Katibu wa CCM mkoa wa Morogoro, Shaka Hamdu Shaka
Na Mwandishi Maalum, Morogoro
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM)Mkoa wa Morogoro kimesema Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Maalim seif Sharif Hamad hana uwezo wa kuiunganisha Zanzibari kwani hana historia safi na aina ya siasa na uongozi wake hulenga kuwagawa wananchi.
Hayo yameelezwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Morogoro Shaka Hamdu Shaka akiwa ofisini kwake mkoani hapa baada ya matamshi ya Maalim Seif aliyesema akishinda atawaunganisha wananchi wa visiwa vya Unguaja na Pemba .
Shaka alisema kabla ya Maalim Seif kuwa Kiongozi wa SMZ na CCM Zanzibar haikuwa na msamiati wa Unguja na Upemba lakini toka ateuliwa kuwa Waziri wa Elimu na baadae Waziri Kiongozi SMZ, hapo ndipo misamiati ya upemba na uunguja ilipochipuka na kutamalaki kutokana na aina ya uongozi wake wa kibaguzi.
Alisema hapo zamani ukimsikia muunguja anamwita mtu mpemba au mpemba anamwita rafiki yake muunguja, ulikiwa ni sehemu ya utani na dhihaka isio na gharama lakini haukuwa na makali kama aliposhika nyadhifa za juu Maalim Seif.
"Si kweli kama Maalim Seif ana uwezo wa kuwaunganisha wazanzibari kama anavyojitapa .Umahiri na uwezo wake katika upinzani ni kuwagawa wananchi kwa asili, nasaba na rangi zao.Ni kiongozi mbaguzi, mbinafsi mwenye uwezo wa kuwagawa watu kwa mafungu "Alisema shaka
Alieleza ili kumjua kiongozi hiyo si mpenda umoja bali anachokitamani ni siasa za mvurugano na mgawanyiko, ameshagombana takriban na viongozi wote wa juu wakati wa chama kimoja akiwemo Hayati Mzee Aboud Jumbe ,Mzee Idris Abdul Wakil, Mzee Ramadhan Haji Fakhi na marehmu baba wa Taifa Mwalimu Julius Myerere.
"Maalim Seif alipotaka kuanza siasa baada ya ujio wa vyama vingi kwanza alikwenda msasani kumuomba radhi mwalimu Nyerere .Siri hii haisemi kwakuwa alijua ana sifa ya ukabila na nasaba jambo ambalo lilipingwa vikali na uongozi wa mwalimu "Alisema shaka
Katibu huyo wa mkoa alisema hata hayati Mzee Hasan Nassor Moyo alivurugana naye wakati alipokuwa waziri wa kilimo huku maalim seif akiwa waziri kiongozi alimtishia kumpandisha kizimbani kwa madai alihusika na ubadhirifu katika shamba la smz lililoko Makurunge wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani .
"Urafiki kati ya Maalim Seif na mzee Moyo uliibuka wakati wa kuundwa Serikali ya Umoja wa kitaifa.Kama si busara za Dk Amani Karume, mzee moyo angekufa akiwa mfundo dhidi ya Maalim Seif. Ndiyo maana hata kwenye mazishi ya mzee jumbe alikataa kumsalimia Rais Dk Ali Mohamed Shein kwakuwa ana kinyongo" Alisema shaka
Shaka alisema ikiwa Maalim Sief alifukuzwa CCM kutokana na tishio la kuigawa CCM na viongoizi wake , katu hawezi kuwaunganisha wananchi zanzibar ili wawe wamoja wanaopendana, kuthaminiana na kuishi pamoja kama anavyojigamba wakati huu kuelekea uchaguzi mkuu.
"Ana maadui wengi wanaompinga kwa hoja za msingi toka akiwa ccm hadi cuf na sasa amehamia Act wazalando. Kitendo cha kutoka kwake CUF kwenda ACT Wazalando amewagawa hata wananachi huko Pemba. Siasa zake chafu zimewagawa hadi wananchi katika majimbo mbali ya Unguja na kuwa mafungu mafungu hadi leo wakiwa hawaelewi mustakabali wao lakini wanafanya kufunika kombe mwanaharamu" Alieleza shaka
Shaka alikumbushia juhudi zilizochukuliwa na viongozi wa CCM kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa zanzibar na kwakuwa maalim seif ni mpenda madaraka na vyeo, ndiye aliyekuwa chanzo cha kuigawa serikali hiyo kwa kutoa siri za smz kwenye mikutano ya hadhara ya CUF.
Hata hivyo Shaka alisema Maalim Seif ikiwa amegombana na mwalimu wake hayati mzee Jumbe hayati Mzee Juma Ngwali na Hamad Rashid mohamed ni ukweli uliowazi kuwa hawezi kuwaunganisha wananchi na ushuhuda wa hayo ni kitendo cha kugombana na wenziwe wa karibu na wasiri wake wakubwa akina Mussa Haji kombo, Juma Othman na Abass Muhunzi hawezi kupatana na mtu mwingine maishani mwake na wala hana uwezo wa kumuunganisha hata kuku ili wale nafaka pamoja.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇