Mgombea Ubunge Jimbo la Kondoa Vijijini, Dk. Ashatu Kijaji akiomba kura zake, za Mgombea Urais wa CCM, Dk John Magufuli na madiwani katika Kata ya Thawi. |
Baadhi ya akina mama waliohudhuria kikao cha ndani katika Kata ya Kolo, Kondoa Mjini,
Okash akiomba kura kwa wagombea wa CCM huku akiwa amepiga magoti katika kampeni za CCM Kata ya Masenge Kondoa Vijijini.
Na Mwandishi Wetu, Kondoa.
MGOMBEA Ubunge Viti Maalumu Mkoa wa Dodoma kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Halima Okash amewasihi wananchi wa Jimbo la Kondoa Vijijini, kumpigia kura nyingi Mgombea Ubunge, Dk. Ashatu Kijaji ambaye amemfananisha thamani yake na madini ya dhahabu.
Akifanya kampeni za nguvu kwa wagombea wa CCM, katika Kata mbalimbali jimboni humo, Okash alisema wanaKondoa wasifanye makosa kuacha kumpigia kura Dk Kijaji kwani ni dhahabu ya kujivunia kwa uchapakazi wake serikalini na katika maendeleo ya jimbo hilo.
"Kondoa Vijijini mna dhahabu ya kujivunia ambayo ni Dk. Kijaji kiongozi mwanamke wa mfano, kwani amesimamia vema majukumu ya unaibu waziri wa Fedha na Mipango aliyopewa na Rais John Magufuli, na kulitendea haki kimaendeleo jimbo la Kondoa Vijijini," alisema Okash na kuwaomba wampigie kura ili aliongoze tena jimbo hilo kwa miaka mitano.
Akiwa katika kikao cha ndani katika Kata ya Masange, Okash, aliwaeleza wananchi wa Kondoa kuwa licha uchaguzi mkuu 2015, kuipatia CCM kura chache, lakini Rais John Magufuli hakuwatelekeza aliendelea kuwapelekea maendeleo, hivyo kuwataka Oktoba 28, kumuonesha shukrani kwa kumpatia kura za kutosha.
Katika kikao cha ndani Kata ya Kinyasi, Okash aliwaeleza wanawake mazuri yote yaliyofanywa na Serikali ya CCM ya Awamu ya Tano, hivyo kuwaomba Oktoba 28, kutokosa kumpigia Mgombea Urais wa CCM, Dk Magufuli Mgombea Ubunge Kondoa Vijijini, Dk. Kijaji na wagombea udiwani wa CCM.
Okash, alitaja baadhi ya mambo makubwa yaliyofanywa na yanayoendelea kutekelezwa Dodoma chini ya Uongozi wa Dk. Magufuli kuwa ni;Kukmilika kwa ujenzi wa barabara ya lami ya Dodoma- Manyara inayopita Kondoa, Ujenzi wa barabara za kisasa ikiwemo ya Pete (Ring Road) ya njia nne itakayozunguka jiji la Dodoma, ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR, Hospitali za kisasa ikiwemo ya Benjamin Mkapa, Soko la kisasa la Ndugai, Stendi ya kisasa ya mabasi na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato unaoanza kujengwa hivi karibuni. Pia ameahidi kujenga uwanja mkubwa wa kisasa wa michezo.
Akiwa katika Jimbo hilo la Kondoa Vijijini, Okash amefanya kampeni katika kata za; Bumbuta, Thawi, Masange, Kinyasi na Kata ya Kolo iliyopo katika Jimbo la Kondoa Mjini ambapo alimuombea kura Mgombea Ubunge wa jimbo hilo, Ally Makoa na Mgombea udiwani wa kata hiyo, Jumanne Mnyau pamoja na Mgombea Urais wa Tanzania kupitia CCM, Dk Magufuli.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇