Na Mwandish Wetu, Migori.
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Isimani kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM), William Lukuvi, amemuomba Mgombea Urais wa Tanzania kupitia chama hicho, Dk John Magufuli katika mipango yake akishinda urais, alifikirie jimbo hilo kuwa wilaya.
Lukuvi ambaye amesifiwa na Rais Magufuli kuwa ni mchapakazi na kuwaomba wananchi wampigie kura awe naye katika kipindi cha miaka mingine mitano, alilitoa ombi hilo wakati Dk Magufuli alipofanya mkutano wa kampeni juzi eneo la Migori, Isimani akitokea Dodoma kwenda Iringa kuendelea na kampeni,
Mgombea huyo wa Jimbo la Isimani, ambaye pia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, alisema kuwa kijiografia jimbo hilo lenye ukubwa wa kilomita za ukubwa 17000 ni kubwa kuliko wilaya zote za Mkoa wa Iringa wenye jumla ya Kilomita za ukubwa 35000, hivyo inawawia vigumu wananchi kufuata huduma muhimu makao makuu ya wilaya yaliyo umbali wa Km 125.
Amesema kwa umuhimu huo, ndiyo maana uongozi wa Mkoa wa Iringa, uliamua Hospitali ya Wilaya ijengwe Migori, Isimani ili kuwapunguzia kero wananchi wa jimbo hilo.
"Wananchi wa Isimani wanakupenda sana. kwa kipindi cha miaka mitano umewafanyia mambo mengi. kipindi chako umewaletea mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya sh. bil 1.6 na tayari umekamilika na maji yatasambazwa katika maeneo mengine ya jimbo hilo,"amesema Lukuvi.
Ametaja miradi mingine iliyokamilika kuwa umeme wa REA, katika vijiji 60 vya Jimbo hilo tayari isipokuwa vijiji vitatu tu. Elimu bure sh.bil. 16, barabara sh.bil. 60. Tasaf bil. 3.3. Mradi wa kisima Izasi mil. 800 . "Hayo ni machache uliyotufanyia Dk Magufuli, tunakuombea uhai mwema, afya njema na wananchi wa Migori wanasema watakupa kura."
"Mzee jimbo la Isimani unalijua sana ulikuja Pawaga, Iringa Mkoa wote una kilomita za ukubwa 35000, Isimani ni kubwa kuliko wilaya zote ina Kilomita za ukubwa 17000, na ilitoke kona ya tarafa moja uwafuate akina Kasesera (Mkuu wa Wilaya ya Iringa) ni umbali wa Kilomita 125. kwa hiyo ili utawala uwe mzuri, tungeomba kwa jiografia hiyo utupatie wilaya," aliomba kwa lugha ya unyenyekevu.
Akizungumza katika mkutano huo, Dk Magufuli alimmwagia sifa lukuki Lukuvi na kuwaomba wananchi kumpigia kura nyingi ili katika awamu nyingine ya miaka mitano amalizie naye kazi.
"Lukuvi namfahamu sana tuliingia wote wakati wa Mkapa, wote tuliteuliwa kuwa manaibu waziri, inawezekana mimi namfahamu zaidi hata kuliko nyie. Alikuwa ananisumbua sana kutengeneza barabara ya Mbuga ya Ruaha ambayo ni kubwa kuliko zingine. Nileteeni Lukuvi, nifanye naye kazi ili miaka mitano nimalize naye, kama mnanipenda nipeni Lukuvi,"alisema Dk Magufuli huku akishangiliwa na umati mkubwa wa watu katika mkutano huo.
"Mbunge wenu amezungumza mengi nimeyabeba, nasema nimeyabeba, mniachie. ila nawataka muendelee kudumisha mshikamano msije mkabaguana mjenge umoja kama aliouacha Nyerere. Msigawanywe kwenye majimbo kama pesa."
Dk. Magufuli amesema endapo akichaguliwa yeye, Lukuvi na madiwani wa CCM, ameahidi kuzitafutia ufumbuzi baadhi ya changamaoto kwa kumalizia uwekaji umeme katika vijiji vitatu vilivyobakia kati vijiji 60 vya jimbo hilo ambapo tayari vijiji 57 vimepatiwa. Pia miradi ya afya na maji itakamilishwa.
"Nawaomba Oktoba 28, mnipe kura zenu zote, mpeni Kura Lukuvi na madiwani wote wa CCM,"alimalizia kusema Dk. Magufuli huku akiaga tayari kwa safari ya kwenda Mjini Iringa kuendelea na kampeni.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇