LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Nov 4, 2020

LUKUVI APOKEA TAARIFA YA AWALI YA UHAKIKI ENEO LA MGOGORO MTAKUJA DODOMA

 


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akifuatilia uwasilishaji Taarifa ya Uhakiki wa wananchi wanaomiliki maeneo yenye mgogoro eneo la Mtakuja lililopo kata ya Chang’ombe leo tarehe 4 Oktoba 2020 jijini Dodoma. Wengine katika picha ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira Anthony Mavunde (wa pili kushoto), Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Mary Makondo (wa Kwanza kushoto), Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nicolaus Mkapa (kushoto kwa Waziri) na Kamishna wa Ardhi Nathaniel Nhonge (wa pili kulia).

Kamishna Msaidizi wa Ardhi Uratibu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Wilson Luge akiwasilisha Taarifa ya Uhakiki wa wananchi wanaomiliki maeneo yenye mgogoro katika eneo la Mtakuja lililopo kata ya Chang’ombe leo tarehe 4 Oktoba 2020 mkoani Dodoma.

Afisa Mipango Miji Eliza Lushu (Kushoto) akihakiki taarifa za mkazi wa Mtakuja kata ya Chang’ombe mkoa wa Dodoma Enesmo Lucas Sunday wakati timu ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikiendesha zoezi la uhakiki wananchi wanaomiliki maeneo yenye mgogoro katika eneo hilo lenye ukubwa wa hekta kumi.

Mkazi wa eneo la Mtakuja mkoani Dodoma Bi. Janet Charles Mwaluko (Kushoto) akitia saini ikiwa ni ishara ya kukubaliana na uhakiki unaoendelea eneo lenye mgogoro la Mtakuja katika kata ya Chang’ombe.

Mkazi wa Mtakuja mkoani Dodoma Stanslaus Barayata (wa tatu kushoto) akihakiki taarifa zake kutoka kwa Afisa Mipango Miji Eliza Lushu (wa pili kulia) wakati wa zoezi la uhakiki wananchi wanaomiliki maeneo yenye mgogoro eneo la Mtakuja lenye ukubwa wa hekta kumi. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Wananchi katika eneo hilo Kinara Vangiringa Mwilafi.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi (wa Tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na timu inayoshiriki zoezi la uhakiki katika eneo lenye mgogoro la mtakuja kata ya Chang’ombe mkoa wa Dodoma baada ya kupata taarifa ya maendeleo ya zoezi hilo jana. Wengine katika picha ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana na Ajira Anthony Mavunde (wa tatu Kulia) Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Mary Makondo (wa pili kushoto) na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nicolaus Mkapa (wa kwanza kushoto). (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI). 

………………………………………………………………..

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amepokea taarifa ya awali ya uhakiki wa eneo lenye Mgogoro la Mtakuja lilipo Kata ya Chang’ombe mkoani Dodoma.

Taarifa ya uhakiki wa eneo hilo lenye ukubwa hekta kumi uliwasilishwa leo tarehe 4 Oktoba 2020 katika ofisi za Wizara eneo la Mtumba jijini Dodoma na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Uratibu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Wilson Luge kwa niaba ya timu inayofanya uhakiki kwa wakazi wanaoishi eneo hilo.

Uwasilishaji taarifa hiyo unafuatia kukwama kwa mara kadhaa mazoezi yaliyofanyika huko nyuma na kusababisha Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi kuelekeza kufanyika uhakiki mwingine ili kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro wa muda mrefu kwenye eneo hilo.

Kwa mujibu wa Kmaishna Msaidizi wa Ardhi Uratibu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Wilson Luge, tayari timu ya uhakiki mgogoro huo imeshawapitia wananchi 750 kati ya 1,025 watakaofanyiwa uhakiki.

Luge alisema, kazi kubwa inayofanywa na timu ya uhakiki ni kupitia taarifa ya kila mwananchi na kuangalia hali ya maendelezo yaliyofanyika katika kila eneo la mwananchi analomiliki.

Mazoezi ya uhakiki eneo la Mtakuja Kata ya Chang’ombe mkoa wa Dodoma yamefanyika mara kadhaa katika miaka ya 2005, 2008 na 2015 ambapo zoezi linaloendelea sasa linatarajiwa kuleta suluhu ya mgogoro huo.

Uwasilishwaji taarifa ya uhakiki wa mgogoro wa eneo la Mtakuja Dodoma, ulihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi,Vijana na Ajira ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mary Makondo, Naibu wake Nocolaus Mkapa, Kamishna wa Ardhi Nathaniel Nhonge na Watendaji wa Wizara, Jiji la Dodoma pamoja na wa Kata ya Chang’ombe.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages