LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 30, 2020

WATU 557 WAFA, 817 WAJERUHIWA KATIKA MAJANGA MBALIMBALI 2020-ZIMAMOTO



 Msemaji wa Jeshi Zimamoto na Uokoaji Tanzania, Mkaguzi Joseph Masabeja, akizungumza na vyombo vya habari Makao Makuu ya Jeshi hilo, jijini Dodoma leo, kuhusu taarifa ya mwaka ya maokozi ya majanga mbalimbali yaliyotokea nchini na kusababisha vifo na majeruhi. PICHA NA RICHARD MWAIKENDA


Na Richard Mwaikenda, Dodoma

 WATU 557 wamepoteza maisha katika majanga mbalimbali yaliyotokea nchini kuanzia Januari hadi Desemba 2020.

 

Akitoa taarifa ya mwaka ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Tanzania, Msemaji wa Jeshi hilo, Mkaguzi Joseph Masabeja, alisema  vifo hivyo vimetokea katika maokozi ya ajali za barabara, mafuriko , kwenye migodi, mashimo ya vyoo, mito, mabwawa, baharini pamoja na maeneo mengine.

 

Mkaguzi Mwasabeja akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Jeshi hilo, jijini Dodoma leo, alisema katika maokozi hayo majeruhi yalikuwa  817 na kati ya hao wanaume ni 570 na wanawake ni 247.

 

Pia, alisema kuwa kati ya Januari na Desemba 2020, Jeshi limekabiliana na matukio ya moto 1925 ambayo yamesababisha  vifo vya watu 62, kati ya hao wanaume ni 45 na wanawake 17, pia matukio hayo yalisababisha  majeruhi 74 wanaume 52 na wanawake 22.

 

Alitaja shule zilizoungua kwa moto kuwa ni 44 ambazo zimesabisha vifo vya baadhi ya wanafunzi, kuharibu miundombinu na kuteketea kwa vifaa vingi.

 

"Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limebaini majanga mengi ya moto yanatokana na uzembe, hujuma na hitilafu za umeme. hata hivyo kwa upande wa shule za bweni  tumebaini wanafunzi wanachaji simu kwa kificho kwa kutumia nyaya za umeme zilizopita darini, kutumia heater, kutumia pasi bila kuwa waangalifu, mishumaa wakati umeme ukikatika, na kutumia taa zinazotumia mafuta sehemu ambazo umeme hakuna," alisema Mwasabeja.

 

Aidha, ili kupunguza  majanga ya moto shuleni, alisema jeshi limeingia makubaliano na  Chama Cha Skauti Tanzania, kutoa elimu kwa wanafunzi baada ya wao kupatiwa mafunzo ya utoaji  elimu ya kinga na tahadhari ya majanga ya moto na kwamba Skauti watakuwa sehemu ya wazimamoto wa kujitolea.

 

Pia, Jeshi limeanzisha  klabu 786 rafiki za zimamoto katika shule za msingi na sekondari zenye jumla ya wanachama 34,018.

 

Ili kukabiliana na uhaba wa magari ya zimamoto, jeshi hilo limeingia makubaliano na Shirika la Nyumbu, kuyafanyia matengenezo magari  yaliyoharibika na kununua mapya kwa awamu.

 

Pia, jeshi hilo  litaongeza utoaji elimu kwa umma kwa kutumia vyombo vya habari ikiwemo kufanya vipindi vingi vya kuelimisha ili kuyafikia maeneo mengi zaidi.

 

Vilevile, Jeshi limejidhatiti kufanya ukaguzi wa kinga na tahadhari ya majanga ya moto kwenye maeneo yote ya mikusanyiko ya watu zikiwemo shule zote za bweni na za kutwa ambazo hivi karibuni zimeshambuliwa na majanga ya moto.

 

 

 


No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages