Alhamisi, 24 Disemba, 2020 Dar es Salaam, Tanzania.
Washindi wa kwanza wa Tuzo za Kidigitali (Tanzania Digital Awards) mwaka 2020 wametangazwa rasmi baada ya watanzania kupiga kura.
Jumla ya wawania tuzo 50 wameibuka washindi katika jumla ya vipengele 50 kutoka katika makundi tisa ikiwemo kundi la Serikali Mtandaoni, Maendeleo na Diplomasia Mtandaoni, Masoko Mtandao, Burudani Mtandaoni, Vyombo vya Habari Mtandaoni, Uvumbuzi wa Kidijitali, Mawasiliano ya Kidijitali, Uchechemuzi Mtandaoni na Tuzo ya Ujumla ya Chaguo la Watu.
Tuzo hizi zilizinduliwa nchini kwa mara ya kwanza mnamo Januari 16, 2020 kwa lengo la kutambua juhudi za watu binafsi, mashirika, kampuni na hata Serikali katika kutumia teknolojia ya kidigitali kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Baadhi ya walioshinda vipengele vingi ni pamoja na Diamond Platnumz ambaye ameshinda vipengele vitatu ikiwemo kipengele cha Tuzo ya Ujumla, Msanii bora wa mwaka na mraghibishi wa mwaka. Millard Ayo pia ametwaa tuzo tatu, tuzo ya kiongozi bora wa vyombo vya habari vya mtandaoni, TV bora ya Mtandaoni na Blog bora ya Mtandaoni.
Taasisi zilizonyakua tuzo nyingi ni pamoja na Ubongo Kids na Idara ya Uhamiaji –kila mmoja tuzo mbili. Ubongo Kids wametwaa tuzo tuzo ya ukurasa bora wa elimu mtandaoni na tuzo ya aplikesheni bora ya elimu mtandaoni. Idara ya Uhamiaji wametwaa tuzo ya uvumbuzi bora kupitia huduma yao ya kutoa hati ya kusafiria kielektroniki. Uhamiaji pia wameshinda tuzo ya taasisi bora ya Serikali mtandaoni.
Vodacom Tanzania imeibuka na tuzo mbili baada ya aplikesheni yake ya M-PESA kuzawadiwa kama Aplikesheni Bora ya Huduma za Kifedha. Tuzo nyingine iliyoenda kwa Vodacom ni tuzo ya Kampeni Bora ya Masoko Mtandaoni ambapo Vodacom wameshinda kupitia kampeni yake ya ‘Yajayo Yanafurahisha’.
Tuzo ya heshima imekwenda kwa Muhidin Issa Michuzi ambaye ametambuliwa kama kiongozi bora wa vyombo vya habari mtandaoni kwa kuanzisha na kuendeleza vyombo vya habari kwa njia ya mtandao nchini Tanzania.
Baada ya kutangaza orodha ya washindi, Mkuu wa Programu, Utafiti na Uvumbuzi wa Serengeti Bytes, Ndugu Genos Martin amesema kwa kiasi kikubwa tuzo hizi ziliathiriwa na mlipuko wa Covid-19 uliojitokeza mara baada ya kuzinduliwa kwa tuzo hizo. Hata hivyo, Martin anakiri kwamba Covid-19 kwa kiasi fulani imesaidia kuweka msisitizo wa namna ambavyo teknolojia za kidijitali haziepukiki katika maisha ya sasa na hivyo kufanya tuzo za Tanzania Digital Awards kuwa na maana zaidi.
‘’Mara baada ya kutangaza tuzo hizi kwa mara ya kwanza mwezi Januari tulipata mwitikio mkubwa sana wa watu na makampuni na hata taasisi za serikali na wadau wengine kujitokeza kushiriki. Kuingia kwa mlipuko wa Covid-19 nchini kumeathiri kwa kiasi kikubwa maandalizi ya tuzo hizi. Hata hivyo, Corona haijaharibu pekee bali kwa upande mwingine imeonesha wadau na hata sisi waandaaji kwamba matumzizi ya teknolojia za kidigitali ndio mtindo mpya wa maisha hivyo tuzo hizi zimekuja wakati sahihi na kila mmoja anapaswa kuziunga mkono”. – amesema Martin.
Akizungumzia kuhusu washindi, Martin amesema washindi wote wa tuzo za Tanzania Digital Awards wamestahili kushinda hasa kwa kutazama mambo makubwa wanayoyafanya kupitia majukwaa ya kidigitali. Martin amefafanua kwamba mwakani tuzo hizo zitatanuliwa zaidi kuhakikisha watu wengi zaidi wanashiriki na kila sekta inaguswa kwa lengo la kuchochea ubunifu na uvumbuzi katika kukuza maendeleo ya teknolojia za digitali nchini Tanzania.
“Tunawapongeza washindi wote kwa kupigiwa kura nyingi katika vipangele walivyowania, washindi wote wamestahili ushindi kwa kutazama juhudi zao katika majukwaa ya kidigitali. Tunaamini ushindi wao utachochea ubunifu na uvumbuzi katika kutatua changamoto mbalimbali katika jamii na taifa kwa ujumla. Katika tuzo zijazo tutahakikisha wadau wengi zaidi wa teknolojia za kidigitali kutoka katika sekta zote wanapata taarifa na kushiriki kikamilifu”,amesema Martin.
Tuzo za Tanzania Digital Awards zilizunduliwa rasmi Januari 16, 2020 kwa lengo la kuwatambua watu, taasisi na kampuni zinazotumia teknolojia za kiditali kuleta mabadiliko chanya katika jamii. Tanzania Digital Awards zinalenga kuchagiza Uwajibikaji, Ubunifu na Uvumbuzi kwenye majukwaa ya Dijitali. Zikiwa katika Makundi tisa na zaidi ya vipengele vidogo 50, tuzo hizi ni za kwanza na kubwa zaidi kutambua juhudi zinazofanyika ili kuleta mapinduzi ya kidijitali Tanzania na nje ya mipaka.
Katika msimu wa kwanza, yalifanyika mapendekezo ya wawania tuzo zaidi ya 54, 034 huku kura zaidi ya 100,000 zikipigwa katika vipengele 50.
Kwa taarifa zaidi tembelea
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇