Jumatano ya Oktoba 28, 2020, yaani wiki hii Watanzania Walifanya Uchaguzi na Taifa lingine kubwa la Afrika ya Magharibi la Ivory Coast ambako Rais aliyekuwa madarakani Alassane Quattara alichaguliwa tena kuiongoza nchi hiyo kwa muhula wake mwingine.
Kama ilivyo kawaida wapinzani wake watatu, Rais wa zamani wa nchi hiyo Henri Konan Bedie wa Chama cha PDCI, Pascal Affi N'Guessan na Kouadio Konan Bertin wamekataa matokeo yaliyompa ushindi Alassane Quattara na kudai hawayatambui.
Nchi kubwa na washirika wakubwa wa nchi hiyo Ufaransa chini ya Rais wake Emmanuel Macron wameutambua ushindi wa Alassane na Rais Macron ametoa povu zito sana kwa wapinzani wa nchi hiyo na Afrika kwa ujumla. Rais Macron anasema kuna kaugonjwa flani hivi Afrika kwa watu kuingia kwenye uchaguzi halafu wakishindwa wanakataa matokeo na kutoa malalamiko mengi sana.
"Kama ulitambua tume sio huru, unajua utaibiwa kura kwanini ushiriki uchaguzi huo?" amesema Rais huyo wa Ufaransa Emmanuel Macron wakiwahoji wanasiasa wote wa Afrika ambao kila wanaposhindwa katika Uchaguzi hukataa matokeo na kutoa malalamiko tele.
Sasa tukija hapa Tanzania, baada ya uchaguzi uliofanyika wiki hii, kama ilivyo kawaida ya Ushindani ni lazima atokee anayeshinda na anayeshindwa, sasa baada ya matokeo na Mgombea wa Chama Tawala CCM Dk. John Magufuli kutangazwa mshindi tena kwa kupata kura za kishindo, kuna watu wameshindwa uchaguzi na tayari tumeshuhudia wakitoa matamko na malalamishi yaleyale aliyoyakemea Rais Macron.
Tusishangae! Narudia tusishangae mana ndio kawaida ya wapinzani sio tu hapa Tanzania bali ni Afrika nzima hii, na wala sio mwaka huu tu bali ni kila mwaka. 2015, 2010, 2005, 2000 na 1995 kote walikataa matokeo. Kenya, Ivory Coast, Sudan, Msumbiji, Uganda na kote waliko wapinzani ndio jadi na kawaida yao kukataa matokeo. Kwahiyo Watanzania wala tusishangae.
Haitakuwa mwanzo wala mwisho uchaguzi huu wapinzani kukataa na kutoyakubali matokeo. Ndivyo walivyo. Hata pawe na Tume gani? Hata pawe na mazingira gani na hata uchaguzi uendeshweje lakini tegemea Chama cha siasa tena kwenye mfumo huu wa kidemokrasia mmoja au wawili hivi wakatae matokeo. Ni jambo la kawaida sana hapa Afrika.
Kitu pekee ninachoweza kuwaomba na kuwaasa sana Watanzania ni amani! amani! amani!. Dunia nzima inaimezea mate Tanzania. Kufanya uchaguzi mkuu kwa amani na utulivu kiasi hiki ni neema isiyo na kifani.
Kuna nchi zimefanya uchaguzi miaka 10 au 5 imepita lakini hadi leo bado watu wanavurugana tu. Hakuna kazi wala chochote kinachoendelea zaidi ya kuponya na kutuliza migogoro tu. Hapa tumepata bahati, mnafanya uchaguzi mpaka unaisha hujasikia hata mlio wa bunduki na watu kulala maporini. Hii ni bahati na haijawahi kutokea kokote duniani zaidi ya Tanzania tu.
Watanzania tusijaribu kuichezea hii amani tuliyobarikiwa. Kamwe tusijaribu. Anapotokea mtu akakwambia andamana, mwambie kwanza aanze yeye. Atoe mkewe, baba na mama yake na watoto wake ndo waandamane na wawe mstari wa mbele. Wewe baba, mama na kijana unayetaka kushawishika uamke asubuhi ukaandamane, kabla ya kwenda jiulize familia yako itakula nini? Na wewe kijana mwenye ndoto zako nyingi, leo eti uharibu hizo ndoto kisa fulani kakosa madaraka anataka ayapate kwa kumwaga damu yako! Usijaribu. Kumbuka maneno ya Rais Mstaafu Jakaya Kikwete aliwahi kusema "akili za kuambia changanya na zako", sasa wakati ni huu.
Kwenye mfumo wa kawaida wa kidemokrasia ya vyama vingi mshindi lazima apatikane na baada ya uchaguzi hapa nchini tayari mshindi ameshapatikana. Kilichosalia sasa ni Watanzania tuondoe tofauti zetu za kisiasa, turudi wote kama Taifa kuendelea na ujenzi wa nchi yetu. Hili pekee kwa sasa ndilo la msingi sana kwa Watanzania wote.
Imeandikwa na Na Bwanku M Bwanku (0657475347) na Kuhaririwa na Msimamizi Mkuu wa Blog hii Bashir Nkoromo (0712498008)
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇