Askari mwingine wa Umoja wa Mataifa kutoka Burundi ameuawa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR na wengine wawili wamejeruhiwa, kitendo ambacho kimelaaniwa vikali na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, AntĂłnio Guterres.
Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ametoa taarifa jijini New York, akisema kuwa shambulio hilo linadaiwa kufanywa na kikundi kiitwacho Coalition des Patriotes pour le Changement (CPC) ambao walishambulia pia msafara wa askari wa kulinda amani wanaohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini CAR, MINUSCA kwenye eneo la Grimari jimboni Ouaka.
Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya askarii huyo na wananchi na serikali ya Burundi huku akiwatakia afueni ya haraka askari wengine wawili waliojeruhiwa.
Guterres amesisitiza kuwa mashambulizi yoyote dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa yanaweza kuwa uhalifu wa kivita huku akitoa wito kwa mamlaka nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati kutumia uwezo wake wote kusaka wahusika wa shambulio hilo ili wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria.
Katibu Mkuu wa UN amesema mashambulizi dhidi ya walinda amani hayapasi kukwepa sheria.
Amebainisha tena wasiwasi wake juu ya kuendelea njama za kuvurugua amani na utulivu kwenye maeneo mbali mbali nchini humo.
Guterres ametoa wito kwa pande kinzani kukomesha ghasia mara moja na kusaka suluhu na kumaliza tofauti zao kwa njia ya amani.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa umoja huo uko tayari kusaidia wananchi na serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati katika juhudi zao za kurejesha amani na utulivu.
Tukio hilo la kuuawa askari wa kulinda amani wa Burundi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati limekuja siku chache baada ya kuuawa kwa mlinda amani mwingine wa Umoja wa Mataifa kutoka Rwanda.../
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇