LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 28, 2020

MAADHIMISHO YA KUMBUKIZI YA MIAKA 40 YA NIMR YAFANA DODOMA

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa,Dk Selemani Serera  akihutubia wakati wa kumbukizi ya maadhimisho ya miaka 40 ya Taasisi ya ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania kwenye viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma Novemba 27,2020. Dk Serera alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge ambaye alikuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo.Kutoka kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa NIMR Dodoma, Dk. Lucas Matemba, Dk. Mary Mayige Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa NIMRY, Dk.Yunus Mgaya.

PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA, CCM BLOG.

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa,Dk Selemani Serera akipima afya wakati wa maadhimisho hayo.


Dk. Mary Mayige Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa Nimr .Yunus Mgaya akitoa neno wakati wa maadhimisho hayo.

Wananchi wakipata huduma za upimaji wa afya wakati wa maadhimisho hayo.


Mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Francis Bujileu akielezea umuhimu wa Taasisi ya Nimr katika utafiti wa dawa za asili za kutibu magonjwa mbalimbali ya binadamu. Kutoka kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa,Dk Selemani Serera  na Monica Kessy Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa.


Mmoja wa wananchi akipima urefu ikiwa ni sehemu ya upimaji wa afya huduma ambayo ilifanyika sambamba wakati wa maadhimisho hayo.


Baadhi ya dawa ambazo NIMR inazifanyiwa majaribio na zilizofanikiwa kutibu magonjwa mbalimbali ya binadamu 



Hotuba ya Mh.Dr. Benilith Mahenge Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Dok. Selemani Serera  wakati wa Maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 40 ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania.

 

Mkurugenzi Mkuu, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu, Tanzania

 

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma

 

Mkurugenzi wa NIMR kituo cha Dodoma

 

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Benjamin Mkapa.

 

 

Wageni waalikwa

Waandishi wa Habari

Mabibi na Mabwana,

Habari za asubuhi,

 

Nina heshima kubwa kupata fursa hii ya kusema maneno machache katika maadhimisho haya muhimu. Awali ya yote, napenda kuwakaribisha wote katika maadhimsho haya na napenda kutambua kazi kubwa inayofanywa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu hasa kwa kupambana na adui yetu  mkubwa ambaye ni magonjwa ya Binadamu.

 

Ni furaha yangu kubwa kuwa nanyi hapa leo.

 

Mabibi na Mabwana,

Nimeelezwa kuwa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu iliazishwa mwaka 1979, na ilianza kutekeleza majukumu yake mwaka 1980. Napenda kuipongeza Taasisi hii kwa kuadhimisha umri wa miaka 40 tangu ilivyoanza kutekeleza majukumu yake. Ikumbukwe kwamba nchi yetu ilivopata uhuru mwaka 1961, Rais wa awamu ya kwanza Mwl.Julius Kambarage Nyerere aliwatangazia wananchi kuwa serikali yetu inao maadui watatu wakubwa ambao ni Umasikini, Ujinga na Maradhi, ninyi ni mashahidi kuwa hawa maadui aliowatangaza Mwl.Nyerere mwaka 1961 bado ni maadui zetu hata leo, magonjwa bado yapo yanasumbua binadamu na si kwa waTanzania tu bali Dunia nzima hata nchi zilizoendelea. Nimeelezwa kuwa Taasisi hii inafanya utafiti wa magonjwa ya Binadamu kwa nia ya kupata njia bora zaidi za kisayansi za kukabiliana na adui magojwa kwa lengo la kuboresha afya ya watanzania na Jamii yote kwa ujumla. Afya ya Binadamu ni muhimu sana na ni mtaji wa kwanza katika maendeleo ya Mwanadamu, ili Dodoma na jamii yetu iweze kusonga mbele tunahitaji mazingira salama yasiyokuwa na magonjwa pia mbinu bora na za kisayansi katika kupambana na adui magonjwa. Kwa mantiki hiyo Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu mnalo jukumu kubwa  kujibu matarajio ya jamii yetu kama alivyoelekeleza Baba wa Taifa  letu Mwl. Nyerere kuwa tunatakiwa kupambana na maadui zetu hao watatu ambao nimewataja hapa awali, Taasisi hii ikifanikiwa kupata njia bora ya kutokomeza magonjwa tayari itakuwa imeondoa umasikini unaosababishwa na magonjwa yanayomshambulia Binadamu na kumdhoofisha kiafya, kiuchumi na hata kusababisha kifo.

 

Mabibi na Mabwana, Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Mzalendo Mwenzetu Mheshimiwa Dr.John Pombe Magufuri inalenga zaidi katika kuimarisha miundo mbinu ya utoaji huduma za afya ya Binadamu kwa lengo la kuwezesha kila mTanzania awe na  afya bora kwa, hivyo jukumu la Taasisi hii ni muhimu katika kutekeleza malengo ya Serikali kwa kuwa bila utafiti hatuwezi kupata njia bora za Kisayansi za kukabiliana na magonjwa.

 

 Mabibi na Mabwana, napenda nitumie fursa hii kuwapongeza Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu, kwa kazi kubwa mnayoifanya kutafti njia bora za kutokomeza magonjwa, kama kifua kikuu, Ukimwi, Malaria na mengineyo, kazi kubwa mnayoifanya ni ushahidi tosha kuwa Taasisi hii inachochea utekelezaji wa malengo ya serikali ya awamu ya tano hongereni sana. Natumaini mnaelewa kuwa hakuna Binadamu anaeweza kuendelea ikiwa hajaweza kudhibiti magonjwa katika mazingira yake. Kwa hiyo ninawaagiza NIMR mfanye utafiti na kutoa suruhisho kwa magonjwa yanayosumbua Dodoma na ikiwezekana magonjwa hayo yatokomezwe kabisa ili katika mkoa wetu Dodoma tufanye shughuli za maendeleo tukiwa na afya njema pasipo kukwamishwa na magonjwa.

 

Mabibi na Mabwana,

Leo hii tunapoadhimisha miaka 40 ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa  Magonjwa ya Binadamu Tanzania, tunatakiwa kujikita katika kufanya tafiti zenye kujibu matatizo ya WaTanzania hususan kwa mkoa wetu wa Dodoma. Tafiti mnazozifanya zitakuwa na tija kwa waTanzania iwapo mtalenga kupata njia bora za kutokomeza magonjwa ambayo yanasumbua jamii yetu hivi leo, Maendeleo ya familia zetu, jamii yetu na Taifa letu, yanategemea WaTanzania wenye afya njema. Kwa kuzingatia majukumu ya Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu, ninyi ndiyo washauri wa Serikali kuhakikisha tunapata njia bora na sahihi za kisayansi katika kukabiliana na magonjwa, kwahiyo mnapoadhimisha miaka 40 ya Taasisi hii muwekeze zaidi katika kuisaidia jamii yetu kupata njia bora za kutokomeza magonjwa yote yanayoikabili jamii yetu ili tuishi katika jamii isiyo na magonjwa.

 

Mabibi na Mabwana, Nitumie fursa hii kuwakaribisha Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu hapa Dodoma. Kufunguliwa kwa kituo chenu hapa Dodoma umekuja wakati muafaka hasa ukizingatia kuwa tuna ongezeko kubwa la watu pamoja na kupanuka kwa jiji la Dodoma, jambo ambalo mara nyingi linaambatana na mabadiliko makubwa ikiwemo pia ongezeko la magonjwa ikiwa ni pamoja na yale yasiyoambukiza. Kwa maana hiyo uwepo wenu hapa utakuwa na manufaa makubwa kwa wanaDodoma na Jamii yote kwa ujumla, iwapo mtawekeza katika kutafuta mbinu bora na sahihi za kuzuia na hata kutokomeza kabisa magonjwa haya. Kwa mantiki hiyo ninaamini tukishirikiana vizuri nyinyi watafiti pamoja na wataalam wangu wa Afya, tutaijenga Dodoma isiyo na Magonjwa.

 

AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA.

 

 

 

 

 

 

 


No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages