LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 21, 2021

KANISA HALISI KUFANYA IBADA MAALUM YA KUFUNGUA BIASHARA YA UTALII UKANDA WA KASKAZINI, ARUSHA

Na CCM Blog, Dar es Salaam

Sekta ya Maliasili na Utalii hapa Nchini Tanzania ni miongoni mwa sekta zinazochangia kwa sehemu kubwa ya pato la Taifa  na  kuendeleza maisha ya Wananchi wengi kwa njia mbalimbali ikiwepo fursa za kutoa ajira. Kwa mfano Sekta Ndogo ya Utalii kupitia vivutio mbalimbali inachangia zaidi ya asilimia 17 ya pato la Taifa na asilimia 25 ya fedha zote za Kigeni huku ikikadiriwa kuajiri zaidi ya watu milioni 5.5 kwa mwaka.


Katika Hotuba ya Bajeti ya 2020-2021 ya Waziri Mwenye dhamana ya Maliasili na Utalii aliyoitoa Bungeni jijini Dodoma ni kwamba Mapato yatokanayo na utalii wa Kimataifa yaliongezeka kutoka Dola za Marekani Bilioni 2.4 mwaka 2018 hadi Dola za Marekani Bilioni 2.6 mwaka 2019. Aidha, wastani wa siku za Watalii kukaa nchini ziliongezeka kutoka siku 10 mwaka 2018 hadi siku 13 kwa mwaka 2019.

 

Vilevile, matumizi ya watalii kwa siku yaliongezeka kutoka Dola za Marekani 193 mwaka 2018 hadi Dola za Marekani 266 mwaka 2019 na kwamba mafanikio hayo yalitokana, pamoja na mambo mengine jitihada za kuendeleza na kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi.


Waziri alisema, Serikali imeongeza idadi ya Hifadhi za Taifa kutoka 16 hadi 22 na misitu ya hifadhi ya mazingira asilia kutoka 17 hadi 19. Ongezeko la Hifadhi za Taifa limetokana na kupandisha hadhi mapori ya akiba ya Burigi, Biharamulo, Kimisi; Ibanda; na Rumanyika - Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa za Burigi - Chato, Ibanda - Kyerwa na Rumanyika - Karagwe; sehemu ya Pori la Akiba Selous kuwa Hifadhi ya Taifa Nyerere; sehemu ya Pori la Akiba Ugalla kuwa Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla na Pori la Akiba 


Sasa ni wazi kwamba ili Taifa liendelee kunufaika na Sekta ya Utalii bila Shaka pamoja na mambo mengine ni lazima  Juhudi za Serikali ziungwa mkono na kila Mtanzania kwa njia mbalimbali ikiwemo kushiriki kuvitunza na kuvilinda vivutio vya Utalii na pia kushiriki kuhamasisha ukuaji wa Utalii ndani na nje ya Tanzaniai kwa njia mbalimbali.


Uhamasishaji huu unawahusu mtu mmojammoja, Kampuni na Taasisi mbalimbali zikiwemo za Serikali na za Watu binafsi na pia Taasisi za kijamii zikiwemo za kidini.


Na kwa kuwa Rais Dk. John Magufuli amekuwa wakati wote  akiwafundisha Watanzania kumtanguliza Mungu kwa kila jambo, hivyo kulinda na kuvitunza vivutio vya Utalii nchini na kuhamasisha utalii ndani na nje ya Tanzania tu bila pia kumuomba Mungu hasa katika kuombea Utalii uzidi kukua haliwezi kufikia hatua inayohitajika.


Kanisa Halisi la Mungu Baba lililopo Tegeta jijini Dar es Salalaam, lenyewe kwa maono yake, limeamua kushiriki katika kufungua Biashara ya Utalii izidi kushamiri Ukanda wa Kaskazini ili Tanzania na Watanzania kwa jumla wanufaike katika sekta hiyo ya Maliasili na Utalii.


Taarifa iliyotolewa na Kiongozi was Kanisa hilo Baba wa Uzao (jina la Kikanisa), imesema, Kanisa hilo limeandaa Ibada Maalum ya Kufungua Biashara ya Utalii Ukanda wa Kaskazini, ambayo itafanyika tarehe 24, mwezi huu, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.


 Tafadhali Soma Taaraifa Kamili Hapo👇



Lango la 25-26 Ethanimu, Vol.1 (2-3 Januari 2021) nilienda Arusha kuachilia Mito ya Utajiri kutokea kwenye BUSTANI MPYA YA MUNGU BABA, ili mito hiyo iende kwenye Moyo wa kila mmoja Aliyekusudiwa.  Nilikusudia kuhudumia Uzao wa MUNGU BABA peke yake, badala yake nikapokelewa na wanachi wote wa Mkoa wa Arusha kupitia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mkuu wa Wilaya ya Monduli na Mkuu Wilaya ya Arumeru.


Tangu niache kazi ya Umma na kuhamia Utajirishoni (Madhabahuni), ilikuwa ni mara ya Kwanza kustareheshwa Hotelini, hivyo ina maana Uhalisia wote ulinipokea.  Maana pale Hotelini watu wa kila aina wanakuwepo: weupe, weusi na wekundu pia.    Namtukuza MUNGU BABA, kwa Uhalisia wake wa Moyo (Mithali 4:13), kwa sababu ya Uumbaji na Uhalisia wote kunipokea.


Katika 2Wafalme 4:8-17 tunajifunza kitu kinachofanana na mapokezi hayo niliyotaja hapo juu.

Elisha akiwa katika kuhubiri lango (siku) moja alienda Shunami akamkuta mama mmoja aliyekuwa na Cheo.  Mama yule alipomwona Elisha anapita mara kwa mara, akaamua kumtengenezea Chumba Maalum Gorofani chenye kitanda, taa na meza ya kufanyia Maandalizi ya Ibada.  Jambo hili lilitengeneza deni ndani ya Moyo wa Elisha, ndipo akamtuma Geazi (aliyekuwa Msaidizi wake) kwenda kuuliza kuwa yule mama mwenye Cheo aliyewapokea anashida gani ili kupitia upendo ule aliouonyesha kwa Elisha, hoja ijengwe kwa MUNGU BABA tatizo hilo litatuliwe.  Geazi alielezwa kuwa yule mama hana mtoto na mume wake ni mzee sana.  Elisha aliagiza yule mama aitwe kuelezwa kuwa baada ya Miezi Tisa (9), kuanzia kipindi kile, atakuwa na mtoto.  Yule mama ndani ya Moyo wake alikuwa ameshakata tamaa na kuona hawezi tena kupata mtoto, akamweleza Elisha kuwa asimueleze uongo. Elisha hakutaka kubishana naye, aliendelea mbele kwa kutumia Mamlaka ya MUNGU BABA iliyokuwa ndani yake na kumtamkia kuwa “mwakani majira kama hii utakuwa na mtoto.”  Ndivyo ilivyotokea.  Baada ya Miezi Tisa, kweli yule mama alikuwa na mtoto.

Kilichosababisha yule mtoto azaliwe ni ule upendo ndani ya yule mama kwa Elisha.  Aidha, aliyependwa siyo Elisha, bali ni MUNGU BABA ndani ya Elisha ndiye aliyependwa. Kwa kuwa mwenye uweza wote ndiye aliyependwa, alilipa lile deni la upendo.  Pia yule mama wakati anamhudumia Elisha alifanya hivyo kwa dhati kabisa kutoka ndani ya Moyo wake.  Ndiyo maana Elisha alipopeleka hoja mbele za MUNGU BABA, ilijibiwa saa hiyo hiyo.


Nilitangulia kukueleza kuwa Wananchi wote wa Arusha walinipokea kwa upendo mkubwa kupitiliza lango la 25-26 Ethanimu, Vol.1 (2-3 Januari, 2021) kupitia Mkuu wa Mkoa na kunifahamisha kuwa Biashara ya Utalii imeanguka kabisa. Mkuu wa Mkoa alieleza kama Sulemani katika 1Falme 3:11; yaani si kwa nafsi yake. Kama vile ilivyotokea kwa Sulemani kupata hata yale ambayo hajaomba, basi imetokea hivyo hivyo kwa upande wa Biashara ya Utalii kufunguka kwa upya jiji la Arusha. 

Kuanguka kwa Biashara ya Utalii ni kutokana na ugonjwa wa Korona ambao umedumu kwa muda wa Mwaka Mmoja sasa.  Biashara ya Utalii inagusa:

+ Kilimo;

+ Uvuvi;

+ Ufugaji;

+ Viwanda;

+    Lugha;

+    Madini;

+ Ujenzi wa Nyumba;

+ Barabara;

+ Huduma za Usafiri na Usafirishaji;

+ Huduma za Hoteli;

+ Utamaduni;

+ Utawala;

+ Amani na Utulivu;

+ Dini, Madhehebu na Huduma Binafsi;

+ Na kadhalika.


Kwa upande wa Mji wa Arusha, hakuna asiyeguswa na Biashara ya Utalii ambayo, kama nilivyoeleza awali,  imetokana na ugonjwa wa korona ulioanzia Nchi za Magharibi.


Habari Njema (Ushuhuda)

Wakati naelezwa hali hiyo ya kuanguka kwa biashara ya Utalii, nilimkumbuka Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mjini ambaye wakati wa Hija ya Pili (2019) akiwa anaifungua, alitushirikisha shida ya Mji ule ambayo ilikuwa inawatesa, pepo teleza.  Hakuweza hata kuhudhuria Ibada kwa kuwa alikuwa anawahi kuongea na Wananchi ili kujua wafanye nini kudhibiti hali hiyo iliyokuwa inasumbua ule Mji kwa muda mrefu. Tulipoinua hoja mbele za MUNGU BABA, kuwa nisingeweza kufanya chochote bila hiyo shida kuondoka kwanza, hoja ya dakika tatu ilimaliza hilo tatizo.


Aidha, wakati naelezwa tatizo hilo, nilimkumbuka Mkuu wa Mkoa wa zamani wa Tabora Agrey Mwanri kuhusu tatizo la mauaji ya watu Tabora kishirikina, tatiza ambalo wakati anatueleza lilimtoa machozi.  Tatizo hilo nalo tuligalagala chini kwa muda wa saa moja likaisha hapo hapo hadi leo. 

Baada ya kukumbuka Habari Njema (Shuhuda) hizo, nilijua hata hilo tatizo la Biashara ya Utalii linaisha kupitia ule upendo ambao  Wananchi wa Arusha walioonyesha kwangu.


Kwa nini yule mama wa Shunami, tatizo lake liliisha?  Ushuhuda wa yule mama Mshunami, ni sawa na yule Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Mjini, na Mkuu wa Mkoa wa zamani wa Tabora.


Shida  yoyote inaletwa na jeshi la pepo wabaya, wakuu wa giza, falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho (Waefeso 6:12).  Katika Kitabu, imeandikwa vizuri kuwa ni Kanisa ndilo linatakiwa kufuta hilo jeshi la pepo wabaya, wakuu wa giza, falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho (Waefeso. 3:10).


Suala la korona halina tofauti na tatizo la mauaji ya watu yaliyokuwa yanafanyika kule Tabora kishirikiana. Tatizo hilo halina tofauti pia na teleza aliyekuwa anasumbua kule Kigoma. Ni wakuu wa giza, falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho ndio wanafanya hayo ili kuendelea kuzuia kweli isitajwe au kufundishwa katika jamii.


Kinachotakiwa ni nini sasa?

Katika suala la kufungua Biashara ya Utalii Ukanda wa Kaskazini mwa Tanzania, ni lazima tuangalie soko liko wapi.  Soko la Utalii huu liko Ulaya, Amerika, Asia, (Australia na NewZealand kidogo).  Aidha, soko liko ndani ya Nchi kama tutakubali kujitambua kuwa hata sisi tuna umuhimu wa kutembelea vivutio vya utalii. Nchi za Magharibi ndizo zimeathiriwa na korona hata kama waliotengeneza virusi hivyo hawakuwa wamelenga hayo Mataifa! 

Kwa upande wa soko la ndani, hatuna korona kwa upendeleo mkubwa wa MUNGU BABA mwenyewe (Isaya 60:10). 


Kwa upande wa soko la Magharibi, inatubidi tujenge hoja mbele ya aliyeumba kila kitu bila kuangalia mipaka, bali tuangalie rasilimali ya Wanyamapori na vivutio vingine wanavyofuata hapa Tanzania.  Tanzania, kwa maelekezo ya Mhe. Rais Magufuli, tuliponywa na MUNGU BABA.  Inabidi, hata kwa suala la Soko la Utalii kule Magharibi, turudi kwa huyo huyo aliyetuponya Tanzania kumweleza haja ya Moyo, kama tulivyojiombea sisi wenyewe.


Ni kweli tumepona, ila ni lazima tule, tunywe, watoto waende shule, tulipie pango la nyumba na mengine mengi.  Ili hilo lifanikiwe ni lazima tuwafungue soko la  Mataifa ya Ulaya, Amerika, Asia, Australia, New Zealand na Mataifa ya Afrika kama vile South Afrika.


Tukiwaachia wao wenyewe, hawana huo unyenyekevu wa kumrudia MUNGU BABA.  Hivyo, tufanye sisi kwa kuwa hata sisi tuna hitaji soko lao la Utalii.  Kuwa na vivutio haitoshi bila watu kuja kuviangalia.  Hao watu wanaotakiwa kuja  kuviangalia, bado wamefungwa kwa suala la MUNGU BABA. Tuwafungue sisi.


Pili, tuanze sisi kutembelea vivutio vyetu.  Gharama ya jambo hili ni watunza vivutio kama vile TANAPA na NGORONGORO kupunguza bei. Watoa  huduma za Hoteli na usafiri pia inabidi kupunguza bei kwanza (kwa kuwa uchumi wa Mtanzania mmoja mmoja ulikuwa bado haujawa kama watu wa Magharibi).


Tupite Barabara ipi?

Watanzania tushukuru kwanza kuponywa korona bila dawa.  Katika Kumbukumbu 28:47-48, Kitabu kinasema kuwa kama umetendewa mengi, usiposhukuru, kongwa la chuma linakuwa shingoni mwako na kuwa mtumwa wa wabaya.


Kanisa Halisi la MUNGU BABA tulishukuru ni kweli, lakini wananchi hatujawahi kwenda Uwanjani tukashukuru kwa Sauti hadharani kwa kusema “MUNGU BABA tunashukuru kutuponya korona bila dawa”. Sasa tufanye hivyo, hii ndiyo majira husika.


Tuwasemehe bure wote waliotengeneza kirusi cha korona kwa nia yoyote mbaya waliyokuwa nayo (Isaya 43:25).  Kwa kuwa Watanzania wote sasa wana Moyo Mpya wa MUNGU BABA Mwenyewe, atasikia na kufuta korona ili Soko la Utalii kwa upande wa Magharibi lifunguke kwa upya.


Ukishukuru milango iliyokuwa imefungwa, inafunguka (Zaburi 100:4); ukishukuru, kilichokuwa kimekufa kinafufuka (Yohana 11:44-45); na ukishukuru, vichache vinaongeszeka (Yohana 6:11-13).


Hakuna ujanja mwingine.  Karibuni nyote twende Karume Stadium, Lango la 19 Buli, vol.1 (24 Januari,2021) kufanya Ibada hiyo ya kufungua Biashara ya Utalii Ukanda wa Kaskazini.

3 comments:

  1. Hongereni Sana kwa ibada hiyo, Asante tupo pamoja katika ibada. Mungu awasimaie. Asante Sana tupo pamoja.

    ReplyDelete
  2. Hongereni Sana kwa ibada hiyo, Asante tupo pamoja katika ibada. Mungu awasimaie. Asante Sana tupo pamoja.

    ReplyDelete
  3. Wape hongera nyingi, tunawatakia mafanikio mazuri kwenye hiyo ibada. Tupo pamoja

    ReplyDelete

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages