MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Pombe Magufuli amepiga simu na kuwaomba wakazi wa Ushetu wampigie kura za kutosha ili awatumikie.
Ameongea nao leo jioni (Alhamisi, Oktoba mosi, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa Ushetu kupitia simu aliyompigia Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM, Kassim Majaliwa ambaye alikuwa akihutubia mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye uwanja wa Nyamilangano, wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.
“Watu wa Ushetu ninawashukuru sana kwa kumpitisha bila kupingwa Engineer Kuandikwa. Mimi niko Tunduma, nilitamani niwe hapo na ninyi lakini nimemtuma Waziri Mkuu aje kuniombea kura. Yote ambayo atazungumza Majaliwa nimemtuma mimi, nawatakia mkutano mwema,” amesema.
Alisema ahadi yake aliyoitoa ya kutengeneza barabara ya Ushetu-Kahama iko palepale na kwamba akimaliza uchaguzi atafika kuwatembelea. “Naikumbuka hiyo barabara ya Ushetu kwenda Kahama, tutaitengeneza kwa kiwango cha lami. Naomba kura zenu pamoja na madiwani wote wa CCM.”
Eng. Kwandikwa aliwataka wananchi wa Ushetu wamchague Rais Dk. Magufuli ili awaletee maendeleo katika nyanja mbalimbali zikiwemo huduma za afya, umeme, maji na barabara
Mheshimiwa Majaliwa ambaye amemaliza ziara yake ya siku moja mkoani Geita yuko Mkoa wa Shinyanga akiendelea kutafuta kura katika wilaya mbalimbali.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇