Benki ya NMB
imeshinda tuzo ya umahiri baada ya kuibuka benki salama zaidi Tanzania kwa
mwaka 2020.
Tuzo hizo zimetolewa
Jumatatu tarehe 20 Oktoba, 2020 na Jarida la kimataifa la Global Finance la
jijini New York, Marekani lililojikita katika uchapishaji wa habari za masoko
ya fedha na mitaji ulimwenguni.
Tuzo za
benki salama zaidi hufanyika kila mwaka kwa kila bara na kwa kila nchi duniani na
hutolewa baada ya kufanyika tathmini ya kina kwa kuzingatia viwango vya makampuni
ya Moody’s, Standard & Poor’s na Fitch - vigezo hivi ni vya kimataifa
vinavyotoa taarifa za afya za mabenki na uwezo wa makampuni kujiendesha.
Tuzo hii
imekuja miezi michache tu baada ya Benki ya NMB kutunukiwa tuzo ya kuwa benki
bora zaidi Tanzania kwa mara ya nane mfululizo na Jarida la Euromoney lenye
makao makuu jijini London nchini Uingereza linalochapisha habari za masoko ya
fedha na mitaji pia.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna amesema: “Ni heshima kubwa kwetu kutambulika kama
benki salama zaidi na yenye uwezo wa kuendelea na biashara kuleta faida kwa
wanahisa wetu na nchi kwa ujumla. Tuzo hii ni ishara ya uimara wa Benki ya NMB kuhudumia
wateja katika soko lenye ushindani na mazingira yanayobadilika kila wakati. Wakati wasiwasi wa janga la Covid-19
ukiendelea kuisumbua dunia, tuzo hii inadhihirisha uimara, utulivu na kasi yetu
ya kubadilika kiteknolojia kuwawezesha wafanyakazi, wateja wetu na watanzania
kwa ujumla kufanikisha malengo yao ya kiuchumi.”
Zaipuna amesema
tuzo hii inaonyesha juhudi kubwa ya Benki ya NMB kutoa huduma bora na salama
kwa wateja wake kwa viwango vya kimataifa na kuweka mustakabali wa huduma za kibenki
nchini.
Taarifa za
fedha za Benki ya NMB zinaonyesha kwa mwaka 2019 benki ilipata faida ya TZS 142
bilioni baada ya kodi ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 46 kutoka TZS 98 bilioni
iliyopata mwaka uliotangulia hivyo kuifanya iendelee kuwa benki inayopata faida
kubwa zaidi nchini kwa zaidi ya muongo mmoja sasa. Kwa sasa mali za benki ya
NMB zimefikia Zaidi ya shilingi trilioni 7.
Miongoni mwa wanahisa wa Benki ya NMB ni Rabobank yenye asilimia 34.9
pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yenye asilimia 31.8.
Joseph D. Giarraputo, Mhariri Mkuu wa Jarida la Global Finance
amesema: “Janga la corona limeathiri sehemu kubwa ya
biashara kwa mwaka 2020 hivyo kufanya utabiri na makisio duniani kuwa mgumu;
lakini biashara lazima iendelee. Benki ya NMB ni mfano wa taasisi iliyokuwa
imejipanga kuinuka na kuchangamkia fursa za kutoa huduma mbadala za kibenki kidijitali katika
kipindi cha janga la corona hivyo kuwa salama hata sasa. Matokeo ya tuzo hii
yatatumiwa na kampuni kubwa, wawekezaji hata watu binafsi kupima usalama wa
benki wanayopenda kufanya nayo biashara.”
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇