TANZANIA imetupwa nje ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) baada ya sare ya 2-2 na Guinea usiku wa Jumatano katika mchezo wa mwisho wa Kundi D Uwanja wa Reunification Jijini Douala nchini Cameroon.
Mabao ya Tanzania yamefungwa na kiungo wa Mtibwa Sugar, Baraka Majogoro dakika ya 23 na beki wa Namungo FC, Edward Charles Manyama dakika ya 67, wakati ya Guinea yamefungwa na Barry Yacouba kwa penalti dakika ya tano baada ya mlinzi Carlos Protas kuunawa mpira na la pili Victor Kantabadouno dakika ya 82.
Taifa Stars iliyo chini ya kocha Mrundi, Etienne Ndayiragije inamaliza na pointi nne nyuma ya Guinea na Zambia zilizofungana kwa pointi tano kila moja.
Baada ya sare ya 0-0 na Zambia katika mchezo wa mwisho Jumatano Uwanja wa Limbe, Namibia inamaliza na pointi moja na kuungana na Tanzania kurejea nyumbani.
Sasa Zambia itamenyana na mabingwa watetezi, Morocco na Guinea na Rwanda Jumapili, wakati Robo Fainali nyingine ni Jumamosi Mali na Kongo na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) dhidi ya Cameroon.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇