Wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma imebarikiwa kuwa na fukwe za asilikatika ziwa Nyasa ambazo hazifanani na fukwe nyingine zozote duniani na endapo zitaendelezwa zinaweza kuwa chanzo muhimu cha mapato kwa serikali na wananchi.
Fukwe ya Mhalo iliyopo katika kijiji cha Ruhekei Kata ya Kilosa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa imeendelezwa kwa kujengwa vivutio vya utalii pamoja na hoteli ya Mhalo beach Lodge iliyojengwa mwambao mwa fukwe za Mhalo.
Benado Lisambo ni Meneja wa Mhalo Beach Lodge anasema fukwe hizo zina maajabu ambayo hayawezi kupatikana sehemu nyingine hali ambayo inavutia wageni wengi wa ndani na nje ya nchi kufanya utalii na kupatahuduma zote zinazostahili kwa watalii.
Anakitaja kivutio kikubwa katika fukwe hizo kuwa ni mtalii anaweza kuona mipaka miwili ya nchi mbili za Malawi na Msumbiji kwa wakati mmoja jambo ambalo linawavutia watalii wengi wanaotembelea fukwe hizo.
“Sisi wilaya Nyasa tuna bahati sana,ukiwa hapa Mhalo beach ukiangalia kusini unaona milima ya nchi ya Msumbiji na ukiangalia Magharibi unaona milima ya nchi ya Malawi,wakati wa usiku unaweza kuona taa za magari katika nchi hizo kwa kweli inavutia sana’’,anasisitiza Lisambo.
Hata hivyo anasema fukwe yote ya Mhalo inavutia wageni wengi wa ndani na nje ya nchi kwa sababu haina uchafu,maji yake ni maangavu hali ambayo inamwezesha mtalii kuwaona samaki wanavyotembea ndani yamaji katika ziwa Nyasa.
Kulingana na Meneja huyo,toka fukwe ya Mhalo hadi mpakani na nchi ya Msumbiji ni umbali wa kilometa 30 na kwamba unaweza kusafiri kwa boti kupitia ziwa Nyasa na kwamba kusafiri kwa boti toka fukwe ya Mhalo hadi nchini Malawi ni safari ya saa sita.
Anawataja watalii ambao wametembelea fukwe za Mhalo kuwa wametoka nchi za Ujerumani, Italia, Uingereza, Marekani, Japan,Afrika ya Kusini,Malawi, Msumbiji, Zimbabwe na kwamba wanapokea pia watalii
wengi kutoka ndani ya nchi.
“Watalii wakifika hapa Mhalo beach kuna vivutio vingi, wanaweza kufanya utalii wa kuogelea,kupanda milima ya Livingstone, kutembea ufukweni kilometa mbili,kuona ngoma za asili mwambao mwa ziwa Nyasa, ikiwemo ngoma ya mganda,kioda na lindeku na kufanya safari za majini kwa kutumia boti’’,anasema Lisambo.
Joseph Ndomondo Mwongoza watalii Mkazi wa Liuli ziwa Nyasa anasema fukwe za ziwa Nyasa upande wa Tanzania ni bora zaidi kwa kuwa ni za asili ambazo zimetengenezwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe.
“Fukwe za ziwa Nyasa upande wa Malawi zimetengenezwa toka kingo za milima hivyo zimechimbwa hali ambayo inadhihirisha ubora wake hauwezi kulingana na fukwe za ziwa Nyasa upande wa Tanzania,’’anasema Domondo.
Afisa Maliasili na Utalii wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa Bugingo Bugingo anasema ziwa hilo limebarikiwa kuwa na fukwe nzuri za asili na zinazofaa kwa uwekezaji kwenye sekta ya utalii hivyo ametoa rai kwa wawekezaji kuwekeza ziwa Nyasa.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇