Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa NHIF, Bernard Konga (kushoto) wakisaini mkataba wa uzinduzi wa Mpango wa DUNDULIZA kwa huduma za NHIF kupitia Benki ya NMB . Kulia ni Afisa Mkuu wa wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa NHIF, Bernard Konga (kushoto) wakibadilishana mkataba wa uzinduzi wa Mpango wa DUNDULIZA kwa huduma za NHIF kupitia Benki ya NMB . Kulia ni Afisa Mkuu wa wateja Binafsi na Biashara wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi.
Benki ya NMB na Mfuko wa Taifa wa Bima ya
Afya (NHIF) zimeweka historia mpya na
ya aina yake nchini kwa kuanzisha utaratibu wa kipekee wa bima ya afya utakaowawezesha wananchi wengi kupata huduma
hiyo kiurahisi na kwa nafuu kubwa kwa kuweka akiba kidogo kidogo kulingana na
vipato vyao.
Historia hiyo iliandikwa jijini Dar es
Salaam baada ya taasisi hizo mbili kuingia makubaliano ya kutekeleza mpango huo
ambao unatarajiwa kuwa na mchango mkubwa kwenye malengo ya taifa ya kuboresha
rasilimali afya na upatikanaji wa tiba.
Mpango huo mahsusi wa huduma ya afya kwa
wote ujulikanayo kwa jina la DUNDULIZA ulizinduliwa katika hafla iliyofanyika
PSSSF Complex na kuhudhuriwa na viongozi na wafanyakazi wa taasisi hizo mbili
pamoja na wadau mbalimbali.
Wakizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa
Mtendaji Mkuu wa NMB, Bi Ruth Zaipuna, na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bw. Bernard
Konga,walisema ukubwa wa mtandao wa huduma wa benki hiyo utasaidia sana
kuipeleka DUNDULIZA kwa Watanzania hasa wale wa kawaida kama wakulima na
wajasiliamali. Pia walisema kuwa huduma hiyo mpya itakuwa na mchango mkubwa
katika mipango ya serikali ya kuhakikisha afya bora kwa Watanzania wote kupitia
bima ya afya.
“NHIF wanapoingia makubaliano nasi, maana yake
wataweza kuwafikia Watanzania wote kila pembe ya nchi hii kutokana na mtandao
wetu mpana wa matawi na hata mtandao wa wakala wetu ambao ni wawakilishi katika
huduma za kifedha. NMB ina matawi 227 na ipo katika kila wilaya na baadhi ya
kata hapa nchini huku tukiwa na wakala wa benki (NMB Wakala) zaidi ya 7,000,”
Bi Zaipuna aliongeza.
Kuhusu DUNDULIZA, alisema ni mpango
unaomwezesha mwananchi kujiwekea akiba ya fedha kidogo
kidogo za michango kwa ajili bima yake ya afya na hata wategemezi kupitia Benki
ya NMB. Kwa utaratibu huu, alifafanua, mtu ataweza kufanikisha kuchangia
mojawapo ya vifurushi vya bima ya afya vinavyotolewa na NHIF ambavyo ni Najali
Afya, Wekeza Afya na Timiza Afya.
Kwa mujibu wa Bi. Zaipuna, Benki ya NMB
imeamua kuwekeza katika mpango wa DUNDULIZA na kushirikiana na NHIF
kuufanikisha kwa sababu afya bora ni mtaji kwao kama taasisi ya kifedha.
Alisema upatikanaji wa tiba kwa kutumia bima ya afya badala ya akiba
zilizowekwa benki ni swala la msingi si kwao tu lakini pia kwa wateja na
wananchi kwa ujumla.
“Huu ni mpango wa kwanza na wa aina yake
kutokea hapa nchini na tunafurahia kuwa wa kwanza kuweka historia hii ya
kushirikiana na Serikali kupitia NHIF katika kuboresha huduma ya afya kwa
Watanzania. Utaratibu huu pamoja na kupata bima ya
afya pia unamjengea mwananchi utamaduni wa kujiwekea akiba kwa kutimiza
malengo mbalimbali,” Bi Zaipuna alifafanua.
Mkurugenzi Mkuu wa NHIF alisema kuwa
wakati NHIF inazindua mpango wa vifurushi Novemba mwaka jana, changamoto
iliyoonekana ni pamoja na uwezo wa wananchi kulipa fedha zote kwa awamu moja
hatua iliyoifanya menejimenti ya mfuko huo kufungua milango na kuanza
kushirikiana na wadau wa taasisi za kifedha kama Benki ya NMB ambayo ililipokea
wazo la DUNDULIZA na kulifanyia kazi haraka.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇