LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 6, 2020

VITENDO VINA SAUTI NA TAKWIMU ZINAONGEA RAIS MAGUFULI KUSHINDA UCHAGUZI HUU

Dk. John Magufuli

Kwa mfululizo wa vitendo vinavyotoa sauti, kuonwa na kusikika kwa kila mtu na mfululizo wa takwimu zilizoshiba za kazi  alizozifanya Rais Dk. John Magufuli kwa miaka mitano tu ya uongozi wake hapana shaka kila mwananchi atakapofika kwenye sanduku la kupiga kura siku ya Jumatano ya tarehe 28 mwezi huu, hataanza kujiuliza nani wa kumpigia kura ya kiti cha Urais, bali atachukua tu kura yake na kuweka alama ya vema ilipo nembo ya CCM na picha ya Dk.  Magufuli ili kazi iendelee.


Baadhi ya mambo makubwa aliyofanika katika uongozi uliosimamiwa na Rais Dk. Magufuli kwa kasi kubwa ni pamoja na utekelezaji wa miradi 1423 ya maji yenye thamani ya Sh. trilioni 1.2 nchi nzima, ambayo imefanya upatikanaji wa maji Vijijini kuongezeka kutoka asilimia 47 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 70.1 na mijini upatikanaji wa maji ukiongezeka kutoka asilimia 74 mwaka 2015 hadi asilimia 84 mwaka huu. 


Umoja wa Mataifa (UN) unasema uwekezaji huu mkubwa wa Serikali ya awamu ya 5 kwenye sekta hii muhimu ya maji imeifanya Tanzania kuokoa takriban Sh. trilioni 5.2 ambazo Serikali ingetumia kutibu watu magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa maji safi na salama.


Kwenye Sekta ya umeme kila mmoja ameshuhudia mapinduzi ya kihistoria kwa nchi kutoka vijiji 2018 vilivyokuwa na umeme toka Tanzania ipate uhuru na alivyovikuta Dk. Magufuli mwaka 2015, Sasa kwa miaka 5 tu Rais huyu ameshafanikisha kupelekwa umeme hadi kufikia zaidi ya vijiji 9570 na kubakiza vijiji chini ya 2500 tu hivyo kuonyesha kuwa nchi imefikisha asilimia 85 ya vijiji vyenye umeme kutoka chini ya asilimia 35 mwaka 2015 na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika kwa usambazaji mkubwa wa umeme vijijini.


Hii inajumuisha Serikali chini ya Rais Magufuli kupunguza kwa zaidi ya asilimia 60  gharama ya kuunganisha umeme kutoka 177,000 mwaka 2015 hadi 27,000 tu, jambo lililowafanya Watanzania wengi sana hata wenye vipato vya chini kabisa kuunganisha umeme.


Mafanikio haya yanaifanya Tanzania kupita maoteo ya Benki ya Dunia (WB) ambayo yalikadiria kwamba suala la umeme kwa wote kufikiwa litafikiwa kwenye karne ya 22 yaani mwaka wa 2101, lakini kwa kasi hii ya Rais Magufuli ambaye ameshasema hadi kufikia mwaka 2025 vijiji vyote nchini vitakuwa na umeme hivyo Tanzania kufika kwenye maoteo ya WB kabla hata ya muda wake wa takriban miaka 75 ijayo.


Hii inaendana na Tanzania kuongoza kwa bei nafuu ya umeme kwa kaya kwa ukanda mzima wa Afrika Mashariki ambapo Tanzania inauza uniti 1 kwa senti 10, Uganda senti 18, Kenya senti 21 na Rwanda senti 26.


Yote haya yanafanikiwa kwa sababu ya Serikali ibayoongozwa na Rais Magufuli kuwa na misingi mizuri ya usimamizi wa fedha ikiwemo kupambana na vitendo vya rushwa, ufisadi, ubadhirifu na uzembe ambapo Jukwaa la Uchumi duniani (WEF) kwenye ripoti yao ya mwaka jana (2019) iliitaja Tanzania kuwa ya 28 duniani kwa usimamizi madhubuti wa fedha na kuziacha nchi majirani na zingine kubwa duniani kwa mbali sana.


Nchi ambazo zipo jirani ambazo WEF imezitaja kupitwa na Tanzania ni pamoja na Kenya ambyo ipo nafasi ya 70, Botswana 37, Msumbiji 69, Uganda 100 na Malawi 106. 


Hii inathibitika pia kwa namna watu walivyo na imani kubwa na Serikali yao kwa kupambana na rushwa ambapo Taasisi ya Kimataifa ya Uwazi ya Transparency International (Global Africa Corruption Barometer ya 2019) ilisema asilimia 72 ya wananchi wana imani na Rais Magufuli  katika vita dhidi ya ufisadi kulinganisha na asilimia 13 tu ya Watanzania ambao mwaka 2015 ndio pekee walikubali nchi yao kupambana na ufisadi.


Usimamizi huu mzuri wa rasilimali fedha uliosimamiwa na Rais Magufuli, ndio umeifanya Tanzania kuwa na uwezo mkubwa wa kutekeleza kwa fedha zake yenyewe za ndani  miradi  mikubwa ya kimkakati kama Ujenzi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere (Stirglers Gorge) inaotekelezwa kwa gharama ya sh. trilioni 6.5, ujenzi wa reli ya kisasa na ya mwendo kasi ya Standard Gauge (SGR) unatekelezwa kwa ghara ya Dola za Kimarekani bilioni 1.92 na kutoa elimu bila malipo kwa sababu fedha zote zilizokuwa zinaliwa na mafisadi zimekombolewa kwa kudhibiti wizi, ubadhirifu, ufisadi na matumizi yasiyo ya lazima.


Eneo la afya ambalo ni la msingi sana ili kujenga Taifa lenye ustawi, Serikali imeshajenga vituo 1769 vya kutolea huduma za afya zikiwemo zahanati 1198, hospitali za wilaya 71, za mikoa 10 na za kanda 3 ikiwemo ujenzi wa hospitali ya mkoa wa Mara ambayo ilisimama toka miaka ya 1970, kupandisha bajeti ya dawa na vifaa tiba kutoka sh. bilioni 30 hadi Sh. bilioni 270, kuajiri watumishi 14,479 wa kada za afya na mengine mengi sana.


Mapinduzi haya makubwa kwenye sekta ya afya ndio yaliyolifanya Shirika la Afya Duniani (WHO) kuitaja Tanzania kupunguza maambukizi ya malaria kwa asilimia 50 kutoka asilimia 14.2 mwaka 2014 hadi asilimia 7 mwaka 2018.


Kutoa elimu bila malipo ambapo Serikali imeshatumia takriban sh. trilioni 1.01 kugharamia ambapo kutangazwa tu kwa fursa hiyo na Serikali, idadi ya wanafunzi wanaojiunga na darasa la kwanza iliongezeka kutoka wastani wa wanafunzi milioni 1 hadi milioni 1.6, jambo lililookoa malaki kwa malaki ya watoto wa maskini ambao walikuwa wanakosa fursa ya kupata elimu. 


Kumbuka Takwimu hizi zote zinatolewa na hao hao Wazungu wenyewe ambao mapema mwezi Julai mwaka huu Benki ya Dunia iliitangaza Tanzania kuingia uchumi wa kati kutoka nchi maskini kabisa.


Tanzania ilitangazwa na Benki ya Dunia kuingia Uchumi wa kati kwa haraka zaidi kabla hata ya mpango wake wa maendeleo ambao uliikadiria Tanzania kuingia uchumi wa kiwango hicho ifikapo mwaka 2025.


Kila mtu amemkubali Rais Magufuli na Serikali yake, nani tena abishe? Hapo hujaenda kwenye mapinduzi makubwa yaliyopatikana kwenye miundombinu ya barabara ambapo kwa mara ya kwanza toka Tanzania iasisiwe ilipeleka fedha za miradi ya barabara kwenye mikoa na wilaya zote nchini.


Ununuzi wa ndege 11 baada ya kusugua miaka kwa miaka na mindege ya kukodi na mibovu. Hujaenda kwenye mapinduzi mazito yaliyofanyika kwenye madini, utalii, kilimo na kwingine kwingi. Kwa bahati mbaya ukurasa hautoshi.


Mambo ni mengi sana lakini kwa uchache na kwa kumalizia ni eneo la amani na utulivu ambapo ndipo msingi wa utekelezaji wa mipango yote ya maendeleo. Hapa bado Serikali hii imeendelea kuweka mkazo mzito sana kwa kuifanya Tanzania kuendelea kuwa kitovu na kisiwa cha amani kote duniani jambo lililofanya mtandao wa Global Peace Index unaohusika na kupima hali ya amani duniani kuitaja Tanzania kuwa nchi yenye amani na utulivu wa hali ya juu sana Afrika na dunia kwa ujumla. Kwa mujibu wa ripoti ya mtandao huo mwaka 2020 iliitaja Tanzania kuongoza kwa amani na utulivu Afrika Mashariki, huku ikishika nafasi ya 6 barani Afrika na 52 duniani. Kwa vitendo na takwimu hizi chache tu kati ya nyingi zilizotapakaa kwenye kila sekta inatosha kusema Mitano Tena kwa Dkt John Pombe Magufuli ili kazi iendeleeee.

//Makala hii imeandikwa na Bwanku Bwaju : 0657475347, Imehaririwa na B. Nkoromo Msimamizi Mkuu wa Blog ya Taifa ya CCM.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages