LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Oct 13, 2020

KUKAMILIKA KWA MRADI WA MAJI KWANUSURU NDOA ZA KINAMAMA MULEBA

Na Allawi  Kaboyo, Muleba.


Jamii ya Kitongoji cha Maizigela katika Kijiji cha Kiteme kilichopo katika Kata ya Kasharunga  Wilaya Muleba Mkoani Kagera wameishukuru na kuipongeza serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Magufuli kwa kazi kubwa ambayo imekuwa ikifanyika hasa katika miradi ya maji.


Wananchi hao wametoa shukrani hizo jana mbele ya Naibu katibu Mkuu  wa Wizaya ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba aliyefika katika Kitongojini hicho kukagua upatikanaji wa huduma ya maji pamoja na kukagua miradi mbalimbali ya maji.


Mkazi mmoja wa Kitongoji hicho, Paskazia Frolian alielezea kuishukuru serikali kwa kuweza kuwaboreshea mradi  wa maji uliokuwa  umekufa kwa miaka mingi na kuwasababishia wananchi kutembea umbali mrefu kwenda kufuata maji huku wakipanda milima na mabonde huku wakishindwa  kufanya kazi nyingine kutokana na uchovu.


“Kwanza niseme tu ukweli tunamshukuru Rais Magufuli kwa kutuangalia  na sisi wananchi  wa vijijini, sisi kina mama tulikuwa tukiteseka kufuata maji mbali, mtu unabeba dumu moja umechoka na huwezi kufanya kazi nyingine hata kuwahudumia waume zetu tulikuwa tukishindwa na wengine kutishiwa kuachwa, lakini kwa sasa maisha ni safi maji tunachota muda wowote.” alisema Paskazia.


Kwa upande wake mmoja wa mabalozi wa kitongoji hicho Vedasto Tindibaiyukao Tofiri alisema mradi huo umekuwa msaada mkubwa kwa wananchi  wa Kitongoji hicho pamoja na Wananchi wa Vitongoji jirani kutokana na utoaji wa maji kwa kipindi kirefu na kwa uhakika.


Amesema kuwa tangu anakuwa mradi huo aliukuta lakini kipindi hicho maji yalikuwa hayatoki kwa uhakika hali iliyokuwa ikiwapelekea wanawake wa kijiji na kitongoji hicho kuhangaika kutwa nzima wakitafuta maji na wengine kutumia gharama nyingi kununua maji kwa gharama ya kuanzia shilingi mia 300 hadi shilingi mia tano 500 kwa dumu la lita 20 ambapo kwa sasa wananchota maji hayo  kwa shilingi 50 kwa ndoo  ya lita 20.


Hata hivyo mwenyekiti wa jumuiya ya watumiaji maji Shaaban Juma ameeleza kuwa mradi huo umekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa kitongoji kizima ambapo amesema kuwa kwa kipindi cha miezi miwili tangu mradi  huo uanze kutoa maji, jamii tayari imechangia kiasi cha zaidi ya shilingi laki tatu kutokana na kununua maji.


Ameongeza kuwa awali ulipotambuishwa mradi huo alipata changamoto kubwa ya jamii kukataa kununua maji na kuendelea kuchota maji katika mito waliyoizoea na kuongeza kuwa baada ya kuwapatia elimu ya kutosha kwa kufanya mikutano mbalimbali sasa jamii imekuwa na muamko wa kuyatumia maji hayo ambayo amesema kuwa ni maji safi na salama.


Awali  akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa naibu katibu mkuu,  Jerome Patrick amesema kuwa kuwa mradi huo umegharimu kiasi cha shiingi milioni 48 katika ukarabati wake ambapo ulianza  kutoa maji tangu tarehe 15, mei mwaka huu ambapo hadi sasa unaendelea huku vikiwa vimejengwa vituo vya kuchotea maji 10.


Jerome amesema kuwa mradihuo chanzo chake ni chemichemi ambapo kwasasa kinahudumia zaidi ya watu 3500, ambapo amebainisha kuwa moja ya changamoto iliyokuwa ikisumbua ni uwepo wa vyanzo vya asili ambavyo wananchi walikuwa wakivitumia na kukataa kulipia maji.


Kwaupande wake naibu katibu mkuu wizara ya Maji ameupongeza uongozi wa RUWASA Mkoa wa Kagera pamoja na wilaya Muleba kwa kusimamia vyema miradi ya maji ambayo sasa imeanza kutoa matunda kwa wananchi walengwa.


Aidaha ameitaka jamii kuwa walinzi wa miradi hiyo kwa kuhakikisha inakuwa salama wakati wote ili iendelee kuwahudumia kwa kuhakikisha miundombinu yake haihujumiwi na kuharibiwa na watu ambao sio wazalendo na wenye nia hovu.


“Niwapongeze kwa kupata maji, ila niseme tu mradi huu sio wa serikali mradi huu ni wa kwenu hivyo kila mmoja wenu anawajibika kuwa mlizi hapa, tunataka na watoto hawa wakikuwa waukute mradi huu ukifanya kazi .” Amesisitiza Naibu katibu mkuu.


Hata hivyo meneja wa wakla wa maji mjini na vijijini RUWASA Mkoa wa Kagera Mhandisi Walioba Sanya amewaeleza wananchi hao kuwa waendelee kutumia maji hayo kwa kuchangia kwa kuwa fedha hiyo ya maji inabaki kwenye miliki yao ambayo wataweza kuitumia hata kufanyia marekebisho ya miundombinu pale itakapoonekeana kuharibika.

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba kakimtua ndoo ya maji mmoja wa wanawake baada ya kukagua mradi wa maji wa Maizigela Kata ya Kasharunga wilaya Muleba, jana.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages