
Alibainisha kuwa kazi ya taasisi hii ni kuweza kusaidia serikali kujenga taifa linalojiweza kiuchumi pamoja na kimaendeleo.
Aliongeza kuwa mkutano huu utasaidia kuwawezesha kujadili njia bora itakayosababisha utendaji kazi kuwa mzuri ,ambapo pia watajadili namna ya kutatua matatizo waliyonayo ikiwemo upungufu wa idadi ya Wataalam wa mamlaka hiyo , upungufu wa vitendea kazi pamoja na ukosefu wa nyumba za Wataalam wanaoishi maeneo ya mipakani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇