Dar es Salaam.
Mtumishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyekuwa akifanyakazi katika Jumuiya ya CCM ya Umoja wa Wazazi Tanzania Kamanda, Ally Debwani (Pichani), amefariki Dunia jana jioni nyumbani kwao mtaa wa Ludewa, Kata ya Makumla, Ubungo Dar es Salaam.
Akizungumza na Wafanyakazi wa Jumuiya ya Wazazi waluofika msibani kutoa pole wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Erasto Sima, Mdogo wa Marehemu, Said Debwani, alisema jana Jumapili Kamanda Ally, alikuwa mazingira ya nyumbani kwa muda mrefu kibarazani muda mwingi akisikiliza radio yake.
Said alisema ilipofika alasiri akaanza kubandika mabango ya Rais Dk. Magufuli na Mgombea Ubunge Jimbo la Ubungo, Profesa Mkumbo, Baada ya kumaliza alikaa chini alipotaka kusimama akashindwa akaanguka hakuamka hadi umauti unamkuta wakiwa njiani kumpeleka hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu.
"Jana Kaka Kamanda Ally mda mwingi alikuwa mazingira ya nyumbani tena alikaa hapa kibarazani ilipofika saa tisa alasiri akiwa na radio yake anasikiliza nyimbo mbalimbali zikiwemo nyimbo za CCM alichukua mabango ya Mgombea wa Urais kupitia tiketi ya CCM, Dk. John Joseph Magufuli.
Wakati Kaka Ally akiendelea na kubandika mabango alipita muuza ndizi akanunua akala na nyingine akawagawia watoto aliokuwa nao hapo kibarazani" Alisema Said.
Taarifa ya awali kutoka kwa ndugu wa marehemu, Kamanda Ally, walisema miaka mitano iliyopita Kamanda Ally alipatwa na tatizo la kuishiwa nguvu na kuzimia hali hiyo ilipotea Ila kipindi cha hivi karibuni hali hiyo ilikuwa ikimtokea tena mara kwa mara na humpeleka hospitali kwa matibabu ya huduma ya kwanza na kupatiwa dawa za kutumia.
Marehemu Kamanda Ally ameacha watoto wawili wa kike, Khadija Ally Debwani na Asma Ally Debwani, Mazishi yake yanatarajiwa kufanyika kesho, saa saba mchana katika makaburi ya Kimamba Old Traford yaliyopo Mtaa wa Ludewa, Kata ya Makumla, Wilayani Ubungo, Jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇