LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 29, 2020

KAMPENI ZA CCM ZINAZOONGOZWA NA MGOMBEA URAIS DK MAGUFULI ZARINDIMA MAKAMBAKO, NJOMBE

 

Mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi CCM Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na wananchi wa Makambako mkoani Njombe katika Mkutano wa Kampeni wa CCM leo tarehe 29 Septemba 2020 Makambako mjini

Sehemu ya Wananchi wa Makambako waliohudhuria mkutano wa Kampeni wa Mgombea Urais kupitia Chama cha Mapinduzi CCM Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 29 Septemba 2020 Makambako mjini.





DK MAGUFULI AMEAHIDI KUJENGA UWANJA WA NDEGE WA LAMI NJOMBE


MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM), Dk.John Magufuli amesema katika miaka mitano ijayo Serikali inatarajia kuujenga kwa lami Uwanja wa Ndege Mkoa wa Njombe ili ndege zinapotua ziweze kubeba mazao mbalimbali yakiwemo ya Chai na Parachichi na kisha kupelekwa Ulaya yakitokea hapa.

Akizungumza leo Septemba 29, 2020 mbele ya wananchi wa Mkoa wa Njombe akiwa katika mkutano wake wa kampeni za kuomba ridhaa ili apewe tena miaka mitano mingine kuongoza nchini, Dk.Magufuli amesema Uwanja wa Ndege wa Njombe utakapojengwa kwa lami utafungua fursa ya ndege kutua na kubeba mazao yanayolipwa katika mkoa huo.

"Mkoa wa Njombe ni maarufu kwa kilimo cha parachichi na hata chai, tunataka ndege iwe inaruka kutoka hapa kwenda London.Tunataka Tanzania iwe kama Ulaya, naomba mniamini, tunataka kuisuka nchi hii Wazungu wakija washangae, ndio maana ndani ya kipindi cha miaka mitano tumetoka kuwa masikini wa kutupwa hadi uchumi wa kati., hii ndio sadaka yangu kwa Watanzania , hii ndio sadaka kwa wana Njombe,"amesema Dk.Magufuli.

Pia amesema katika kuufungua mkoa huo kwa miundombinu ya usafiri Ilani ya Uchaguzi Mkuu mwaka 2020 inaeleza wazi mkakati wa kununua vichwa saba vya treni pamoja na mabehewa 21 kwa ajili ya reli ya TAZARA na hivyo kurahisisha usafiri wa treni katika mkoa huo.

Dk.Magufuli amesisitiza wataboresha bandari ya Manda ili kurahisisha usafiri katika Ziwa Nyasa"Kama mnavyofahamu tumejenga meli mpya tatu Ziwa Nyasa kwa gharama ya Sh.bilioni 20.4. Tunatak meli hizo ziwe zinakwenda hadi Manda. Pia tumepanga kufikisha umeme katika vijiji vyote 91 ambavyo vimebakia katika Mkoa wa Njombe.

"Tunataka pia kuzalisha mewagati 580 za umeme ambazo zitatoka Mkoa wa njombe kupitia mradi wa umeme Rumakali pamoja na mradi wa Ruhuji. Mkakati wetu tunataka tuwe na umeme wa kutosha ambao utauzwa kwa bei ya chini na ikiwezekana tuuze umeme hadi nje ya nchi yetu, ndio mana tuna mradi wa umeme wa Bwawa la Julius Nyerere ambao ume wake utaunganishwa katika gridi ya Taifa na kutumika kote nchini,"amesema Dk.Magufuli na kuongeza kuwa kuna mkakati wa kukiendeleza Kiwanda cha Chai Lupembe ili wakulima wa zao hilo wawe na uhakika wa soko la chai.

Pamoja na hayo Dk.Magufuli amefafanua kwa kina mafanikio ambayo yamepatikana katika katika Mkoa wa Njombe katika kipindi cha miaka mitano iliyopita."Leo nataka kujikita kwa kuelezea machache, kwanza nimekuja kuomba kura kwasababu mbili, kwanza kwa kuweza kutekeleza ahadi zetu kwa kipindi kilichopita. Hiyo ndio sababu ya kuwaomba kura na pili tumekuja kuomba kura kwasababu kuna mipango mizuri ya kuendelea kuongoza nchi na hatimaye kuleta maendeleo.Njombe wanajua tulikotoka , tuliko na tunakokwenda , hivyo tumekuja kuomba tena kura.

"Katika kipindi cha miaka mitano, nataka nitaje mafanikio machache tu, kwa Mkoa wa Njombe tumetumia Sh.bilioni 498.76 kwa ajili ya ujenzi wa barabara.Leo Njombe hakuna tatizo katika kusafiri hata wakati wa msimu wa mvua hakuna tatizo,"amesema Dk.Magufuli na kuongeza wamejenga soko la kisasa pamoja na na stendi kuu.

Pia amesema wametumia Sh.bilioni 41.1 kuimarisha huduma za afya, ikiwemo kujenga hospitali ya rufaa ya mkoa,hospitali tatu za wilaya, kujenga na kukarabati vituo 18 vya afya, zahanati 34, kujenga nyumba za watumishi na kwamba uwekezaji huo umesaidia kupunguza vifo vya akina mama kutoka wastani wa vifo 32 kwa mwaka hadi vifo 14 kwa mwaka.

"Usione vyaelea vimuendwa na waundaji ni Serikali ya CCM, haya mabarabara na hospitali wanaotumia sio wa CCM tu bali ni watu wote.Shilingi bilioni 44.18 zimetumika kwa ajili ya kuboresha na kupanua wigo wa elimu na katika elimu bure zimetumika Sh.bilioni 21 na Sh. bilioni 22.169 zimetumika katika ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu.Ndio maana tumekuja tena kuomba kura.

"Tumetekeleza miradi 84 ya maji kwa gharama ya Sh.bilioni 24.58 na hiyo imefanya hali ya upatikanaji maji miji kufikia asilimia silimia 84 kwa mijini na asilimia 72 kwa vijijini.Haya maji yakipatikana hayabagui, kwamba ukienda kufungua bomba yanatoka kwa wana CCM tu na kwa Chadema hayatoki hapana wote wanakunywa, hata ng’ombe zetu wanakunywa.

"Tumefikisha umeme kwenye vijiji 290 , kati ya vijiji 381 sawa na asilimia 76, vimebaki vijiji 91 tu ili kwenda kumalizia kwa hapa Njombe, tunajua fedha ziko wapi, makandarasi wako wapi, umeme utakuwa wa watanzania wote, ndio maana nawaomba mwaka huu tutakapokuwa tunachagua watu wa vyama vyote wa watanzania tuangalie maendeleo, tuasiangalie vyama vyetu na katika kuangalia maendeleo mimi Rais wa CCM nitafurahi nikipata wabunge wa CCM, madiwani wa CCM,"amesema Dk.Magufuli.

Amesisitiza ndio maana wamebakisha vijiji 91kupata umeme huku akifafanua wakatati wanaingia madarakani vijiji vyenye umeme vilikuwa 2018 na katika kipindi cha miaka mitano ambavyo vimepata umeme ni 9,700 vikiwemo vijiji vya Mkoa wa Njombe, Tanzania nzima vimebaki vijiji 2,500 na kwa Njombe vibaki vijiji 91, ndio maana anaomba kura ili akamalizie hilo deni na kwamba anataka kuitengeneza Tanzania mpya.

Hata hivyo amesema katika miaka mitano ijayo iwapo watapata ridhaa ya kuongoza nchi, wanataka kuendelea kuimarisha huduma za kijamii na hasa maji, elimu na afya."Kwa Mkoa wa Njombe miradi mitatu yenye thamani Sh.bilioni 121, tumezipanga kuzitela hapa kwa ajili ya kushughulikia maji, kwa Makambako Sh.bilioni 42 na Wangingombe Sh.bilioni 50.Njombe nimekuja kueleza habari hizi nzuri.Pia tutaendelea kutekeleza miradi midogo midogo ya maji.Kwa upande wa elimu tutaendelea kutoa elimu bila malipo, tutakamilisha Chuo cha Ufundi VETA ili vijana waweze kupata mafunzo ya ufundi".

Kuhusu afya, Dk.Magufuli amesema watakamilisha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 85 na watajenga barabara yenye urefu wa kilometa nne inayokwenda katika hospitali hiyo huku akifafanua kuwa hospitali ya Wilaya zitaimarishwa ikiwemo kupatiwa vifaa vya kwa ajili ya upasuaji, ili watu wasihangaike kwenda Iringa.Pia hawataki kuona akinana wanapoteza maisha wakati wanaweza kuwanusuru.

"Tumejipanga pia kutengeneza uratatibu mzuri wa kuhakikisha wana Njombe na Watanzania wanapata bima ya afya, na ili uwe na bima ya afya lazima uboreshe miundombinu ya huduma za afya kwa kujenga hospitali za rufaa, hospitali za mikoa, hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati.Tumeongeza bajeti ya dawa na ukweli huwezi kupeleka bima ya afya wakati hakuna hospitali za mikoa , wilaya na rufaa.Pia tumejitahidi kuwahudumia wazee na watoto kwa kuwapatia huduma za afya bure,"amesema Dk.Magufuli.

Ametumia nafasi hiyo kusisitiza kuwa wataendelea na ujenzi wa miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Njombe na ndio maana wamekuja tena kuomba kura kwasababu wanafahamu mikakati, mbinu, hawahitaji fedha kutoka nje, fedha ziko hapa hapa,wamewabana mafisadi na fedha zinakwenda kwa wananchi.

Imeandikwa na Said  Mwishehe wa Michuzi TV

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages