*****************************************
KAZI imeanza! Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Morogoro, Godwin Kunambi kuanza ziara jimboni kwake ambapo amefanya mkutano katika kata ya Uchindile ambapo amechangia mifuko 50 ya Saruji kwa ajili ya Ujenzi wa Zahanati katika kijiji cha Lugala.
” Nimefika leo kwa kazi mbili, moja kuwashukuru kwa kumchagua Rais Dk John Magufuli na kweli kura zote mlimpa, yapo mengi niliwaahidi wakati wa kampeni lakini mimi nimeona uhai ni bora zaidi, hivyo tutaanza ujenzi wa Zahanati ya kijiji chetu hivyo nachangia mifuko 50 ya saruji ili ujenzi uanze mara moja, lengo langu ni kuona wote mnatibiwa katika Zahanati hii.
Kwenye ziara yangu nimetembelea kiwanda cha karatasi cha Mufindi Papers Mills tumeongea nao na wamekubali kutujengea Kituo cha Afya kama sehemu ya mchango wao kwetu kwa kuwa wamewekeza katika kata yetu, hivyo kuanzia Januari 15 ujenzi wa kituo hiko utaanza, lengo langu ndani ya mwaka mmoja ni kuona wananchi wa Uchindile wakiepukana na changamoto ya kufuata huduma za afya umbali mrefu.
Kwenye elimu nilipofika hapa mliniambia kuna changamoto ya uhaba wa walimu, nimepambana wametuletea walimu wanne, najua bado changamoto ipo niwahakikishie tutapambana pamoja kuhakikisha serikali inatuongezea tena walimu wengine ili watoto wetu wapate elimu bora itakayokua msaada kwao na kwenye Jimbo letu kwa ujumla,” Amesema Mbunge wa Mlimba, Godwin Kunambi.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇