LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Dec 23, 2020

NDALICHAKO AWATANGAZIA KIAMA WAKUU WA SHULE WADANGANIFU WA MITIHANI+VIDEO

Viongozi waliopo meza kuu wakiongozwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako wakipiga makofi baada ya kumaliza kuimba wimbo wa Taifa wakati wa kufunga Mkutano Mkuu 15 wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania TAHOSSA, jijini Dodoma Desemba 22,2020. Mratibu Mkuu wa mkutano huo ni Taasisi ya Global Education Link. PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,Profesa  Joyce Ndalichako akihutubia alipokuwa akifunga Mkutano Mkuu wa 15 wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA), kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete katika Kituo cha Mikutano cha Dodoma Desemba 22,2020. Zaidi ya walimu 2000 walihudhuria. 
Sehemu ya Wanachama wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA), wakiimba wimbo maalumu wa kuonesha mshikamano wa TAHOSSA  kabla ya  Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa  Joyce Ndalichako kufunga Mkutano Mkuu wa 15 chama hicho, kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete katika Kituo cha Mikutano cha Dodoma . Zaidi ya walimu 2000 walihudhuria. PICHA NA RICHARD MWAIKENDA
Katiu Mkuu wa Wazara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Joseph Nyamhanga akitoa maneno ya utangulizi kabla ya kumkaribisha Profesa Ndalichako.
Wajumbe wa mkutano huo, wakipiga makofi baada ya kufurahishwa na hotuba ya Waziri Ndalichako
Viongozi walio meza kuu wakiongozwa na Waziri Ndalichako wakiwa wameshikana walipokuwa wakiimba wimbo maalumu wa TAHOSSA.


Naibu Waziri wa Tamisemi (Elimu),  David Silinde akihutubia mkutano wa TAHOSSA na kuwataka wakuu wa shule kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa vyumba vya madarasa, vyoo na miundombinu mingine ili wanafunzi waliochaguliwa  kuingia kidato cha kwanza wasikose nafasi. Aliagiza ujenzi huo ukamilike kabla ya Februari 2, 2021.
Profesa Ndalichako akipongezwa na Mwenyekiti wa TAHOSSA kwa hotuba yake nzuri.
Waziri Profesa Ndalichako akimkabidhi tuzo maalumu ya TAHOSSA, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Bwawani, Chalinze mkoani Pwani, Musiba Evarist kwa kuonesha vifaa vipya vya kufundishia hisabati wakati wa mkutano huo.
Waziri Profesa Ndalichako akimkabidhi tuzo maalumu ya TAHOSSA, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Kawe Ukwamani Kinondoni, Dar es Salaam, Esther Mlewa  kwa kuonesha vifaa vipya vya kufundishia hisabati wakati wa mkutano huo.


Waziri Profesa Ndalichako (wa pili kulia), akipata maelezo kuhusu utendaji wa Taasisi ya Global Education Link alipotembelea banda hilo kwenye maoneho yaliyofanyika sambamba na mkutano mkuu wa TAHOSSA.  Anayetoa  maelezo (kulia) ni Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Abdulmaliki Mollel ambaye pia ni mratibu mkuu wa mkutano huo.
 

Waziri Profesa Ndalichako (wa pili kulia), akipata maelezo kuhusu utendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alipotembelea banda hilo kwenye maonesho yaliyofanyika sambamba na mkutano mkuu wa TAHOSSA.  Kushoto ni Naibu Waziri wa Tamisemi (Elimu), David Silinde.


Na Richard Mwaikenda, Dodoma.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojis, Profesa Joyce Ndalichako amewatangazia kiama walimu wakuu wa shule za Sekondari nchini, wanaoshiriki katika sakata la udanganyifu wa mitihani.


Akihutubia wakati wa kufunga  Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA), jijini Dodoma Desemba 22, 2020, Profesa Ndalichako, alisema serikali haitosita kuwachulia hatua walimu wakuu wanaoshiriki kwenye vitendo hivyo viovu.


Amesema ni aibu tena fedheha kwa mwalimu mkuu ambaye amepewa dhamana ya kuiongoza shule kinidhamu na kitaaluma, kushiriki katika udanganyifu kwa kuiba mitihani na kuwapatia majibu wanafunzi kwa lengo batili la shule kupata ufaulu mzuri.


"Haiwezekani udanganyifu ufanyike katika darasa zima bila mkuu wa shule kujua au kuhusika, nawaonya acheni kabisa tabia hiyo, hatuwataki kabisa wadanganyifu," alisema na kusisitiza kwamba...


Natangaza kiama kwa watu wenye tabia hiyo mbaya, tutakuwa wakali sana kwenye jambo hili, tutawatimua kazi na kuwachukulia hatua kali za kisheria, ikiwemo kuwatimua kazi, wapo wengi wanaohitaji kazi hiyo ya ualimu."


Profesa Ndalichako alitoa mfano uliotokea katika shule moja mkoani Kagera, ambapo Mkuu wa Shule alikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) akiwasaidia wanafunzi kupata majibu ya mtihani.


Alisema kuwa ni aibu kwa mkuu wa shule kushiriki kwenye udanganyifu huo, kiasi kwamba wengine hushiriki kutuma majibu ya mtihani kwa meseji, akigundulika atatiwa hatiani yeye, lakini mwanafunzi akikutwa ameandika majibu kwenye mapaja na kwenye nguo zao, hilo halitakuhusu ataadhibiwa mwanafunzi.


Waalimu walipoulizwa na Profesa Ndalichako, kuwa wanafikiri sababu kubwa ya kufanya udangayifu huo ni nini?, walijibu kuwa mara nyingine wanatishwa na maafisa elimu kwamba shule isipofanya vizuri kwenye mitihani watafukuza kazi.


Profesa Ndalichako, alisema ni kweli wana taarifa hizo za maafisa elimu kuwatisha, aliwaonya maafisa hao na kwamba kwa yeyote atakayemtishia mwalimu 'atakula naye sahani moja'.


Aliwataka walimu wakuu kutoogopa kuwapa taarifa ya afisa elimu yeyote alikayeshiriki kuwatishia na watakaotoa taarifa watalindwa. Mkutano huo ulihudhuriwa na zaidi ya wakuu wa shule 2000 za binafsi na za serikali. Mratiu Mkuu ilikuwa ni Taasisi ya Global Education Link.


Aliwaasa walimu kujibidisha katika ufundishaji kitaaluma na kinidhamu ambayo ndiyo dawa pekee ya shule zao kupata ufaulu mzuri kuliko kushiriki kwenye udanganyifu wa mitihani.


Aliwataka maafisa elimu badala ya kukimbilia kuwatimua  kazi walimu wa shule zinazofanya vibaya, kwanza waangalie kinachosababisha shule hizo kutofanya vizuri na kutatua kwanza changamoto zinazozikabili.


Alisema katika baadhi ya shule za aina hiyo, tatizo linakuwa siyo walimu bali ni matatizo ya muda mrefu yaliyopo katika shule hizo, hivyo ni bora kuyatatua, ama sivyo kila walimu watakaopangiwa shule hizo watakuwa wanafukuzwa kwa kuonewa.


Pamoja na mambo yote hayo, Profesa Ndalichako hakusita kuwapongeza walimu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya usimamizi mzuri katika shule zao, kiasi sasa kwa miaka ya hivi karibuni ufaulu umeongezeka, hivyo kiwango cha elimu kupanda.


SIKILIZA CLIP HII YA VIDEO PROFESA NDALICHAKO AKIHUTUBIA MKUTANO HUO WA TAHOSSA.

IMEANDALIWA NA;
 RICHARD MWAIKENDA 
MHARIRI LOG YA TAIFA YA CCM 
0754264203

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages